Serikali
inaendelea na mchakato wa kufanikisha uwepo wa Mfumo wa soko la bidhaa
(Commodity Exchange) ambapo miongoni mwa kazi za Mfumo huo utalenga
kupunguza gharama za uendeshaji wa masoko ya mazao yote ya chakula na
biashara ili kuwawezesha wakulima kupata bei nzuri na yenye tija.
Hayo
yamesemwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Machuche
Mwanjelwa Bungeni Mjini Dodoma Wakati akijibu swali la Mbunge wa Lulindi
Mkoani Mtwara Mhe JEROME DISMAS BWANAUSI aliyetaka kufahamu ni lini
Serikali itaanzisha mfumo wa “Commodity Exchange” ili kuwasaidia
wananchi wanaolima Korosho kupata bei nzuri katika misimu husika.
Mhe Naibu
Waziri alisema kuwa Maandalizi ya Soko la Bidhaa (Commodity Exchange)
yalianza tangu mwaka 2011 kwa lengo la kufanya biashara ya mazao kuwa ya
wazi na yenye ushindani kulingana na nguvu ya soko.
Mhe
Mwanjelwa alizitaja hatua ambazo zimechukuliwa na serikali mpaka hivi
sasa kuwa ni pamoja na kupitishwa kwa Waraka wa Soko hilo, Kuundwa kwa
Bodi ya Soko, kutungwa kwa Sheria ya mwaka 2015 ya Soko la Bidhaa pamoja
na kanuni zake, Kufanya uzinduzi wa kuanzisha Soko hilo, Kutoa mafunzo
kwa Madalali watakaoendesha soko hilo na Kutoa mafunzo kwa baadhi ya
viongozi wa Serikali na Sekta Binafsi ili kujenga uelewa wa pamoja.
Alisema,
Ofisi na Jukwaa la soko hilo vimefunguliwa katika jengo la LAPF lililoko
Kijitonyama jijini Dar es Salaam ambapo kazi za uwekaji wa vifaa katika
Ofisi na Jukwaa hilo zinaendelea.
Mhe
Mwanjelwa alisema, Elimu ya Soko la Bidhaa inaendelea kutolewa kwa
baadhi ya viongozi wa ngazi za Mkoa na Wilaya na Maafisa Kilimo,
Ushirika, Biashara na Maendeleo ya Jamii katika mikoa ya Lindi, Mtwara,
Morogoro, Dodoma na Singida.
Aidha,
elimu hiyo imekwisha kutolewa kwa Viongozi wa Vyama Vikuu vya Ushirika
na Viongozi wa Vyama vya Msingi na Vyama visivyokuwa vya Kiserikali ili
kujenga uelewa wa soko hilo. Pia, elimu itaendelea kutolewa kwa wakulima
na wananchi kwa ujumla ili wadau waufahamu mfumo huo wa soko.
Kuhusu
suala la kodi kwa wakulima wa korosho Mhe Naibu Waziri alisema kuwa
Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imeondoa ushuru na tozo na
kubakiza makato ya usafirishaji korosho kulingana na umbali halisi,
mchango wa kuendeleza zao na ushirika na kuondoa shilingi 50 kwa kila
kilo zilizokuwa zinatozwa kwa ajili ya kufungashia korosho. Aidha,
Serikali imepunguza ushuru kwa Halmashauri za Wilaya kutoka asilimia 5
hadi 3.
Sambamba
na hayo pia Naibu Waziri Mhe Mwanjelwa akijibu swali la Mbunge wa Jimbo
la Busokelo Mhe Fredy Atupele Mwakibete Mkoani Mbeya kuhusu ujenzi wa
chuo cha kilimo na mifugo Kata ya Lufilyo alisema kuwa Wizara ya Kilimo
ina jukumu la kusimamia na kuviendeleza Vyuo vya Kilimo hapa nchini.
Alisema,
Kwa mujibu wa maelezo ya Afisa Kilimo wa Wilaya ya Busokelo, Chuo
kilichotajwa na Mhe. Mbunge sio Chuo cha Kilimo na Mifugo bali ni Kituo
kidogo cha kutoa mafunzo ya kilimo kwenye Skimu za Umwagiliaji (Ward
Agricultural Resource Centre). Kituo hicho kilijengwa kwa jitihada za
aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Rungwe Mashariki Mheshimiwa Profesa Mark
Mwandosya ambapo mwisho alikabidhi kituo hicho kwa Halmashauri ya Wilaya
ya Rungwe ili wakamilishe sehemu iliyobaki.
Aliongeza
kuwa Wizara inatambua uwepo wa kituo hicho na inaendelea kushirikiana
na wadau mbalimbali ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo ili kupata
fedha za kukamilisha ujenzi wa majengo hayo kwa ajili ya kutumika kama
ilivyokusudiwa.
Vyuo vya
Kilimo vinavyosimamiwa na Wizara ya Kilimo viko 14. Vyote hivyo
vimejengwa muda mrefu na hivi sasa vinakabiliwa na changamoto nyingi
ikiwa ni pamoja na uchakavu wa miundombinu ikiwemo Ofisi za Walimu,
Madarasa, Mabweni, Maabara, Nyumba za walimu, Maktaba na Karakana.
Changamoto zingine ni uhaba wa Wakufunzi na Watumishi wa kada zingine
pamoja na vifaa vya kufundishia.
Aidha,
Kutokana na changamoto hizo Wizara imeweka kipaumbele cha kuboresha Vyuo
vilivyopo badala ya kufikiria kuongeza Vyuo vingine.
Mhe
Mwanjelwa alisisitiza kuwa Vyuo hivyo vikiakarabatiwa vitaweza kuchukua
wanafunzi wengi hivyo kuwezesha Serikali kufikia lengo la kuwa na
mtaalamu mmoja wa kilimo katika kila kijiji na pia kuzalisha Maafisa
Ugani wenye uwezo wa kutoa huduma bora kwa wakulima.
Aidha,
katika mwaka huu wa fedha wa 2017/2018 Serikali imeshatenga shilingi
773,208,000/= kwa kuanzia kwa ajili ya kufanya ukarabati katika Vyuo vya
MATI.
No comments:
Post a Comment