KARAMA NA USTAWI WA KANISA. 27.05.2021 - KABATA

This is the special room for news where you need to settle with!


Breaking

Thursday, 27 May 2021

KARAMA NA USTAWI WA KANISA. 27.05.2021

 

Na: Mchungaji Daniel Ntebi

NENO: WAEFESO 4:7-14, YOEL 2:28

KUSUDI: KUMWEZESHA KILA MKRISTO AFAHAMU KWA KIASI KUHUSU KARAMA YAKE MWENYEWE NA KUMHAMASISHA AITUMIE KWA USTAWI WA KANISA.

MAMBO YA MSINGI TUTAKAYOYATAZAMA.

·         Utangulizi.

·         Maana ya Karama.

·         Orodha ya Karama.

·         Kwanini Mungu alitoa Karama.

·         Kutambua, kukuza na kutumia Karama.

·         Karama zinazotumika isivyo Kanisani.

·         Kustawisha Karama Kanisa.

 

1.       UTANGULIZI.

Mungu amemimina Roho Mtakatifu kwa kila Mkristo. Hivyo, Mungu anatarajia kuona Karama au vipawa mbalimbali katika Kanisa. Kanisa likikosa Karama ni sawa na mtu aliye hai lakini ni mgonjwa tabani. Hii hupelekea Kanisa kuwa dhaifu sana. Karama zikitumika Kanisa ipasavyo, Kanisa litakuwa hai a lenye afya kamili.

 

2.       MAANA YA KARAMA.

-          Karama ni zawadi anayopewa Mkristo baada ya kuamini kama nyenzo ya kutumika katika kuutangaza ufalme wa Mungu.

-          Kipawa ni uwezo anaozaliwa nao mtu kumsaidia katika Maisha yake anapoishi na jamii inayomzunguka.

Kwaiyo, Karama inamilikiwa na Mkristo tu, bali Kipawa anaweza kuwa nacho mtu yeyote. Kipawa cha mtu aliyeokoka hugeuka na kuwa Karama. Wakati mwingine maneno haya mawili yanaweza kutumika kwa Mkristo kama neno moja linalofanana. Efeso 4:8 “Hivyo husema, Alipopaa juu aliteka mateka, Akawapa wanadamu vipawa”.

-          Kuna tofauti kati ya ‘Karama’ na ‘Tunda la Roho Mtakatifu’;

a.       Karama huonyesha mtu anachofanya.

-          Mfano; ni kufundishana na kuonyana n.k.

b.       Tunda La Roho Mtakatifu huonyesha jinsi mtu alivyo. Wagalatia 5:22,23 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhli, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sharia”.

-          Mfano; ni upendo, upole, uvumilivu n.k.

 

 

3.       ORODHA YA KARAMA.

- 1 Korintho 12, Warumi 12, Waefeso 4.

a.       Unabii

b.       Huduma

c.        Kufundishana

d.       Kuonyana

e.       Kukirimu

f.         Kusimamia

g.       Kurehemu

h.       Hekima

i.         Maarifa

j.         Imani

k.       Kuponya

l.         Miujiza

m.     Kupambanua Roho

n.       Aina za Lugha

o.       Tafsiri za Lugha

p.       Utawala

q.      Useja – 1 Korintho 7:7 “Ila nipendalo ni kwamba watu wote wawe kama mimi nilivyo; walakini kila mtu ana Karama yake mwenyewe itokayo kwa Mungu, huyu hivi, na huyu hivi”.

4.       KWANINI MUNGU ALITOA KARAMA?

a.       Ili Mungu atukuzwe.

1 Petro 4:10,11 “Kila mmoja kwa kadiri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana; kama mawakili wema wa neema mbalimbali za Mungu. Mtu akisema, na aseme kama mausia ya Mungu; mtu akihudumu, na ahudumu kwa nguvu anazojaliwa na Mungu; ili Mungu atukuzwe katika mambo yote kwa Yesu Kristo. Utukufu na uweza una yeye hata milele na milele. Amina.”

Ø  Karama zte zimelenga kumtukuza Mungu peke yake

b.       Ili wakristo wapate kufaidiana.

Kila mkristo anahitaji kufaidika na baraka za Mungu kwa njia ya Karama mbalimbali. Kwa mfano; uponyaji n.k. 1 Korintho 12:7 “Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.”

c.        Ili kuujenga mwili wa Kristo.

Kanisa linafananishwa na nyumba inayojengwa mpaka ikamilike au ifikie kiwango kinachotakiwa.

1 Korintho 14:26 “Basi ndugu imekuaje? Mkutanapo pamoja, kila mmoja ana zaburi, ana fundisho, ana ufunuo, ana Lugha, ana tafsiri. Mambo yote na yatendeke kw kusudi la kujenga.”

Waefeso 4:12 “Kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya Huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe.”

 

5.       I. KUTAMBUA KARAMA YAKO

Wakristo wengi hawafahamu karama zao. Zifuatazo ni njia zitakazomsaidia mkristo kutambua Karama yake:-

a.       Tafakari moyo wako unakusukuma kufanya nini kaanisani? Msukumo huu huwa hautulii.

Yeremia 20:9 “Nami nikisema, sitamtaja, wala sitasema tena kwa jina lake; basi, ndipo moyoni mwangu kumekuwamo kama moto uwakao, uliofungwa ndani ya mifupa yangu, nami nimechoka kustahimili, wala siwezi kujizuia.”

b.       Ukifanya hilo jambo unajisikiaje au usipolifanya unajisikiaje?

Ukiifanya Karama yako lazima ujisikie vizuri na usipoifanya utajisikia vibaya. 1 Korintho 9:16 Maana, japo kuwa naihubiri injili, sina la kujisifia; maana nimeweka sharti; tena ole wangu nisipoihubiri injili.”

c.        Je, watu wanamwitikio gani kwa Huduma yako?

Ø  Wanaweza kufurahi. Matendo 21:17 “Tulipofika Yerusalemu ndugu wakatukaribisha kwa furaha.”

Ø  Hata hivyo, kumbuka shetani yumo kazini anaweza kukukatisha tamaa. Matendo 16:16 “Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua.”

II. KUKUZA KARAMA YAKO.

    Karama hukua kwa kila mkristo. Yapo mambo ya kuzingatia ili kukuza Karama yako.

a.       Omba Mungu aikuze Karama yako. Waefeso 9:19 “Pia, na kwa ajili yangu mimi, nipewe usemi kwa kufumbua kinywa changu, ili niihubiri kwa ujasiri ile siri ya injili.”

b.       Soma Neno la Mungu litaikuza Karama yako.

2 Timotheo 4:13 “Lile joho nililoliacha kwa Karpo huko Troa, ujapo ulilete, na vile vitabu, hasa vile vya Ngozi.”

c.        Kaa karibu na kiongozi wako, atakuelekeza ili ukue. Yesu naye alikaa na mitume.

Matendo 15:39 “Basi palitoke mashindano baina yao hata wakatengana. Barnaba akamchukua marko akatweka kwenda Kipro. Linganisha na 2 Timotheo 4:11 “Luka peke yake yupo hapa pamoja nami. Umtwae Marko, umlete pamoja nawe, maana ananifaa kwa utumishi.

d.      Jifunze Neno la Mungu kutoka vyanzo sahihi. Mfano kuhudhuria semina, makongamano, ibadani n.k. Waefeso 4:11-12 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na walimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya Huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe.”

III. KUTUMIA KARAMA YAKO.

a.       Tumia Karama yako kwa ustawi wa Kanisa. 1 Wakorintho 12:7 “Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana”. Kila Mkristo amapewa Karama hiyo kwa ustawi wa Kanisa. Mkristo anaelalia Karama yake ana lengo la kudhoofisha Kanisa.

b.      Mkristo anayetumia Karama yake atapata thawabu siku ya mwisho. Daniel 12:3 “Na walio na Hekima watang’aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang’aa kama nyota milele na milele”.

c.       Mkristo aliyekalia Karama yake ataadhibiwa siku ya mwisho. Luka 12:47 “Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana”.

6.       KARAMA ZINAZOTUMIKA ISIVYO KANISANI.

Kuna Karama chache ambazo Kanisa la leo halizitumii ipasavyo:-

A.       Kunena kwa Lugha. 1 Wakorintho 14: 1-2 “Ufuateni upendo, na kutaka sana Karama za rohoni, lakini zaidi kwamba mpate kuhutubu. Maana yeye anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna asikiaye; lakini anena mambo ya siri katika roho yake”. Makanisa ya kipentekoste yameitazama Karama hii kuwa ni tofauti kabisa.

i.                    Hulazimisha kila mtu anene kwa lugha. Marko 16:17,18 “Na ishara hizi zitafuatana nao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya”. Paulo analiweka sawa hili kuwa wote hawawezi kuwa na Karama moja tu Kanisa; 1 Wakorintho 12: 8,9,30 “Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la Hekima; na mwingine neno ka maarifa, apendavyo Roho yeye yule; mwingine Imani katika Roho yeye yule; na mwingine Karama za kuponya katika Roho yule mmoja; wote wanakarama za kuponya wagonjwa? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri?”.

ii.                  Wapentekoste hulazimisha kunena wakati wowote tu hata anahubiri au kuomba. Paulo anatoa utaratibu wanene wawili au watatu, tena zamu kwa zamu ikiwa yupo wa kufasiri.         1 Wakorintho 14:27 “Kama mtu akinena kwa lugha, wanene wawili, au watatu, na wengine wapambanue”. Kama hayuko wa kufasiri Kanisani asitokee wa kunena kwa lugha.  1 Wakorintho 14:28 “Lakini asipokuwapo mwenye kufasiri na anyamaze katika Kanisa; aseme na nafsi yake tena na Mungu”.

B.       Kutoa Unabii. Unabii ni maneno yote ya Mungu aliyotuletea Mungu yaani maneno yote yaliyomo katika Biblia. Nabii ni mtu yeyote aliyejaa Roho Mtakatifu anayepokea neno la Mungu kulipeleka kwa watu. Agano la Kale Mungu alizungumza nasi kupitia manabii. Lakini siku hizi Mungu amesema nasi kupitia mwanaye.

-          Robo tatu ya unabii wa Biblia unaonya au unawahamasisha watu kuishi Maisha ya Mbinguni (forthtell) na Robo inayobakia inazungumzia siku zijazo (foretell).

-          Kwa kuwa sasa Mungu amesema kupitia mwana wake (Agano jipya), hakuna unabii mpya tunaweza kupata.

-          Kila mtu atayenena maneno ya unabii (Biblia) lazima tumpime kama anasema sawa kama Waberoya walivyowapima wahubiri. Yohana anasema tuzijaribu kila roho, maana wapo manabii wa uongo wadanganyao watu. 1 Yohana 4:1-4 “Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetoka na Mungu; kwa sababu manabiiwa uongo wengi wametokea duniani. Katika hili mwamjua Roho wa Mungu; kila roho ikiriyo kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatokana na Mungu. Kila roho isiyomkiri Yesu haitokani na Mungu. Na hii ndio roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani. Ninyi, Watoto wadogo, mwatokana na Mungu nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia”.

 

C.      Uponyaji. Karama hii imechezewa sana, kwani hata ushirikina umeingia ndani. Mfano; Ni vyema kuwa makini na mtu aliyebeba Karama hii. Hata wengine wametoza watu fedha nyingi kwa shida zo, jambo ambalo si sawa. Mathayo 10:8 “Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure”.

 

7.       KUSTAWISHA KARAMA KANISANI.

Ili Kanisa listawi kabisa, yafuatayo yazingatiwe:-

a.       Viungo vyote vya mwili vifanye kazi kwa ushirikiano. 1 Wakorintho 12:12-15 “Maana kama vile mwili mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu wahayahudi au kwamba tu wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja. Kwa maana mwili si kiungo kimoja, bali ni vingi. Mguu ukisema, kwa kuwa mimi si mkono, mimi si wa mwili; je! Si wa mwili kwa sababu hiyo?”. Kwahiyo, kila mtu Kanisani anatakiwa awajibike na Karama yake mfano, Mwalimu, Mwanasheria, Afisa rasilimali watu, Fedha, Takwimu, IT, Mfanyabiashara, mwimbaji, Mshauri, Mwanatheorogia n.k, kila kiungo/Karama lazima kiheshimiwe. Zaburi 133:1-3 “Tazama, jinsi ilivyo vyema, na kupendeza, ndugu wakae pamoja, kwa umoja. Ni kama Mafuta mazuri kichwani, yashukayo ndevuni, ndevu za Haruni, yashukayo mpaka upindo wa mavazi yake. Kama umande wa Hermoni ushukao milimani pa Sayuni. Maana ndiko BWANA alikoamuru baraka, Naam, uzima hata milele.

b.       Kuwatii na kuwanyenyekea wenye kuwaongoza. Hakuna mwanafunzi anayefaulu darasani kama siyo mtiifu na mnyenyekevu. Mambo haya mawili hufungua mlango wa mafanikio kwa Kanisa.

Waebrania 13:17

Watiini wenye kuwaongoza, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana isingewafaa ninyi.

c.        Kanisa litie juhudi sana katika Maombi. 1 Wathethalonike 5:17 “Ombeni bila kukoma”. Palipo na maombi panamafanikio makubwa.

 

MWISHO.

Baada yakujifunza somo hili, naamini kila mtu atawajibika katika kutumia Karama yake. Wale ambao hawakujua Karama sasa wanaweza kuzitambua na kuanza kutumika Kanisa.

Bwana alistawishe Kanisa Lake.

Endapo una mwaswali au ushauri, tuma kwa Rev. Daniel Ntebi rntebi@yahoo.com au kwa kutumia namba ya simu +255 786 533 028.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here