Tutashinda, atamba mkwasa - KABATA

This is the special room for news where you need to settle with!


Breaking

Wednesday, 1 January 2020

Tutashinda, atamba mkwasa



KOCHA wa Yanga, Charles Mkwasa, amesema siku zilizosalia zinatosha kuiandaa timu yake kabla ya kuikabili Simba kwenye mechi ya Ligi Kuu Jumamosi wiki hii katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Mkwasa alisema juzi kuwa, siku hizo zinatosha kuiandaa timu yake kisaikolojia na mbinu zitakazowafanya kuibuka na ushindi kwenye mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini.
Kauli hiyo ya Mkwasa imekuja baada ya kuifunga Biashara United bao 1-0 katika mechi ya ligi hiyo juzi na kushika nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na pointi 24. Alisema anachanga karata zake kupitia mbinu hizo, lengo likiwa ni kuwang’oa wapinzani wao hao kwenye usukani wa ligi na kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa.
“Siku tatu kama kocha nadhani zinatosha kuwaandaa na kuwajenga wachezaji wangu kisaikolojia, mbinu tutakazoingia nazo kwenye mechi inayokuja dhidi ya Simba, tunahitaji sana ubingwa, naamini kwa kikosi nilichonacho najua hakuna linaloshindikana tunaenda kujipanga,” alisema.
Mkwasa alisema kinachozidi kumtia nguvu kuelekea kwenye mchezo huo ni uwezo unaoneshwa na wachezaji wake kwa kupata ushindi michezo miwili mfululizo na maingizo mapya ya wachezaji waliosajiliwa kipindi hiki cha dirisha dogo lilofunguliwa Desemba 16 na likitarajiwa kufungwa Januari 15.
Mkwasa alisema pamoja na tofauti waliyo nayo dhidi ya Simba, sio kigezo cha kubariki Simba kujihakikishia kutetea ubingwa na kwamba kwenye mchezo wa soka chochote kinawezekana.
Alisema mchezo uliopita dhidi ya Biashara wachezaji wake hawakucheza kwa ubora aliotarajia kwa vile walichoka kutokana na ratiba ya mechi za ligi hiyo kuwa ngumu kwao kwani walipumzika siku moja wakitoka safari ya Nyanda za Juu Kusini kucheza michezo miwili ya ligi dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons.
Aidha, Mkwasa amempongeza mchezaji Tariq Kiakala kwa kuanza na mguu mzuri kwa kitendo cha kuifungia timu hiyo bao pekee kwenye mechi dhidi ya Biashara.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here