Necta yatoa utaratibu usajili waliopata mimba kurudi shule - KABATA

This is the special room for news where you need to settle with!


Breaking

Thursday, 2 December 2021

Necta yatoa utaratibu usajili waliopata mimba kurudi shule

 


Siku chache baada Serikali kuruhusu kurejea kwenye mfumo rasmi wa elimu wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali, ikiwamo ujauzito, Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limetoa utaratibu wa kuwasajili wanafunzi hao kwa ajili ya kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi.


Utaratibu huo uliotolewa na Necta kupitia barua maalumu iliyoelekezwa kwa makatibu tawala umeeleza kuwa Serikali imetoa ruhusa ya kurudia mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kwa watahiniwa waliofeli, walioshindwa kufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ujauzito.


Ruhusa hiyo imewanufaisha pia wanafunzi waliofutiwa matokeo kwa sababu ya udanganyifu ambapo kwa mwaka huu, jumla ya watahiniwa 393 walifutiwa matokeo, wakati mwaka jana rungu hilo liliwakumba watahiniwa 1,059.


Hatua hiyo ya kufutiwa matokeo ilikwenda sambamba na adhabu ya kupoteza sifa ya kufanya mtihani wa Taifa wa darasa la saba katika maisha yao yote, jambo ambalo lililalamikiwa na wadau na watetezi wa haki za elimu kwa watoto wakiitaka Serikali kufanyia mapitio ya adhabu hiyo.


Barua hiyo iliyosainiwa kwa niaba ya Katibu Mtendaji, Dk Charles Msonde ilitoa maelekezo ya kuzingatiwa katika kuwasajili watahiniwa wanaorudia mtihani wa kumaliza elimu ya msingi wakielekezwa kuanza masomo Januari mwakani.


Utaratibu huo unahusisha sifa za mwanafunzi ambaye alifanya na kufaulu mtihani wa upimaji wa darasa la nne na awe amehudhuria elimu ya msingi kwa miaka saba.


Sifa nyingine awe alisajiliwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi na kufeli, kufutiwa matokeo au kushindwa kufanya mtihani kwa sababu mbalimbali.


Kulingana na barua hiyo, mwanafunzi ataruhusiwa kurudia mtihani mara moja katika mwaka unaofuatia baada ya kushindwa kufanya mtihani wa awali kutokana na changamoto zilizompata.


Pia mtahiniwa asajiliwe katika shule ya msingi aliyosoma au nyingine atakayoona inafaa, huku walimu wakuu wakipewa maelekezo ya kusajili watahiniwa kwenye mfumo wa usajili wa wanafunzi wa shule ya msingi unaofahamika kama (PRem) ambao una sehemu maalumu ya watahiniwa wanaorudia mtihani.


Necta katika barua hiyo ilisisitiza kuwa taratibu zote za usajili zikamilike kwa kuzingatia kalenda ya usajili wa watahiniwa wa mwaka husika wa mtihani.


Maoni ya wadau

Akizungumza na Mwananchi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Faraja Kristomus alisema uamuzi wa kuwarudisha shuleni watoto hao ni ushindi mkubwa kwa wadau wa elimu ambao wamekuwa wakipigania haki ya elimu kwa watoto.


Alisema tayari Serikali imeonyesha kuelewa umuhimu wa elimu kwa watoto, hivyo ni vema hatua zote hizo zikawekwa kisheria ili kusiwe na mabadiliko kulingana na kiongozi atakayekaa madarakani.


“Ni wakati wa Serikali sasa kuangalia na kutathmini mifumo ya adhabu, hasa zinazohusu watoto na kugusa suala zima la elimu. Hatua nzuri zimechukuliwa, ni vema zikatungwa sheria na miongozo kusimamia utekelezaji wake.


“Kilichotokea sasa ni kwa sababu ya uongozi uliopo madarakani, sasa tusiishi kwa kusubiri huruma ya kiongozi, lazima tuwe na sheria na miongozo itakayowaongoza watendaji wetu,” alisema.


Kuhusu kupewa nafasi nyingine watoto waliobainika kufanya udanganyifu, Dk Kristomus alisema Serikali imefanya busara ya hali ya juu kwa kuwa adhabu waliyopewa watoto hao ilikuwa kubwa ambayo ingewafanya wengi wao kukosa fursa ya kupata elimu na kuishia kwenye umaskini. Kwa upande wake, Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (Tenmet) Ochola Wayoga alisema: “Kuhusu watoto waliokuwa wanafutiwa matokeo na kuzuiwa wasifanye mtihani tena ilikuwa adhabu kali ambazo kimsingi zingefifisha maisha yao, tunaipongeza Serikali kwa uamuzi huu, kazi kubwa ifanyike sasa katika kuwahamasisha watoto hawa kurejea shule na kuendelea na masomo,” alisema.


Naye mdau wa elimu, Cathleen Sekwao alipongeza hatua hiyo ya Serikali na kuomba hatua stahiki kuchukuliwa kuhakikisha wanafunzi hao wanaorudia shule wanapata mazingira mazuri ya kusoma.


“Jitihada za kujenga vyumba vya madarasa ziongezeke, maana kwa hatua hii wanafunzi watakuwa wengi, waongezwe pia na walimu kuhakikisha wanafunzi wote wanapata haki sawa ya kupata elimu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here