Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Tenki la Maji la Njari.
Waziri
wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe na Mkuu wa Mkoa wa
Kilimanjaro, Mama Anna Mghwira wakifungua bomba kuashiria uzinduzi wa
Mradi wa Maji wa Mang’ana.
Waziri
wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe amkimtua ndoo kichwani
mama kutoka Kijiji cha Mang’ana, akiashiria kutimiza lengo la Serikali
‘‘kumtua mama ndoo kichwani’’ baada ya uzinduzi wa Mradi wa Mang’ana.
Msafara
wa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe ukielekea
kwenye Chanzo cha Maji cha Mang’ana katika uzinduzi wa Mradi wa
Mang’ana.
Waziri
wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe ametoa pongezi nyingi
kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Moshi (MUWSA) kwa
kufanikiwa kutoa huduma ya majisafi na salama kwa asilimia 100 kwa
Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Hayo
aliyasema alipokuwa akizindua Mradi mkubwa wa Maji wa Manga’na, uliopo
Kata ya Uru Kaskazini, utakaohudumia zaidi ya vijiji 11 katika Manispaa
ya Moshi na Wilaya ya Moshi Vijijini baada ya kupokea taarifa ya hali ya
huduma ya maji katika Mji wa Moshi.
“Nawapongeza
MUWSA kwa kazi kubwa na nzuri mliyoifanya, kwa kuwa ndio lengo la
Serikali, kuwa ifikapo mwaka 2020 maeneo ya vijijini huduma ya majisafi
na salama ifikie asilimia 85 na mijini asilimia 95. Nyinyi leo hii
mmeshavuka lengo hilo kwa Manispaa ya Moshi, kwa kweli nimefurahishwa
sana na jambo hili na mnastahili pongezi nyingi’’, alisema Mhandisi
Kamwelwe.
Waziri
Kamwelwe aliendelea kusema kuwa kwa kufanikiwa lengo hilo, mamlaka hiyo
sasa itaongezewa maeneo mengine zaidi, ili kufikisha huduma ya majisafi
na salama kwa wakazi wengine wa Moshi Vijijini ambao hawajafikiwa na
huduma ya maji, na kuahidi kama Waziri mwenye dhamana ya maji
atawatafutia fedha kwa ajili ya kufanikisha lengo hilo.
Katika
hatua nyingine Mhandisi Kamwelwe ameagiza halmashauri zote nchini, kuwa
usifanyike ujenzi wowote wa miradi kabla ya kupata chanzo cha maji cha
uhakika, ili kuondokana na matumizi mabaya ya fedha za miradi ya maji
nchini.
Waziri
Kamwelwe alisema ni ufisadi kutengeneza miundombinu ya maji, bila kuwa
na chanzo cha uhakika cha maji. Sitakubali miradi ikamilike halafu
isitoe maji, wakati umefanyika uwekezaji mkubwa wa fedha za Serikali.
Hivyo, ni marufuku mradi wowote kukamilika bila kutoa maji.
Naye
Mkurugenzi wa MUWSA, Joyce Msiru alisema katika taarifa yake kuwa mradi
huo ni moja ya miradi mikubwa iliyotekelezwa na mamlaka yake, ukiwa
umegharimu zaidi ya Sh. bilioni 2 na utahudumia zaidi ya wananchi
34,000.
Mkurugenzi Msiru alitaja baadhi ya vijiji vitakavyohudumiwa na mradi huo kuwa ni Kariwa, Longuo, Njari, Rau, Okaseni na Msuni.
No comments:
Post a Comment