
Rais
John Magufuli leo Oktoba 18, 2017 amemtumia ujumbe Mfalme wa Oman
Mtukufu Sayyid Qaboos bin Said Al Said na wawekezaji wengine wa Oman
kuwa atafurahi kuona wanakuja kuwekeza nchini tena kwa haraka na kudai
serikali itatoa ushirikiano.
Rais ametuma ujumbe huo kwa mfalme wa Oman kupitia kwa Waziri wa Mafuta
na Gesi wa Oman Mhe. Dkt. Mohammed Hamad Al Rumhy aliyeongozana na
Waziri wa Uwekezaji wa Oman Mhe. Salem Ben Nasser Al Ismaily na Naibu
Waziri wa Utalii Mhe. Maitha Saif Majid, ambao walikua Ikulu Jijini Dar
es Salaam.
Mfalme wa Oman Mtukufu Sayyid Qaboos bin Said Al Said amemhakikishia
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
kuwa nchi hiyo ipo tayari kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya
Tano kwa kuongeza uwekezaji katika viwanda, uzalishaji wa nishati,
kuongeza thamani ya madini, kuendeleza sekta ya gesi na mafuta na
kuendeleza ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo ili kukuza uchumi kwa kasi
zaidi.
“Mhe. Dkt. Mohamed naomba ukamwambie Mfalme kuwa namshukuru kwa ujumbe
huu na namkaribisha sana Tanzania, nimefurahi kuona mpo tayari
kushirikiana nasi kujenga viwanda, kuzalisha mazao na kuendeleza ukanda
wa uwekezaji wa Bagamoyo, sisi tupo tayari hata leo, njooni tushirikiane
kwa sababu nyinyi ni ndugu zetu na tutafanya uwekezaji kwa faida yetu
sote” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametaka Oman iongeze ushirikiano na Tanzania
katika masuala ya utalii na usafiri wa anga, kuwekeza katika usindikaji
wa nyama na uvuvi na ushirikiano katika kubadilishana wataalamu wa
nyanja mbalimbali wakiwemo walimu wa lugha ya Kiswahili na Kiarabu.
Mbali na hilo Rais Magufuli amemshukuru Mfalme wa Oman kwa msaada
kujenga visima vya maji 100 hapa nchini na amemuomba kuungana na
Serikali katika safari yake ya kuhamia Dodoma kwa kujenga miundombinu
itakayoweka kumbukumbu ya ushirikiano wa kidugu na kihistoria kati ya
nchi hizi mbili.
No comments:
Post a Comment