Kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24 Mwaka huu, Jeshi la polisi mkoani Singida limewahakikishia Usalama wananchi wa mkoa huo katika kipindi chote cha kampeni hadi siku ya Uchaguzi.
Akizungumza na wananchi wa kata ya Mitundu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Sweetbert Njeiwike amewasihi wananchi kushiriki uchaguzi huo kikamilifu, kwa amani na utulivu.
“Jeshi la Polisi limejipanga vizuri katika ulinzi kwa lengo la kuhakikisha zoezi la uchaguzi linaenda vizuri tangu kampeni zitakazoanza Novemba 17/2019 hadi siku ya uchaguzi yenyewe”alisema Kamanda Njeiwike.
Aidha Kamanda Njeiwike amesikiliza kero zinazowakabili wananchi wa Kijiji na Kata ya Mitundu Katika Halmashauri ya Itigi iliyopo Wilayani Manyoni ambapo walimweleza kuwa wana uhaba wa askari katika Kata ya Mitundu, ukosefu wa Jengo la kituo cha polisi lenye kutosheleza mahitaji pamoja na viongozi wa serikali kutokufika mara kwa mara katika Kata hiyo kuona maendeleo yao huku akiahidi kuzifanyia kazi na kuhakikisha kuwa kero hizo zinatatuliwa.
Njewike amechukua nafasi hiyo kuwashukuru wananchi hao kwa kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi vizuri jambo ambalo limesaidia kupunguza uhalifu ambapo amewasihi kuendelea kutoa ushirikiano huo ili kuimarisha zaidi usalama Katika Kata ya mitundu na Mkoa wa Singida kwa ujumla huku akimtambulisha kwao Polisi Kata ya CPL Jackson Mbusiro ambaye atashirikiana nao kwa karibu sana katika masuala ya kiusalama.
Nao wananchi wa Mitundu wamemshukuru Kamanda Njewike kwa kufika Mitundu kusikiliza kero zao.
Akiongea kwa niaba ya wananchi, Rose Madumba Diwani wa Viti Maalumu (CCM) amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kufanya kazi nzuri ambapo mpaka sasa hakuna matukio makubwa ya uhalifu.
"Hapo kipindi cha miaka ya nyuma wakati mwingine tulikuwa tunasikia milio ya risasi lakini kwa sasa ni muda mrefu hatujasikia hongereni Jeshi la Polisi , tunaomba tuongezewe askari na nyumba za makazi yao,’’ alisema Rose.
No comments:
Post a Comment