SIKUKUU YA KRISMASI NA CHIMBUKO LAKE - KABATA

This is the special room for news where you need to settle with!


Breaking

Thursday, 26 December 2019

SIKUKUU YA KRISMASI NA CHIMBUKO LAKE

Kwa Nini Kanisa La Waadventista Wa Sabato Hawashriki Kusherekea Sikukuu Ya Krismas Kama Makanisa Mengine Ya Kikristo?1.     UTANGULIZI
Watu mbali mbali huuliza ili kujua sababu inayowafanya waumini wa kanisa la waadventista wa sabato kutokuungana na wenzao kuadhimisha siku kuu ya Krismas kuwa siku rasmi na takatifu ya kuzaliwa kwa Bwana wao Yesu Kristo tofauti na ilivyo kwa ndugu zao wengine wa makanisa ya kikristo.Kinyume na madhehebu mengine ya Kikristo, waadventista hawashiriki kuadhimisha siku kuu ya krismas kama sehemu ya kukiri kwa kile Yesu alichokiagiza katika Mathayo 15:13,Akajibu, akasema, Kila pando asilolipanda Baba yangu wa mbinguni litang'olewa.
Yesu Kristo mwokozi wetu  na ambaye wakristo wote wanakiri kupokea nguvu na uweza wa mamlaka; akijibu hoja za wayahudi waliokuwa wameanzisha tamaduni na desturi zao wenyewe kwa kile Mungu alichokuwa ameagiza. Yesu mwenyewe hakushikamana na mapokeo ya wanadamu yaliyokuwa yameingizwa kuwa sehemu ya kaida za kiibada, badala yake Yesu alijitahidi kadiri awezavyo kuziondoa desturi hizo zilizoingizwa na wanadamu pasipo kuakisi ukweli uliofunuliwa ndani ya Biblia. Ukweli ni kwamba njia sahihi ya kutuweka salama kuondokana na mitego ya wanadamu ni kuchunguza chanzo na asili yake. Usalama wetu ni kujua chanzo cha kila kitu ambacho tunakifanya katika ibada zetu za kila siku.2.     HISTORIA YA KRISMAS
Kwa kupitia asili ya siku kuu ya Krismas na  sikukuu zingine za kidini, waadventista waliziepuka kwa kuamini kuwa ziko kinyume na msimamo wa Yesu Kristo. Kutokana na mtazamo wao waadventista wanaamini  wazi kuwa Krismas haitokani na fundisho la Biblia bali mapokeo ya wanadamu ambayo yaliingizwa  ndani ya kanisa la KikristoFuatana name sasa kwa kina katika kuchunguza ukweli huu wa Tarehe 25 ya Desemba ndani ya UkristoLeo hii kuzaliwa kwa Yesu kunaadhimishwa tarehe 25 yamwezi wa 12 kila mwaka iliyoanzishwa na kanisa la Roman Catholiki. Lakini je ni kweli kuwa Yesu alizaliwa tarehe hiyo au siku kuu hii ina wakilisha kitu kingine?Kule Babeli, kulikuwa na mungu aitwaye Tamuzi ambaye aliabudiwa katika mfumo wa mtoto. Alizaliwa kila tarehe 25 ya Desemba, mungu huyu aliwakilisha kuzaliwa kwa jua. Kama mataifa ya kipagani walivyofanya mungu mtoto huyu aliitwa Baal-berith yaanibwana wa mti wa msonobari. Neno la kibabeli YULE humaanisha mtoto mchanga. Waingereza wa kale waliita tarehe Desemba 25 kuwa ni siku ya Yule dei. Wote wamisri na wapersia walikuwa na desturi ya kuadhimisha miungu yao tarehe 25 ya Decemba. Majina mengine yaliyotumiwa kuita mungu jua kama mtoto ni pamoja na Mithra, Horus, Deoius, Jupiter, Plutus, Ninus, Osiris, Dionysus, Bacchus, Iacchus, Adonis Attis, nk. Elimu ya visasili vinavyohusisha ibada za watoto ni uwakisiaji wa desturi za kale za babeli, (J Arrabito 1990, Laymen For Religiuos Liberty, Florida USA)Hakuna sababu ya msingi kuipatia jina Yule dei iitwayo krismas kuwa ni siku kuu ya ukumbusho wa kuzaliwa Yesu kwa wakristo. Kama hili neno linavyotumika kwa wakalidayo na wa babeli kumaanisha mtoto au mtoto mchanga wanakuwa wakimrejea Tamuzi, uhuisho wa mungu jua ambaye alikuwa akizaliwa wakati wa majira ya baridi ambapo jua huwa kaskazini kabisa (winter solstice) Tarehe 25 Desemba huwa ni siku ya kuzaliwa kwa Tammuzi yaani Mungu jua. Inaitwa Yule dei yaani Christmas day baada ya kurithishwa kutoka kwa waingereza wa kale waitwao anglo-saxons. Karne nyingi kabla ya kuzaliwa kwaYesu siku hii ya 25 Desemba iliadhimishwa kama siku ya kuzaliwa kwa mungu jua, duniani pote. Kwa wababeli aliitwa Tamuzi, Persia aliitwa Mithra, Misri aliitwa Horus, uyunani aliitwa Dionysus na Scandinavia aliitwa Balder, nk.Ibada ya kuabudu jua ilitolewa tamko rasmi katika dola ya kiroma yapat mwaka 270, na maadhimisho ya Desemba 25 ikawa siku ya kuzaliwa kwake nayo iliyosheheni michezo na sherehe kubwa sana. Wakristo wa awali hawakuitunza siku hii ya sherehe ya kipagani hadi kufikia katikati ya karne ya nne. Lakini kadili siku zilivyosonga, ilipofikia katikati ya karne ya nne ndipo kwa mara ya kwanza iliadhimishwa kama siku ya kuzaliwa Yesu huko Roma.( kama kuiga kwa ibada za miungu ya kipagani ndani ya ukristo, siku kuu hizi zilidumishwa kivitendo na kimaana, japo kwa kiasi kidogo maana yake ilibadilishwa)
3.     ASILI YA UBUNIFU WA KRISMAS
Siku kuu kubwa mbili zilikuwa muhimu sana kwa waabudu jua. Siku kuu hizo ni Summa Solstice na ile ya winta solstice, nyakati hizi za mwaka zilitegemea wakati ambao jua linakuwa mbali zaidi kutoka kwenye ikweta. Siku kuu ya midsumma ilikuwa inaadhimishwa Juni 24 ya kila mwaka, siku ambao inasadikika kuwa mchana huwa ni mrefu zaidi kuliko siku zote za mwaka. Siku hii ilitunzwa rasimi kuheshimu jua kama siku ya kukomaa kwa jua.  Katika siku hii wafu waliheshimiwa kwa kufanyiwa ibada na wakati wa majira ya jioni walitengeneza mioto mkubwa sana. Licha ya kutembea kupitia motoni juu ya makaa mekundu ya moto, kila mshindani alisamehewa dhambi zake alizozitenda dhidi ya miungu mikuu yao. Baada ya siku kuu ya midsumma, siku ziliendelea kuwa fupi na kupitia tendo hilo jua lilifikiriwa kuwa linakufa.Lakini wakati wa winta solstice hali ilibadilika; jua lilianza kurejea tena, na tarehe 25 ya Decemba ilidhaniwa kuwa siku ya kuzaliwa kwa jua, na kuwa siku ya mungu jua kuzaliwa tena. Na kuanzia siku hiyo jua lilianza kukua tena. Waabudu jua walifikiria kuwa wangelisaidia jua kupitia njia ya kuwasha mwanga na mioto ili jua lipate tena mwangaza wake. Tamaduni hii ya sanamuki hatimaye ilijipenyeza ndani ya ukristo kupitia mapokeo tuliyo nayo hadi sasa makanisani. Lakini sifa hii pambanuzi haikuwa sahihi machoni pa Mungu. Matakwa ya wanadamu na tamaduni zao haziwezi kushusha viwango vya maagizo ya Mungu au kuchukuanafasi yake. Mungu alishasema kupitia nabii Isaya,“Akawaambia, Isaya alitabiri vema juu yenu ninyi wanafiki, kama ilivyoandikwa, Watu hawa huniheshimu kwa midomo Ila mioyo yao iko mbali nami; Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu, Ninyi mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu. Akawaambia, Vema! Mwaikataa amri ya Mungu mpate kuyashika mapokeo yenu. Marko7:6-9.
Kama ilivyo kwa mungu jua yote, mungu mithra wa kipersia siku ya kuzaliwa kwake ilikuwa pia tarehe 25 ya Decemba. Tarehe hiyo hiyo pia ilikuwa siku ya kuadhimisha kuzaliwa jua katika dola ya kale ya kiroma. Kule uarabuni wasabaenerne wao waliadhimisha siku ya kuzaliwa mungu mwezi tarehe 24 ya Desemba kila mwaka. Kule Roma, Decemba 25 ilisherekewa kanisani kwa mara ya kwanza mwaka 274 BK kama Deis Natalis Solis Invicti (Unconquered sun’s birth day) yaani siku ya kuzaliwa jua isiyoshindwa. Yapata mwaka 336 kanisa la kikristo liliazimia kuithibitisha tarehe 25 Decemba kuwa siku ya kuzaliwa kwa Yesu.Akizungumzia ukweli huu wa mambo Ernest L Martin, (PhD) anasema, licha ya hayo, wapo mamilioni ya waumini wa Kikristo wanaoadhimisha siku kuu hii ya winta Solstice kuwa ndiyo siku aliyozaliwa Yesu. Inatambulika wazi kwa kila aliye na elimu kuwa tendo hilo kwa hakika ni ushikiliaji wa mafundisho ya kipagani katika familia za Kikristo au makanisani na desturi hii haina maana yoyote ile ya mafundisho ndani ya maandiko matakatifu.Sema kweli kwa sababu ya agizo  la mtume Paulo katika 1 Wakoritho 10:14 ikimbieni ibada ya sanamu na lile la mtume Yohana katika 1 Yohana 5:21 jilindeni nafsi zenu na sanamu, badhi ya mamlaka za serikali ziliwahi kupiga marufuku uazimishwaji wa Krismas kama siku ya taasisi za kipagani isiyo na kibali ndani ya maandiko. Uingereza iliwahi kutunga sheria kutoa katazo dhidi ya maadhimisho ya krismas, na mtu yeyote aliyeonekana akiiadhimisha alishitakiwa. Sheria kama hii ilikuwekwa pia katika makoloni ya Marekani. Kule Massachusetts sheria ya katazo la krismas ilipitishwa mwaka 1659  na kudumu kwa miaka 22 kabla ya kusitishwa.Historia inaonesha wazi kuwa mnamo mwaka 336 kanisa la Roman Katholiki chini ya uongozi wa dola ya kipagani ya Rumi ndiyo walioivisha Yule dei siku ya ukumbusho wa kuzaliwa kwa mungu jua kuwa siku ya krismas yaani siku ya kuzaliwa Yesu Kristo. Kumbuka ndugu msomaji kuwa badilko hilo la pili kufanywa na kanisa linakuja baada ya miaka 25 baada ya badiliko la kwanza lililofanyika mwaka 321 BK lililohusisha kubadili sabato ya Biblia kutoka Jumamosi kwenda Jumapili.
4.     ASILI YA MTI WA MKIRISMASI
Leo hii tunashuhudia wakristo wakiadhimisha siku kuu ya krismas wakiwa na mti maalum wa mikrismas. Hakuna uthibitisho wowote wa kibiblia unatoa agizo kuwataka wakristo kusherekea siku ya kuzaliwa kwa Yesu kwa miti ya mikrismasi. Lakini kwa vile sikukuu yenyewe iliingizwa kutoka kwenye desturi za kipagani, waazilishi wa awali wakatoliki walishindwa kutenganisha mapokeo hayo ya kipagani ndani ya kanisa, badala yake walilazimisha kwa kujua ama kutokujua walipoipokea siku ya decemba 25, walipokea pia kaida zingine za kiibada ikiwemo ile ya mti wa mkismas.Sognefest anadokeza kuwa, mti wa mkrismas ilikuwani desturi ya kawaida kwamataifa yote ya kipagani ukianzia Rumi ya kishenzi na Misri ya kale hata kabla ya Yesu kuzaliwa. Nchini misri walitumia mti wa  michikichi (mitende) wakati kule Rumi walitumia mti wa msonobari (mkrismas) kama ilivyooneshwa katika picha hapa chini.Iliaminika kuwa mama mzazi wa mungu jua alibadilika umbo lake kuwa mti wa msonobari wakati alipokuwa anakwenda kumzaa mtoto wake. Mungu wa waskandinavia aitwaye Odin naye alidhaniwa kuheshimiwa kwa kupewa zawadi maalum wakati wa Decemba 25 kwa kupeleka ti mtakatifu wa msonobari yaan fir tree.kutokana na ufafanuzi huu, sote tunatambua kuwa wahenga wetu walisema, Ukipenda boga penda na ua lake; ni wazi kuwa kitendo cha wakristo kuiazima Desemba 25 siku ambayo ilitengwa rasmi kwa ajili ya maadhimisho ya kuzaliwa mungu jua, kwa kuifanya takatifu au siku ya ukumbusho wa kuzaliwa kwa bwana wao Yesu Kristo, iliwalazimu pia kuzikubali kaida zao za ibada ya mungu jua ikiwemo hii ya kuadhimisha kwa kutumia mti wa msonobari, jambo ambalo halina maana yoyote ya kitheolojia au kimaandiko.
Kulingana na Dr Matin mnano mwaka 1991 anasema, kila mkisto mkomavu analijua hilo kuwa Mti wa mkrismas (msonobari) “fir tree” chanzo chake ni upagani. Mifano iliyoruhusiwa ya miti hii ukihusisha mchikichi na krismas ilikuwa inatapakaa sana kila mahali katika ulimwengu wa kipagani wa kale na ilitumika kumuenzi mungu Priapus au miungu mingine ya uzazi (ngono) . Alama na minara ya kisasa tunayoyaona katika makanisa leo hii ni mabaki ya vielelezo vya maumbo yanayohusiana na mahekalu ya kale ya kipagani na sehemu zake takatifu. Katika Yeremia 10:1-5, 8,9 nabii anaweka bayana ibada ya miti kwa wapagani ambayo waisraeli wa kale walikuwa wameanza kuiazima kutoka kwa mataifa hayo yasiyomjua Mungu wa kweli. Mtende ambao ni mti ulio wa kijani kibichi sawa na mti wa mkrismas kwa leo ulikuwa unapambwa kwa dhahabu, fedha na stika za vito vya thamani vyenye rangi mbali mbali za kuvutia. (Sawa sawa na leo jinsi zinavyopambwa kwa miali mbali mbali ya kuvututia). Miti ya aina hii iliitwa ashera na sema kweli aina karibu zote za kale zilikuwa na ibada za kuabudu miti. Muda mrefu kabla ya mataifa mengi ya ulimwengu kutupilia mbali miungu yao ya kiume na kike yenye maumbo ya watu na wanyama, inafahamika kuwa idadi kubwa ya walimwengu waliostarabika na wasio staarabika wote walikuwa na mifumo mbali mbali ya kuabudu mti; The Encyclopedia of Religion and Ethics vol 12, 448-457Katika Ukurasa wa 449 inaandika kuwa; ibada ya miti iliyo kamilika na rahisi, ilihusisha heshima yote kwa kuiadhimisha miti kama Mungu, ilishuhudiwa kwa Arabia ambapo mtende ni mti mtakatifu kule Nejran. Na ulipambwa sana kwa vitambaa vizuri vyembamba na kwa mapambo ya wanawake wakati wa sikukuu ya kila mwaka.Biblia ikielezea mfano wa ibada ya miti inamtaja mwanamke wa Yuda aliyekuwa akijihusisha na ufumaji wa nguo za mapambo maalum kwa ajili ya ibada za mti karibu na hekalu la Yerusalemu; 2 Wafalme 23:7 Akaziangusha nyumba za mahanithi, waliokuwamo nyumbani mwa Bwana, wanawake walipofuma mapazia ya Ashera.
Jambo la kushangaza ni kuwa ikiwa nabii Yeremia angelikuwa leo hai akashuhudia ibada hii ya sikukuu ya Krismas na mti wa mkrismas kuwa ukumbusho wa kuzaliwa Yesu, Je asingelitoa onyo zito zidi ya ibada hii? Au kama leo watafufuka mitume waliotuonya kujiepusha na ibaa za sanamu, je wasingelitoa katazo dhidi ya kuendeleza desturi hizi za kipagani? Lakini ajabu ni kuwa wahubiri na viongozi wa dini leo, wamefumbia macho mambo haya yote na kujifurahisha ndani ya sherehe hizi za kipagani ndani ya kanisa la Kikristo.Ebu sasa tutafakari kwa kina maana haswa ya wakristo kuingiza mti wa mkrismas ndani ya ibada yao. Kwa wapagani wao waliamini kuwa mama mzazi wa mungu jua alipomzaa, alibadilika kuwa mti. Wapagani wao wanaopouenzi mti wa msonobari au mitende ni kutoa heshima kwa mama mungu jua. Sasa ebu tujiulize wakristo wanapoadhimisha krismas kwa miti ya mkrismas wana maanisha nini cha zaidi? Bila shaka, kama tulivyokwisha pitia asili ya fundisho hili, kitendo cha kuiheshimu na kuiadhimisha siku ya Desemba 25 ndani ya ukristo siyo tu alama wakilishi ya mapokeo ya kale ya mataifa ya babeli, misri, uyunani, Persia, roma au taifa jingine lolote lisilo la kikristo, bali pia ni ishara wazi ya ibada za kipagani ndani ya ukristo. Kwa kuyajua mapokeo haya ndani ya ukristo, waadventista wa sabato walikataa maadhimisho ya Decemba 25 kuwa ni siku ya ukumbusho wa kuzaliwa kwa Yesu yaani Krismas wala hawakukubali au kutumia mti wa mkrismasi ndani ya nyumba zao au makanisani mwao kuwa ukumbusho wa Kuzaliwa kwaa Yesu kwa kuzingatia msimamo wa maandiko matakatifu.Ni heri tukiyajua maneno haya kuwa yatoka kwa Mungu; “Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa imani. Kwa maana ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni juu ya uasi wote na uovu wa wanadamu waipingao kweli kwa uovu. Kwa kuwa mambo ya Mungu yanayojulikana yamekuwa dhahiri ndani yao, kwa maana Mungu aliwadhihirishia. Kwa sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu yanaonekana, na kufahamika kwa kazi zake; yaani, uweza wake wa milele na Uungu wake; hata wasiwe na udhuru; kwa sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza. Wakijinena kuwa wenye hekima walipumbazika; wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege, na ya wanyama, na ya vitambaavyo. Kwa ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao, waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao. Kwa maana waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina, Warumi 1:17-25
5.     HITIMISHO
Kwa kuhitimisha, waadventista wanaamini kuwa, tendo la kuweka siku ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo katika siku ya kuzaliwa kwa mungu jua wa mataifa ya kale ya kipagani, tendo hilo linazo maana tano kuu ndani ya maisha ya ukristo.a.     Ni kumfanya Yesu Kristo kuwa na hadhi sawa na mungu jua, jambo ambalo ni kufuru dhidi ya Yesu Kristo. Rudia Mathayo 15
b.     Ni mwendelezo wa kutoa heshima kwa mungu jua na kwa siku yake, jambo ambalo kwa ukamilifu wake ni desturi ya kipagani ndani ya ukristo.
c.      Ni kushusha hadhi ya Yesu Kristo katika viwango vya chini sana kuliko miungu wanayojifanyia wanadamu. Hivi kweli utamuenzije Yesu Kristo aliye Bwana ndani ya siku ya kuadhimisha miungu ya makafiri, Kama hii siyo dharau dhidi ya Mungu?
d.     Ni tendo linaloenda nje kabisa ya ukweli wa Biblia na tendo linalowaambatanisha wanadamu kwenye mapokeo ya wanadamu.
e.     Kwa hivyo, waadventista wanaamini kuwa maadhimisho ya krismas yanayofanywa na wakristo leo hii hayana msingi wowote ndani ya ukristo, bali ni mapokeo ya wanadamu yaliyosimika mizizi yake katika upagani wa kale. Na ieleweke wazi ya kuwa, Desemba 25 siyo siku ya kuzaliwa Yesu Kristo kama wengi wetu tunavyoitangaza kwa watu, bali kuadhimisha siku hiyo ni kumuenzi mungu wa kipagani Tamzi (masihi wa uongo) na ndiyo maana maadhimisho hayo huambatana na mti wa msonobari (Mkrismas) yaani “fir tree” kama utambulisho wake wa kale na kale.
Ili kwa wao kujithatiti na kuonesha kiapo chao cha kweli kuyatii maandiko matakatiku likiwemo agizo la Yesu katika Mathayo 15:13 “Kanuni ya Yesu ya kung’oa mapando yote ya wanadamu”, waadventista waliyakataa mapokeo ya siku kuu za kikristo zisizoagizwa ndani ya Maandiko Matakatifu bali zimeshikamana na  kaida za dini za kale za kipagani. Kwa hakika waliazimia kushikilia mafundisho na kanuni zilizojengwa katika Kristo na ndani ya Biblia peke yake. Na huundiyo ukiri wao thabiti kwa Mungu aliye hai Muumbaji wa mbingu na nchi na vyote vilivyomo. Hii ndiyo sababu pekee na ya msingi inayojibu kwa ukamilifu wake swali la hoja, linalotaka kujua kwa nini waadventista wasabato hawashirikiani na wakristo wengine kuadhimisha siku kuu ya Krismas kama wakristo wenzao wanao abudu siku ya Jumapili.Asante sana kwa usomaji wako makini na kuambatana nami katika somo hili nyeti. Pale mwanadamu anapokubali Yesu Kristo amuongoze, Baraka za Bwana hazipungui tena maishani mwake daima. Kumbuka: UIMARA WA AKILI NI KUISHI MAISHA MATAKATIFU.Amina!!!!!!!!!!!!!!


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here