Ifahamu historia ya mchezaji wa soko kimataifa David de Gea - KABATA

This is the special room for news where you need to settle with!

Monday, 25 November 2019

Ifahamu historia ya mchezaji wa soko kimataifa David de Gea


Novemba 7, 1990 alizaliwa mchezaji wa soka wa kimataifa wa Hispania na mlinda mlango wa timu ya taifa hilo na klabu ya Manchester United David de Gea.
Jina lake halisi ni David de Gea Quintana. Alizaliwa jijini Madrid nchini Hispania. Alianza soka lake akiwa na umri wa miaka 13 kwenye klabu ya Atletico Madrid (Rojiblancos) ambao ni mahasimu wakubwa wa Real Madrid (Los Blancos).
De Gea alikulia katika mji wa Illlescas. Wakati anajiunga na Atletico Madrid klabu ya Rayo Vallecano ya hapo hapo Madrid nayo ilikuwa ikijiandaa kudaka saini yake, kocha wa wakati huo Juan Luis Martin alilalamika kuhusu hilo lakini hatimaye De Gea alitua Rojiblancos. Kocha Diego Diaz Garrido alifanya haraka baada ya kusikia tetesi za Rayo Vallecano kuitaka saini yake na kumsajili.
Katika timu ya vijana ya klabu hiyo alizidi kukua na kuonyesha uwezo mkubwa ndipo mwaka 2008 aliposaini mkataba rasmi akiwa na umri wa miaka 17 ambao ulimbakiza hapo hadi 2011.
Baada ya kusaini mkataba wake msimu uliofuata alisalia na Atletico Madrid B iliyokuwa ikichezwa Segunda B. Majira ya joto ya mwaka 2009 De Gea alianza kufukuziwa na klabu ya Numancia ya Hispania na Queens Parks Rangers ya England ambayo ilikuwa ikimtaka kwa mkopo.
Mkurugenzi wa Michezo wa Atletico Madrid Jesús García Pitarch hakutaka De Gea aendea nje ya Hispania ndipo aliposukuma dili hilo kwa Numancia. De Gea alikataa ombi la mkurugenzi huyo wa michezo na alipewa adhabu ya kujifundisha mwenyewe.
Majuma kadhaa mbeleni kocha wa Atletico Madrid Abel Resino aligundua kuwa De Gea anafanya mazoezi peke yake ndipo alipomwalika kufanya mazoezi na timu ya wakubwa ambako alipata nafasi ya kuwa mlinda mlango wa tatu.
Msimu huo huo Atletico Madrid ilikataa ofa kutoka Wigan Athletic ya England ya kumtaka De Gea moja kwa moja. Baada ya kupambana kutafuta namba ya kuwa mlinda mlango namba moja wa Rojiblancos, alifanikiwa kuisaidia miamba hiyo katika Ligi ya Europa na UEFA Super Cup mwaka 2010.Ubora wake langoni uliwavuta klabu ya Manchester United na kufanikiwa kuidaka saini yake mnamo Juni 2011 kwa kitita cha pauni milioni 18.9 ambacho kilimfanya De Gea kuvunja rekodi ya usajili wa walinda milango katika Ligi Kuu nchini England.
Tangu amejiunga na Manchester United amecheza zaidi ya mechi 300 akishinda taji la Ligi Kuu, Kombe la FA, Kombe la Ligi, Ngao ya Jamii mara tatu na Ligi ya Europa.
Kwa misimu mitatu mfululizo 2013-14 hadi 2015-16 alichaguliwa kupokea tuzo ya klabu ya Manchester United ya Sir Matt Busby ambayo hutolewa kwa mchezaji bora wa mwaka. De Gea ndiye mchezaji wa kwanza mwenye mafanikio makubwa kunyakua tuzo hiyo.
De Gea alichukua tuzo ya Mchezaji Bora wa Kulipwa (PFA) kwa misimu mitatu kutoka 2015 hadi 2018 na pia De Gea aliingia katika kikosi bora cha mwaka cha FIFA mnamo mwaka 2018.
Katika timu ya taifa alikuwamo katika kikosi cha Hispania katika Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil. Mara kadhaa amekuwa akichukuliwa kama mlinda mlango ambaye angechukua mikoba ya Iker Casillas. Hata hivyo De Gea amekuwa akichukuliwa kuwa ni miongoni mwa walinda milango bora ulimwenguni.



No comments:

Post a Comment