HIVI NDIVYO VILIVYOTUFIKISHA HAPA.
Na Allan Albert Ferdinand Mirrupi Mseppa
+255(0)759454787
- allanmseppa@gmail.com
- Nianze kwa kuwashukuru wote walionipigia na kuniandikia ujumbe mfupi wa maandishi kupitia simu za kiganjani kwa kuwa hawa walikuwa wengi sana na hadi hivi sasa ninaposhika kalamu yangu kuandika makala hii, bado naendelea kupokea jumbe za watu mbalimbali. Ni kuhusu makala yangu katika gazeti hili toleo lililopita namba 543 la Februari 21-25, 2018 katika safu ya NASAHA ZA WIKI iliyosomeka HOJA TATA NA DHAIFU ZA PASCAL MAYALLA.
- Nianze kwa kuzigawanya jumbe nilizotumiwa kama ifuatavyo, Mosi nilitumiwa jumbe za kuniponda, kejeli, dharau, dhihaka na hata wengine wakaenda mbali zaidi kwa kunitukana, ambapo baadhi yao waliniandikia kuwa kwa kuandika makala ile nimeonekana sio mzalendo, hivyo nimewaudhi sana kwani ninachangia kuwarudisha nyuma kwa kuua vyama vyao wakati wenyewe wanatumia juhudi kubwa, nguvu nyingi, akili ya ziada na hata kulazimisha inapobidi ili wakamate dola, binafsi sina hakika kama ninaweza kuwa na mchango kati ya hayo wasemayo. Pili ni kwa walionipongeza na kunitia moyo hususan kwa ndugu aliyejitambulisha kwa majina ya J. Kassera, pia yupo mwenye namba inayoishia na 533 na wengine wengi ambapo nikiwaorodhesha safu yangu inaweza kujaa watu hao tu. Tatu ni wale waliokuwa katikati, hawa hawakutaka kukaa upande wowote ispokuwa wanataka baadhi ya mambo yafanyike ili nchi isonge mbele, mmoja wapo ni mwenye namba inayoishia na 032 na mwingine aliyenipigia simu na kujitambulisha kama Baba Robi wa Manzese.
- Na hapa nakiri wazi wazi, kati ya wote waliowasiliana nami wengi zaidi ni walionipongeza, katika jumbe za watu 137, jumbe 91 ni za walionipongeza, zikifuatiwa 33 za walionipinga na 13 ambao hawakuegemea upande wowote.
- Mzee wangu huyu Baba Robi wa Manzese aliyekuwepo toka enzi za kupigania uhuru, na kwa namna anavyoiangalia nchi kwa sasa na Afrika kwa ujumla inaonekana amekata tamaa kabisa, hii imetokana na kuona jinsi nchi yetu ilivyokirimiwa rasilimali za kila namna na Mwenezi Mungu lakini zikaendelea kutumika vibaya na kusababisha umaskini mkubwa kwa watu wake. Baada ya kushauriana naye kwa takriban dakika kumi na ushee akafikia kuamua kuwa ataihifadhi namba yangu kwa muda wa miaka kumi na akasisitiza tuombeane uzima kwa Mungu ili muda ukiwadia anishushue ikiwa nchi itakuwa bado ikisuasua kimaendeleo, nami kwa kuamini juhudi za Mh. Rais Magufuli katika hali ya kujiamini nikathubutu kumkubalia.
- Moja ya mambo yanayomkera mzee huyu ni kwanini katika miaka ya sitini Tanganyika ilikuwa sawa kimaendeleo na baadhi ya nchi za Asia kama Vietnam na Korea Kusini, kwanini leo hii wametuacha kwa mbali
- Jibu langu lilikuwa ni rahisi tu, kwamba tumefikishwa hapa tulipo kutokana na mambo makubwa mawili, Mosi ni kutokana na nchi za magharibi kupitia mgongo wa Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Pili ni kukosekana kwa uzalendo wa kweli kwa watu wa nchi yetu ambapo baadhi ya wasaliti wachache walitumia nafasi zao katika kujitajirisha wao, familia zao na washirika wao wa karibu.
- Kutokana na mapinduzi ya viwanda barani Ulaya, wazungu walihaha huku na kule kutafuta wapi watapata kuwekeza, watendakazi rahisi (cheap labourers), rasilimali vitu (malighafi) na uwekezaji mwingine kwa minajili ya kujinufaisha wao na nchi zao, walianza kunyemelea bara la Afrika kupitia watu kama Vasco Dagama na wapelelezi wengineo. Ndio chanzo cha makampuni makubwa yenye ukwasi wa kutosha yalipozishawishi serikali za nchi zao kuiangalia Afrika kimaslahi zaidi, na ili kuhepuka migongano baina ya wakubwa hawa mara moja na bila kuchelewa ukaitishwa mkutano mkubwa jijini Berlin Ujerumani mwaka 1884/85 kwa ajili ya kuligawana bara la Afrika.
- Hapo ndipo Mfalme Leopold wa Ubelgiji alipojihalalishia nchi ya Congo kwa kupora ardhi, dhahabu na rasilimali nyingine nyingi, Mjerumani alitutwaa Watanganyika mpaka anafurushwa na Mwingereza na tunakuwa chini ya uangalizi wa Mwingereza kwa ridhaa ya Umoja wa Mataifa, alipewa jukumu la uangalizi hadi tutakapopata uwezo wa kujitawala wenyewe. Kwa hiyo wakati nchi za Kiafrika zinagangamala kupigania kujitawala kwa kupata uhuru kamili, tayari wazungu na waarabu walikuwa wameishatuumiza sana, wametunyonya sana, wametudhalilisha sana, wametuua sana, wametudhulumu rasilimali zetu sana na kutusababishia athari kubwa.
- Kwa mchango wa wazalendo wengi waliofanikisha kuanzisha, kuendeleza na kufikia tamati ya kupata uhuru wetu Disemba 9, 1961 nitataja wachache, Mshume Kiyate, John Rupia, Bibi Titi Mohammed, Mwl. Julius Nyerere, Sir George Kahama na wengineo. Baada ya kupewa uhuru wetu, wazungu waliondoka kwa shingo upande kwani waliamua kubadili mfumo wa kututawala ambao ni ukoloni mamboleo (neo-colonialism), aina hii ya ukoloni ndio fupa linaloendelea kutuhangaisha hata leo, ni katika kuhakikisha wanaendelea kututawala kiuchumi, kifikra na kisiasa kwa maslahi yao na nchi zao.
- Ili kujua tunaelekea wapi kama taifa Mwalimu akatangaza adui mwingine tena hatari kuliko wakoloni wenyewe ambao ni Ujinga, Umaskini na Maradhi. Aprili 26, 1964 muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Ndipo kwa niaba ya wananchi, Mwalimu akaanza kutaifisha shule za kimisioni na kuzifanya za Jamhuri ili watoto wa wazalendo wapate fursa ya kusoma ambapo kabla hawakupata nafasi hiyo hata elimu ya watu wazima. Mwaka 1967 likatangazwa Azimio la Arusha likiwa na watetezi kama mwalimu, Kingunge na wengine. Iliwekwa miiko ya uongozi kama kutokuwa na nyumba ya kupangisha, mshahara zaidi ya mmoja na mambo mengine kama hayo, lengo lake ni kujenga usawa wa watu, kujenga uchumi na kujitegemea, ili kuogopa kuwa ombaomba wa wazungu. Lakini Azimio la Arusha lilipingwa kwa chinichini na mabepari kwa kumuogopa mwalimu kwa kuwa walijua alikuwa mjamaa.
- Mwaka 1978/79 tukapigana vita vya Kagera dhidi ya utawala wa fashisti Iddi Amin na tukamshinda, lakini vita ile haikutuacha salama hata kidogo ndipo Septemba 1979 katika uwanja wa taifa (sasa uhuru) Dar Es Salaam, mwalimu alipotangaza miezi kumi na nane (18) ya kujifunga mkwiji kutokana na hali ngumu ya maisha, uchumi wa nchi ulitetereka sana, njaa ikawa kubwa (kumbuka ugali wa yanga), bidhaa zikahadimika, madawa, nguo nk
- Watu walipanga foleni kukunua bidhaa kama sukari, tena ni sheria kwa mathalan kilo moja kwa kila mtu, watu walipanga foleni kwa muda mrefu. Huduma za maji zilikuwa mbali, mama zetu walikuwa wakifunga safari kwenda kuchota maji, ili mradi kero tupu. Hapo sasa nchi za magharibi zikaona Tanzania imeisha dhoofika, kupitia mashirika yao ya kifedha ya Benki ya Dunia na IMF wakaitaka Tanzania iachane na sera za kijamaa ili iingie kwenye mfumo wa kibepari wa soko huria (mwenye mtaji ndiye mwenye kuamua), kushusha sarafu thamani na hapo ndio wakawa wamemtibua mwalimu na akasema hayuko tayari kugeuka jiwe dhidi ya msimamo wake. Mwalimu alijua ikiwa ataruhusu basi ataua viwanda vyetu wenyewe vya Mwatex, Urafiki, ZZK, Nyuzi nk. Kitu ambacho kilikuwa ni sahihi, kwamaana vilikuja kufa vyote.
- Hali ilikuwa sio ya kuridhisha ikafikia wakati wa miaka ya themanini tukatangaza vita vya uhujumu uchumi chini ya dereva wake waziri mkuu Edward Moringe Sokoine, watu walichimbia fedha, wengine walizitupa na vitu vingine vingi vilibainika ambavyo vilifichwa ili kuwepo na uhaba. Hadi Nyerere anaondoka mwaka 1985, nchi hizi za magharibi zilikuwa zimemshika pabaya, mambo yalikuwa hayaendi. Ndipo Rais Mwinyi alipoingia na kuamua kujipeleka mwenyewe majuu kwenda kusalimu amri dhidi ya matakwa ya hao mabwana wakubwa wasio na soni wala nia njema. Hatimaye wakauwa viwanda vyetu, sarafu yetu ikashuka thamani na sera zetu pia zikashindikana kutekelezeka, mfano Siasa ni Kilimo, matabaka yakapiga hodi, hali kadhalika unyonyaji, uonevu, unyanyasaji na kila aina ya roho mbaya na vitimbi vya hapa na pale.
- Sababu ya pili ni sisi waafrika wenyewe kutokuwa wazalendo, tumekuwa wa kujipenda wenyewe kuliko taifa, viongozi wa kiafrika wamekuwa na kasumba inayofanana, wanapopambana kuingia madarakani wanakuwa wapole, wanyenyekevu na wenye bashasha kubwa kwa watu wao. Haijalishi ni njia ipi aliyoitumia kuingia ofisini, iwe kupitia sanduku la kura ama mapinduzi matukufu, kosa tu ni pale anapoonja radha ya madaraka, hali inabadilika, nchi inamtumikia yeye badala ya yeye kuitumikia nchi. Leo hii ni Afrika pekee ambapo madikteta ni wengi hapana mfano, ni Afrika pekee ndipo wanapatikana viongozi wapenda kusalia madarakani na wasiotaka kutolewa kwa njia ya sanduku la kura, ni Afrika pekee ambapo madaraka ni sehemu ya kujipatia utajiri haramu, ni Afrika pekee ambapo gepu la walionacho na wasionacho ni kubwa lisilomfanoe, ni Afrika pekee ambapo ufisadi ni sehemu ya ufahari na ni Afrika pekee haki ya mtu inashindwa kwa fedha, uonevu hadharani, kudhulumiwa hadharani, umasikini wa kutupwa, elimu duni, matumizi holela ya madawa ya kulevya, kubakana kweupe, maradhi ya kila aina nk
- Nitoe mifano michache ya madikteta na wenye kung’ang’ania kusalia madarakani kwa kubadili katiba mara kwa mara katika Afrika baadi hawapo na baadhi wapo; Dikteta Mobutu Sese Seko (DRC),
- dikteta Siad Barre (Somalia), dikteta Jean-Bedel Bokassa (Afrika ya Kati), dikteta Yahya Jammeh (Gambia),
- dikteta Macias Nguema na dikteta Teodoro Obiang Nguema Mbasongo (Guinea ya Ikweta), dikteta Iddi Amin (Uganda), dikteta Blaise Compaore (Burkina Faso),
- Faure Gnassingbe (Togo) na Robert Mugabe (Zimbabwe), kwa kutaja wachache.
- Tumeona ni jinsi gani viongozi waliowengi wa bara la Afrika wanavyotumia madaraka yao vibaya.
- Kwa kuwa Tanzania nayo ni sehemu ya Afrika nayo haikubaki salama, kwa vipindi tofauti tofauti tumekuwa tukishuhudia ufisadi wakupindukia ambao ndio uliotufikisha hapa tulipo, tumeona ufisadi wa Tegeta Escrow Account, Mabilioni ya Uswiss, Mabilioni ya JK, Meremeta, EPA, IPTL, Radar, Ndege ya Rais, Mchuchuma na Liganga, Mikataba ya hovyo kwenye madini, wizi kwenye miradi mbalimbali ya serikali, utoroshaji wa wanyama na mengine mengi. Mambo haya ndiyo yaliyochangia umaskini uliokithiri kwa watanzania, uhaba wa madawa na vifaa tiba mahospitalini, kushamiri kwa vifo vya mama na mtoto, huduma mbovu za kijamii, wakati mwingine kuchelewa kutoka kwa mishahara kwa wakati, migomo ya wafanyakazi, hali mbaya kwa wakulima,wanalima na hawajui wakauze wapi na wamuuzie nani, urasimu katika utoaji wa pembejeo, urasimu kwenye taasisi za kifedha, ufisadi bandarini nk.
- Kuja kwa Rais Magufuli kumekuwa neema kwa wananchi waliowengi, katika utawala wa Rais Magufuli ufisadi umekuwa ni dhambi isiyo na msamaha, tumemshuhudia akipambana na kuushinda mfupa ulioligharimu taifa kwa kipindi kirefu, wapo walioondolewa kwenye nafasi zao kwa matumizi mabaya ya ofisi, wapo waliofikishwa kwenye vyombo vya haki, kaondoa watumishi hewa, mishahara analeta kwa wakati, anajenga miundombinu ya barabara, madaraja, anajenga reli ya kati kwa Standard Gauge, amelifufua shirika la ndege la taifa, wakulima wa korosho hivi sasa hata mifugo yao inajua utamu wa kinywaji soda.
- Rais Magufuli amekuwa akiokoa pesa nyingi kwa kuokoa gharama zilizowekwa kutumika kwenye sherehe mbalimbali na dhifa za kitaifa na kuelekeza pesa hizo kwenye huduma za kijamii na ujenzi wa miundombinu. Kinamama wajawazito muhimbili hivi sasa hawalali chini, ambapo kipindi cha nyuma vifaa tiba viliharibiwa kwa makusudi ili wagonjwa waende kwenye hospitali binafsi wakapigwe pesa japo nakiri kutambua mchango wa sekta binafsi katika Nyanja za afya, elimu na mambo mengine mengi, kwa kuliona hilo Rais Magufuli akatoa agizo vifaa tiba vitengenezwe mara moja, alifanya tendo la huruma na la kibinadamu hasa kwa watanzania wanyonge ingawa ni wajibu wake kufanya hivyo, anastahili pongezi za pekee. Mtu pekee ambaye hawezi kuziona juhudi za Mh. Rais ni yule tu ambaye anatizama lakini haoni.
- Pamoja na kuombwa akubali kuongezewa muda lakini amekaririwa mara kadhaa akikataa wito huo na amesema yeye anaheshimu katiba. Sheria tuliziweka wenyewe, kwa maana hiyo amekataa kuungana na ambao wameridhia kuendelea kuselelea madarakani.
- Nimeamini wanasiasa waliowengi si watu wa kuaminika, nakumbuka baadhi ya viongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini, waliwahi kukaririwa wakisema “ kwa namna nchi hii ilipofikia inahitaji Rais mwenye elementi za kidikteta”, Rais mstaafu Kikwete akasema naondoka miye mpole nawaletea mkali, leo wanatuaminisha Rais Magufuli ni dikteta, kupitia orodha yao ya watu wenye kulitia aibu taifa (lists of shame) na wakaenda mbali kuwa endapo watashika dola basi watawashughulikanao, ameingia Magufuli anawashughulikia wanatuaminisha kuwa anawaonea. Waliwahi kulalamikia uzembe kazini, uwajibikaji na watumishi hewa, Rais kaamua kushughulikanao wanatuaminisha kuwa anawaonea, waliwahi kulalamikia safari za Rais kwamba hazina tija na zinatusababishia hasara kama taifa, kaingia Magufuli kagoma kusafiri wanamlaumu eti Rais gani hatoki kukutana na wakubwa wa dunia, yaani hakuna la afadhali, kwao kila kitu ni kupinga tu.
- Niwaambie watanzania wenzangu, huko duniani hivi sasa Tanzania inapata sifa nyingi kutokana na uongozi wa Rais Magufuli, kwa wasiokubali sawa ni haki yao, siwalazimishi wala siwashawishi kukubali. Hivyo nishauri kuwa ni vizuri ikiwa tutamtia moyo Mh. Rais ili atufanyie kazi ambayo mimi na wewe tumemuajiri atufanyie, na ikiwa kuna mahala tunamuona anateleza basi tutumie njia nzuri na yakiungwana katika kumfikishia ujumbe, lakini tusimvunjie heshima kwa kumdhalilisha yeye na taasisi yake ya Urais.
- Niwashauri vyama vya siasa hususan vyama pinzani, WEKEZENI SANA KATIKA TAFITI mjue wananchi wanataka nini, lini na kwanini. Mbinu yenu ya kumpinga Rais kwa kila kitu siyo nzuri kwani badala yake inamjengea umaarufu na kumpandisha zaidi kisiasa.
- Nihitimishe kwa nukuu ya Mshairi na Mwanafalsafa wa kale Pamenidesi aliwahi kusema “hakuna kinachoweza kuwepo ispokuwa kinachoweza kufikiriwa”
TAFAKARI.
No comments:
Post a Comment