Elanga akimfunga kipa wa Atletico madrid
Licha ya Manchester United kuwa na msimu wa kusuasua, Anthony Elanga amekuwa akionyesha kiwango kikubwa tangu kuanza kwa msimu.
Mshambuliaji huyu wa pembeni kinda, aliifungia Manchester United goli muhimu la kusawazisha katika mchezo wa 16-bora wa ligi ya mabingwa Ulaya usiku wa Jumatano.
Elanga alipachika bao hilo akitokea benchi katika kipindi cha pili. Alifunga bao pia mwishoni mwa juma katika ushindi wa 4-2 dhidi ya Leeds United, mchezo wa ligi kuu.
Hilo lilikuwa bao lake la pili kwenye ligi kuu katika michezo 9 aliyocheza msimu huu. Kwa ujumla mabao matatu aliyoifungia United kwenye michezo 11 aliyocheza msimu huu, si rekodi mbaya, ukichukulia ni mara mbili tu amemaliza kucheza dakika zote 90, na kwa umri wake na ushindani wa ligi kuu ulivyo.
Elanga 'aonesha umahiri wake' wakati United inamhitaji zaidi
Unaweza kuwa umekosea kumpa kongole kocha wa sasa wa United, Rangnick kwa kiwango cha kinda huyo wa Sweden. Mtangulizi wake Ole Gunnar Solskjaer alimpa nafasi ya kucheza kwa mara ya kwanza msimu uliopita mshambuliaji huyo wa timu ya taifa ya Sweden ya chini ya miaka 21. Na ndiye aliyempandisha kutoka kikosi cha vijana kuja timu ya wakubwa msimu huu.
Lakini ilikuwa kwa mara ya kwanza Rangnick alipomuona Elanga mazoezini, siku moja baada ya United kuichapa Arsenal, Disemba 2, 2021. Akiwa mazoezini kwa mara ya kwanza chini ya Mjerumani huyo, alifurahia sana uwezo wake.
Hilo likafanya kocha huyo kuzuia mpango wa kinda huyo kutolewa kwa mkopo mwezi Januari, na hapo kila mtu alijua atacheza mechi nyingi msimu huu, lakini hakuna aliejua kwamba angecheza kwa kiwango cha hali ya juu kama anavyofanya sasa.
"Tangu siku ya kwanza mazoezini, siku moja kabla ya mchezo wetu na Crystal Palace, alinionyesha anachoweza kufanya," alikumbuka Rangnick. "Alionyesha uwezo wake huo kwenye mazoezi.
"Ni kijana mkarimu, anavyafana vitu vyake kwa uhakika, anasikiliza vile anavyotakiwa kufanya na anajaribu kujituma kuboresha kiwango chake."
Anthony Elanga
Elanga ana uraia wa Sweden, lakini alihamia Manchester akiwa na umri wa miaka 12 baada ya baba yake Joseph, mchezaji wa kimataifa wa zamani wa Cameroon aliyeichezea nchi hiyo kwenye kombe la dunia la mwaka 1998 kustaafu.
Hakukaa sana kwenye klabu ya vijana ya Hattersley kabla ya wasaka vibaji kubaini kipaji chake. United ilifanikiwa kumnasa ikiwapiku Manchester City, na vilabu vingine vikubwa Ulaya vilivyokuwa vinamtaka kinda huyo mwenye kasi.
Disemba mwaka jana, amepewa mkataba mpya utakaomuweka Old Trafford mpaka 2026.
"Lengo langu siku zote ni kuichezea Manchester United," alisema Elanga wakati huo anasaini mkataba. "kiwango hapa ni cha hali ya juu, lakini mkataba ni jambo muhimu kwenye safari yangu hii muhimu."
Ingawa ndio kwanza ametoka kusaini mkataba mpya miezi mitau iliyopita, tafsiri ya wengi ni kwamba, anaonekana ni jicho la Manchester kwa miaka mingi ijayo.
Elanga daraja moja la makinda yanayotamba EPL
Elanga ni miongoni mwa makinda yanayotajwa kufanya vizuri katika ligi na wanaopewa nafasi ya kuzibeba timu zao. Ni kama Arsenal wanavyowatumia wakali wao kutoka kituo chao cha kukuza vipaji cha Hale End, kina Bukayo Saka na Emile Smith-Rowe, Liverpool wana Curtis Jones licha ya uwepo wa Mo Salah na Sadio Mane na pale Barcelona kuna vijana kama Pedri, Gavi na Ansu Fati.
Kuna wakati Jadon Sancho, licha ya kununuliwa kwa bei kubwa ilimlazimu kukaa nje, kumpisha kijana huyu kucheza. Wachezaji wengine wakongwe kwenye klabu yake, akiwemo Christiano Ronaldo, wamekuwa wakimsaidia kukua kisoka, akitumika kama 'kaka mkubwa', kumuhamasisha kinda huyo. Elanga, 19, alikosa penati muhimu mwezi uliopita na kusababisha United kutolewa katika michuano ya Carabao Cup. Ronaldo alikuwa wa kwanza kumfariji. Marcus Rashford aliandika kumuambia kijana huyo asikate tamaa.
Wote hawa wanafahamu uwezo wake, na wanatambua kuwa ni mmoja wa wachezaji wanaotarajiwa kutwishwa jukumu kubwa la kuibeba Manchester United katika miaka sita mpaka 10 ijayo. Akianza sasa kuonyesha uwezo wake wa kuitoa shimoni timu hiyo.


No comments:
Post a Comment