Askofu Shoo: Tuwaonee huruma wanaoteseka - KABATA

This is the special room for news where you need to settle with!


Breaking

Saturday, 25 December 2021

Askofu Shoo: Tuwaonee huruma wanaoteseka


Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo amemuomba Mungu awape Watanzania macho ya kuwaona na mioyo ya huruma, wote wanaoteseka na kulia kipindi hiki cha sikukuu.


kuwaonea huruma wote wanaoteseka na kulia kipindi hiki cha sikukuu.


Amesema katika kundi la wanaolia, wapo walioondokewa na ndugu kutokana na ugonjwa wa Uviko-19 na walio magerezani waliotengwa na jamaa zao pengine hata bila kutenda kosa.


Hata hivyo, Askofu Shoo alisema licha ya kirusi cha Omicron, wakristo na Watanzania wanapaswa kujua Mungu yupo, atawalinda na mabaya yote, lakini wasimjaribu kwa kuishi na kutenda kizembe kwa kutochukua tahadhari za kujikinga.


Askofu Shoo alitoa kauli hiyo katika salamu zake za Noeli na mwaka mpya wa 2022 kwa waumini wa kanisa hilo lenye Dayosisi 26 na kutaka Watanzania wasifurahi peke yao, bali wawakumbuke walio na huzuni na majonzi kwa sababu mbalimbali.


Hata hivyo, katika salamu hizo Askofu Shoo ambaye pia ni mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini, hakugusia lolote kuhusiana na migogoro inayoendelea kulitikisa kanisa hilo katika Dayosisi ya Konde mkoani Mbeya na Kaskazini Mashariki iliyopo mkoani Tanga.


Migogoro hiyo imeenda mbali na kusababisha baadhi ya wachungaji kusimamishwa au kuvuliwa uchungaji huku katika Dayosisi ya Konde maaskofu sita akiwamo Askofu Shoo kufunguliwa kesi ya madai Mahakama Kuu Mbeya.


Wadaiwa wengine ni maaskofu Alex Malasusa wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Amos Kinyunyu wa Dayosisi ya Dodoma, Wilson Sanga wa Dayosisi ya Kusini Kati, Blaston Gavile Dayosisi ya Iringa, Renard Mtenji ya Ulanga.


Alichokisema Askofu Shoo

Katika salamu za sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya, Askofu Shoo ameeleza makundi yanayosherehekea sikukuu hizo yakiwa katika mateso na kilio likiwemo waliopo magerezani pengine bila ya kutenda makosa.


“Wapo wasio na chakula, wagonjwa na wanaouguliwa, walioondokewa na wapendwa wao kwa Uviko-19 na madhara mengine, wasio na ajira, walio magerezani na kutengwa na jamaa zao pengine hata bila kutenda kosa.


“Tunapoadhimisha sikukuu ya mwaka huu tunapaswa kufurahi na kumshukuru Mungu kwa upendo wake mkuu kwetu sisi wanadamu. Tusifurahi peke yetu, bali tuwakumbuke wenzetu walio na huzuni na majonzi kwa sababu mbalimbali,” alisema na kuongeza:


“Tusijifariji na kujidanganya kuwa hatuwaoni, hatuwajui wanaolia wakati sisi tunasherehekea. Mungu atupe macho ya kuwaona na mioyo ya huruma kwa wote wanaoteseka na kulia kipindi hiki cha sikukuu,”alisisitiza Askofu Shoo.


“Furaha ya Krismasi inakuwa haijakamilika kwangu wakati jirani yangu au familia yake inahuzunika na kulia, wakati mimi nina uwezo wa kuwasaidia angalau na wao wafurahi,”alisema Askofu Shoo.


“Mungu anataka furaha hii kuu iwe kwa watu wote. Mimi na wewe tuliojaliwa kufurahi na familia zetu tuone sababu ya kufanya tendo lolote litakalompa furaha jirani mwenye huzuni,” alisema Shoo katika salamu hizo na kuongeza;-


“Licha ya kirusi Omicron tujue Mungu yupo na anatuambia msiogope. Tukimtumaini Mungu kwa dhati, atatulinda na kutukinga na mabaya yote, lakini tusimjaribu kwa kuishi na kutenda kizembe, hata kujisababishia madhara.”


Askofu Shoo alisisitiza kuwa kutochukua tahadhari ya kujikinga na maambukizi ya Uviko 19 na kujiletea madhara wao na wengine na kueleza pamoja na kumtegemea Mungu wana wajibu wa kuwasikiliza wataalamu wa afya.


Kauli ya Askofu Shoo imekuja siku chache baada ya Katibu mkuu Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi kuzitahadharisha familia zinazosafiri kwa ajili ya sikukuu za mwisho wa mwaka kuchukua tahadhari kwani visa vya Uviko-19 vinaongezeka kwa kasi.


“Familia zinazosafiri kwa ajili ya sikukuu za mwisho wa mwaka hakikisheni mnawalinda wazee huko vijijini kwa kuchukua tahadhari zote pamoja na kuvaa barakoa na kuchanga“Pamoja na kuongezeka kwa mafua ya kawaida (seasonal influenza), bado tuna maambukizi ya Uviko-19 na yanaongezeka kwa kasi. Nawaomba wananchi waendelee kuchukua tahadhari zote za kinga zikiwamo kuvaa barako na kuchanja,” alisema Profesa Makubi Desemba 19, 2021 Jijini Dodoma.


Hata hivyo, Shirika la Afya Duniani (WHO), limetoa wito kwa watu kuahirisha kusafiri kwenda kwa ajili ya sikukuu za mwisho wa mwaka, ili kukabiliana na kirusi cha Omicron ingawa kwa Tanzania, mamlaka hazijathibitisha kuingia kwake.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here