Mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yana maana gani kwa uongozi wa Rais Samia? - KABATA

This is the special room for news where you need to settle with!


Breaking

Tuesday, 11 January 2022

Mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yana maana gani kwa uongozi wa Rais Samia?

TH

CHANZO CHA PICHA,HABARI MAELEZO

Jumanne, Januari 4, 2022, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akipokea taarifa ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano ya Uviko-19 alieleza mpango wake wa kulifanyia mabadiliko baraza la mawaziri.

Jumamosi, Januari 8, 2022 Ikulu jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga aliweka wazi kwa umma mabadiliko hayo, ambayo ni ya tatu tangu Rais huyo kuingia madarakani, Machi 2021.

Mabadiliko ya kwanza ya Baraza la Mwaziri yalifanyika Machi 2021, Ikulu Chamwino, Dodoma wakati wa hafla ya kumuapisha Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango. Mabadiliko ya pili yalifanyika mwezi Septemba 2021.

Mabadiliko sasa yamekuja na makundi manne; wale waliobaki katika nafasi zao, waliobadilishwa Wizara, waliondolewa katika Baraza moja kwa moja na kundi la walioingizwa katika Baraza hilo.

Nafasi za wanawake

Septemba 15, 2021 akihutubia katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Demokrasia, ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, Rais Samia alieleza mkakati wake wa kuendelea kuwateua wanawake katika nafasi mbali mbali za uongozi na kushughulikia haki za wanawake na usawa wa kijinsia.

TH

CHANZO CHA PICHA,WIZARA YA AFYA

Rais huyo amefanya mabadiliko ya wizara na kuunda Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu. Wizara hii inaakisi juhudi zake za kuhakikisha wanawake hawaachwi nyuma katika shughuli za maendeleo.

Septemba 2021, alipofanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri, alifanya uteuzi wa Mawaziri wanne, wawili wakiwa wanawake na wawili wanaume. Safari hii wanawake walikuwemo pia katika uteuzi.

Mabadiliko ya sasa yameongeza idadi ya Mawaziri wanawake kutoka saba na kufikia tisa. Mawaziri wawili waliofikisha idadi hiyo ni Dkt. Pindi Chana, Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu atakae shughulika na Sera, Bunge na Uratibu.

Mwingine ni Dkt. Angelina Mabula, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Idadi ya mawaziri tisa imelifanya kuwa moja ya Baraza lenye idadi kubwa ya wanawake ukilinganisha na Mabaraza ya huko nyuma.

Wawili kati ya hao tisa wameshika Wizara nyeti, ambao ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stergomena Tax.

Vigogo walioshushwa na waliopandishwa

Mawaziri wanne wameodoshwa katika nafasi zao. Kati ya hao wapo vigogo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), na wakongwe katika siasa za Tanzania. William Lukuvi, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makaazi na aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi.

Jumatatu, Januari 10, 2022, wakati wa kuapishwa viongozi mbali mbali walioteuliwa hivi karibuni wakiwemo mawaziri, Ikulu Chamwino, Rais Samia alieleza kuwa wanasiasa hao wawili amewapangia kazi nyingine za kufanya.

"Kaka yangu Lukuvi yeye ana kazi na mimi na mtaisikia baadae. Kaka yangu Kabudi amefanya kazi nzuri sana kusimamia mazungumzo ya Serikali na mashirika na ndio kazi ninayomkabidhi sasa kindakindaki aendelee nayo."

Mawaziri wapya watano wameteuliwa, yupo Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Wakati wa hayati John Pombe Magufuli alifutwa kazi akiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Hamadi Masauni, ameteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. Uteuzi huu umeifanya idadi ya Mawaziri kutokea upande mwingine wa Muungano, Zanzibar kuongezeka.

Awali alikuwepo Waziri mmoja tu kutokea Zanzibar, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, akiongoza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Mbarawa aliteuliwa na Rais Samia, katika mabadiliko ya pili ya bara hilo, na kabla ya hapo hakukuwa na Waziri kamili kutokea Zanzibar.

Uteuzi wa Masauni umeongeza nguvu kulifanya Baraza kuwa lenye sura ya muungano. Wakati wa utawala uliopita mawaziri kamili kutokea upande wa Zanzibar walikosekana, hatua iliyokosolewa pakubwa na wanaharakati wa kisiasa.

Kwanini mabadiliko yamekuja sasa?

Mwezi Julai na mwanzoni mwa Agosti 2021, vyombo vya usalama nchini Tanzania viliendesha operesheni kadhaa za kuwakamata wafuasi na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Wapo waliokamatwa Mwanza wakiwa na Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe, wengine walikamatwa Dar es Salaam. Kamata kamata hii ilihusisha wale waliotaka kufanya maandamano na mikutano ya kisiasa.

Kufuatia matukio hayo; swali kuu lililozuka ni ikiwa Rais Samia ameamua kuendeleza harakati ambazo upinzani ilidai ni za kuuandama au ameshindwa kudhibiti watendaji wake ambao wengi ni wale waliotokea utawala wa hapo mbeleni .

Je, panga-pangua hii ina uhusiano wowote na Rais Samia kutaka kudhibiti hali ya mambo katika utawala wake? Swali hilo amelijibu mchambuzi wa siasa za Tanzania, Dkt. Nicodemus Minde.

"Mabadiliko haya ni Rais Samia kutaka kuimarisha utawala wake, na kusimamia misingi yake mwenyewe katika serikali na chama, ikizingatiwa kuwa yeye amerithi tu serikali na amekuta kuna watu ambao walikuwa ni wahafidhina wa utawala uliopita."

Katikati ya mwezi Disemba 2021, Rais Samia alihutubia kongamano la vyama vya siasa jijini Dodoama, na akatoa uwanja kwa vyama hivyo kujadili na kupendekeza kwa serikali mambo yatakayo imarisha demokrasia na shughuli za kisiasa.

Hakuna ushahidi wala kauli kwamba mabadiliko haya ni sehemu ya mapendekezo ya vyama vya siasa. Ila kwa wale wanao tamani utawala wa sasa uiweke nchi katika mkondo mpya-tofauti kidogo na awali , mabadiliko haya yanatoa matumaini ya kuanza kwa enzi mpya ya utawala wa Rais Samia.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here