Makamu wa Rais, Dkt Phillip Mpango

CHANZO CHA PICHA,OFISI

Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt Philip Mpango ameelezea kusikitishwa kwake na vitendo vya mauaji vilivyotokea nchini Tanzania.

Kutokana na hali hiyo, amemuagiza Inspekta Jenerali wa Polisi-IGP wa nchi hiyo kuingilia kati haraka na kukomesha mauaji ambayo yamekuwa yakishuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Akiwa katika kijiji ambacho hadi sasa kinaomboleza mauaji ya kikatili ya watu watano wa familia moja, Makamu wa Rais ametoa siku saba kwa IGP kuwakamata wote waliohusika na mauaji hayo.

''Pamoja na kazi iliyofanywa na hatua ambayo Mkuu wa Mkoa amechukua Serikali inatoa agizo kwa vyombo vyote , mauaji haya yafanyiwe kazi mara moja, na taarifa ndani ya siku saba kuanzia leo, taarifa rasmi iwasilishwe kwa ofisini kwa Mheshimiwa Rais''.

''Haikubaliki hata kidogo kwa sababu inashangaza yaani ukifika hapa sielewi, kama nyumba yenyewe ni hiyo , zizi liko hapa na hata nyumba nyingine ziko karibu kabisa, inawezekanaje, iliwezekanaje watu wakauliwa huku ndani, hata jirani kujua kwamba... jirani huyo hajatoka kweli?

Hapana, kwa hiyo vyombo mfanye kazi yenu barabara asibaki hata mtu mmoja, asakwe, wasakwe popote walipo, wachukuliwe hatua mara moja. Hatuwezi kwenda namna hii, niseme mapema, idara yetu ya upelelezi ihakikishe kwamba hapa saa 24 mpaka wabainike na vyombo vingine vyote tusaidiane kuhakikisha kuwa watu wanapatikana.

Tangu mauaji ya kutisha yaliyotokea mwishoni mwa juma, hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa ngazi ya juu kufika katika kijiji hicho ambacho kimegubikwa na hofu kuu.

Hivi karibuni Tanzania imerekodi idadi ya mauaji katika mikoa kadhaa yakiwemo Mtwara, Mbeya na Moshi.

Matukio ya mauaji yalivyotokea maeneo kadhaa nchini Tanzania

Dodoma

Watu watano wa familia moja waliuawa katika viunga vya mji wa Dodoma,

Watu watano wa familia moja wakazi wa kijiji cha Zanka wilayani Bahi Mkoa wa Dodoma katikati mwa Tanzania waliuawa na watu wasiojulikana.

Waliouawa ni mume, mke, watoto wawili na mjukuu mmoja wote wa familia moja.

Mdogo wa baba wa familia hiyo, Noah Kapande amesema aliambia gazeti la Mwananchi kuwa miili hiyo iligunduliwa na watoto waliokwenda kufungua ng'ombe jirani na nyumba hiyo siku ya Jumamosi saa 10 jioni baada ya kuhisi harufu.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka akiongozana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo amewataka wakazi wa kijiji hicho na ndugu kutoa ushirikiano ili waliofanya kitendo hicho wajulikane.

"Hili jambo litakuwa limefanywa kwa ushirikiano na watu wa hapa hawezi kuja mtu kutoka huko kwenye nyumba ya mtu akaua watu watano asiwe na mwenyeji hapa,"amesema.

Ameagiza vyombo vyote vya ulinzi na usalama na uchunguzi vya mkoa kuhamia katika kijiji hicho kufanya uchunguzi wa tukio hilo na waone namna ya kushirikiana na wenzao kama italazimika kufanya hivyo.

Mwanza

Wanawake watatu wanaokadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 18 hadi 30 walikutwa wameuawa na watu wasiojulikana na miili yao kukutwa pembezoni mwa mto eneo la Nyakato jijini Mwanza Kaskazini Magharibi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Gidion Msuya ameliambia Mwananchi kwa simu leo Jumatano Januari 19, 2022 kuwa uchunguzi unaendelea kuhusu tukio hilo ikiwamo kuwatambua marehemu na kuwasaka waliohusika na mauaji hayo.

"Miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya kanda Bugando kwa ajili ya utambuzi na uchunguzi zaidi," alisema Kaimu kamanda Msuya.

Miili ya wanawake hao ilionesha kuwa walikatwa na kitu chenye ncha kali kutokana na majeraha yaliyoonekana maeneo ya shingoni.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa mtaa wa Mecco eneo la Nyakato zilikookotwa maiti hizo, Scolastica Barnabas amesema pamoja na kukutwa na majeraha shingoni, miili yao ilikuwa tupu haijavikwa nguo.

Dar es Salaam

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam limethibitisha kuwakamata watu wawili wanaodaiwa kula njama ya kumuua mwanamke mmoja katika nyumba ya kulala wageni eneo la Tabata Segerea jijini Dar es Salaam.

Mwanamke huyo aliyejulikana kwa jina la Barke Rashid (30) aliuawa tarehe moja mwezi Januari, 2022 baada ya anayedaiwa kuwa mpenzi wake kutoa malipo ya Shilingi za kutanzania milioni 1.7 kwa mtu mmoja ili atekeleze mauaji hayo

Taarifa iliyotolewa na Jeshi hilo leo Jumanne Januari 25, 2022 imeeleza kuwa chanzo cha mauaji hayo ni mwanamke huyo kukabwa shingo mpaka kupoteza maisha akiwa katika nyumba hiyo ya wageni.

Inadaiwa mtuhumiwa wa kwanza alikodiwa na mtuhumiwa wa pili kwa malipo ya Sh1.7 milioni ili amshawishi kimapenzi na baadae aende kumuua mwanamke huyo kwa madai kuwa mtuhumiwa wa pili alimgharamia sana na kumpangishia nyumba lakini ilidaiwa na mtuhumiwa wa pili kuwa mwanamke huyo ana wanaume wengine.

"Mtuhumiwa wa kwanza amekiri kupewa Sh1.2 kwa nyakati tofauti kabla na baada ya kutekeleza mauaji hayo na kwamba alikuwa bado anadai Sh500,000 kwa mtuhumiwa wa pili kwa mauaji ya mwanamke huyo, uchunguzi wa tukio hilo unakamilishwa na watafikishwa Mahakamani haraka iwezekanavyo" ilieleza taarifa hiyo.

Mtwara

Polisi Mkoani Mtwara wamethibitisha kuwakamata na kuwafikisha mahakamani Maafisa wa Polisi saba kwa tuhuma za mauaji ya mfanyabiashara Mkoani Lindi, kusini mwa Tanzania.

Taarifa hiyo imetolewa na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara, ACP Marck Njera imesema mauaji hayo yalifanyika Januari 5, 2022 na mwili wa marehemu ulitupwa kitongoji cha Majengo kijiji cha Hiari Wilayani Mtwara.

Mfanyabiashara huyo ni Mussa Hamisi mkazi wa Kijiji cha Ruponda wilayani Nachingwea Mkoani Lindi.

Maafisa wanaoshikiliwa ni Mrakibu wa Polisi ,Mkuu wa Upelelezi wa wilaya ya Mtwara,Mkuu wa Kikosi cha Intelejensia ya Jinai mkoa wa Mtwara, Mkaguzi wa Polisi na Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara,

Matukio hayo ya mauji yameacha maswali mengi kwa baadhi ya watu huku wakisubiri hatua mbalimbali zichukuliwe na Serikali na kwamba hatua hizo huenda zikasaidia katika kupunguza matukio mbalimbali ambayo yamekuwa yakileta doa kwenye jamii na kwenye Jeshi la Polisi lenye jukumu la kuwalinda wananchi.