Hifadhi ya Tarangire yawapa ofa ya kutalii watu wenye Ulemavu - KABATA

This is the special room for news where you need to settle with!


Breaking

Tuesday, 22 October 2019

Hifadhi ya Tarangire yawapa ofa ya kutalii watu wenye Ulemavu


Shirikisho la watu wenye ulemavu mkoani Manyara limetoa shukrani zao kwa Uongozi wa hifadhi ya Taifa ya Tarangire baada ya kuwapa fursa ya kuitembelea hifadhi hiyo.
 wakiwa hifadhini hapo wamesema hawakudhani kama siku moja wangefika kuona wanyama na viumbe wengine wanaopatikana hapa nchini hivyo wanajivunia kuwa na urithi huo ulioachwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu  Julius Kambarage Nyerere.

Mhifadhi ujirani Mwema hifadhi ya taifa ya Tarangire, Heriel Masaki amewataka Watanzania wajijengee mazoea ya kutembela mbuga za Taifa mara kwa mara ili kujionea rasilimali zilizopo hapa nchini.

Amesema kuwa hifadhi za Taifa zilizopo ni urithi kutoka kwa Mungu na jitihada zilizofanywa na Waasisi wa Taifa hili katika kulinda na kutenga maeneo kwa ajili ya Uhifadhi,hatua ambayo imesaidia kuipa heshima nchi ya Tanzania na kuingiza fedha za kigeni zinazosaidia kwenye Miundo mbinu ya Elimu,Afya na hata Bara bara.

Katibu wa Chama cha watu wenye ulemavu mkoani Manyara Mwalimu Peter Sanka amesema walichokionyesha Tarangire ni jambo la kuigwa na wengine katika jamii.

Hifadhi ya Tarangire imewagharamikia watu wenye ulemavu wapatao 26, kuanzia Usafiri wa kwenda na kurudi Babati pamoja na Chakula.

Jina Tarangire limetokana na Mto Tara na mnyama Ngiri ambapo kabila la Wambugwe linalopatikana katika eneo hilo waliunganisha kwa majina hayo na kutengeneza jina Tarangire.

Hifadhi hiyo inayopatikana wilaya ya Babati mkoa wa Manyara ni Miongoni mwa hifadhi 23 za Taifa, ina ukubwa wa kilomita za mraba 2850,aina 550 za ndege huku ikijivunia miaka 49 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1970.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here