Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani FIFA Gianni Infantino (pichani)
amemshukuru Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF) Ndugu
Wallace Karia kwa kazi nzuri ya maandalizi ya mkutano wa FIFA wa
maendeleo ya mpira (FIFA Football Executive Summit) uliofanyika Februari
22, 2018 Dar es Salaam,Tanzania.
Infantino
amesifia mapokezi na maandalizi yaliyofanywa na TFF katika mkutano huo
mkubwa uliofanyika kwa mara ya kwanza hapa nchini.
Katika barua yake aliyomuandikia Rais wa TFF Ndugu Karia ,Infantino
amesema wameondoka na kumbukumbu zisizosahaulika kuhusu Tanzania ikiwemo
urafiki uliojengeka wakati wote waliokuwepo Tanzania.
Aidha
Infantino ameshukuru kwa chakula cha usiku kilichoandaliwa kwenye
mgahawa wa Cape Town Fish Market lakini pia kwa kukutana na Waziri Mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ndugu Kassim Majaliwa.
Ameshukuru
ukarimu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wananchi kwa
ujumla huku pia akimshukuru binafsi Waziri Mkuu Ndugu Kassim Majaliwa
Amesema FIFA kwa pamoja wameridhishwa na maandalizi na shughuli zote za
mkutano huo na wamepokea mrejesho chanya kutoka kwa wajumbe wote
waliohudhuria.
Infantino
pia amepeleka salamu za shukrani kwa mjumbe wa kamati ya utendaji CAF
Ndugu Leodger Tenga,Kaimu Katibu Mkuu wa TFF Ndugu Kidao Wilfred na timu
yake kwa ukarimu waliouonesha na kujitolea kulikofanikisha mkutano
huo.
Katika
hatua nyingine Infantino ameridhishwa na utendaji kazi wa TFF tokea
Ndugu Karia ameingia madarakani pamoja na Kaimu Katibu Mkuu Ndugu Kidao
akiwataka kuendelea kusimamia mpira katika utaratibu stahiki wenye uwazi
kama wanavyofanya sasa.
Tayari msafara wa FIFA umerejea Zurich yalipo Makao Makuu ya Shirikisho
hilo.

No comments:
Post a Comment