Siku ya Wanawake Duniani: Ina maana gani Afrika? - KABATA

This is the special room for news where you need to settle with!


Breaking

Tuesday 8 March 2022

Siku ya Wanawake Duniani: Ina maana gani Afrika?

 

Farmer in Malawi supported by UN Women.

CHANZO CHA PICHA,UN WOMEN/BENNIE KHANYIZIRA

Kila mwaka Machi 08, Umoja wa Mataifa husheherekea haki zilizopatikana kwa bidii za wanawake- na kuangazia changamoto ambazo bado ziko mbele katika kukomesha ubaguzi wa kijinsia katika karibu nyanja zote za maisha.

"Usawa wa kijinsia wa leo, kesho na endelevu" ndio kauli mbiu ambayo Umoja wa Mataifa umeichagua mwaka huu kuadhimisha kile kinachojulikana rasmi kama Siku ya Kimataifa ya Wanawake.

Kwa nini imechagua mada hii?

Dkt Maxime Houinato, mkurugenzi wa Umoja wa Mataifa wa Wanawake katika kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, aliiambia BBC kwamba "kukuza usawa wa kijinsia katika mazingira ya mzozo wa mabadiliko ya tabia nchi na upunguzaji wa hatari ya majanga ni mojawapo ya changamoto kubwa duniani kwa karne ya 21".

"Wanawake na wasichana wanapitia athari kubwa zaidi za mabadiliko ya tabia nchi," aliongeza.

Kwa kweli, utafiti wa Umoja wa Mataifa unaonesha kuwa wanawake na wasichana hufa kwa idadi kubwa katika majanga ya asili.

"Kwa mfano, asilimia 95 ya waliofariki katika mafuriko ya visiwa vya Solomon 2014 walikuwa wanawake, 55% ya waliofariki katika tetemeko la ardhi la 2015 nchini Nepal walikuwa wanawake na 59% ya waliokimbia makazi yao kufuatia Kimbunga Idai mwaka 2019 nchini Malawi walikuwa wanawake," UN Women imesema kwenye tovuti yake

People walk on the flooded street of Buzi, central Mozambique, on March 20, 2019 after the passage of the cyclone Idai

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,

Vimbunga vimesababisha athari kubwa kusini mwa Afrika

Zaidi ya hayo, majanga yanayohusiana na hali ya hewa yamezidisha matatizo ya kijamii na kiuchumi.

"Nchini Uganda, kwa mfano, upotevu wa mifugo, upungufu wa mazao, na ukosefu wa chakula kutokana na ukame uliokithiri, na uvamizi wa nzige ulibainika kuongeza idadi ya wanafunzi walioacha shule, kulazimisha wasichana kufanya kazi zaidi , na kuongeza matukio ya ndoa za utotoni kwa kubadilishana kwa chakula," makala katika wakala wa habari unaolenga maendeleo, Inter Press Service, inaeleza.

Siku ya Kimataifa ya Wanawake ilianzaje?

Siku ya wanawake ilikuja kutokana na vuguvugu la wafanyakazi mnamo mwaka 1908, na ikatambuliwa rasmi kama hafla ya kila mwaka na miongo kadhaa baadaye, mnamo 1975.

Mnamo mwaka 1908, zaidi ya wanawake 15,000 waliandamana katika jiji la New York kudai muda mfupi wa kufanya kazi, malipo bora na haki ya kupiga kura.

Chama cha Kisoshalisti cha Marekani kilitangaza Siku ya Kitaifa ya Wanawake ya kwanza nchini Marekani mwaka mmoja baadaye.

Mjerumani Marxist na mwanaharakati Clara Zetkin alikuwa mmoja wa waasisi wa utambuzi wa toleo la kimataifa la Siku ya Kitaifa ya Wanawake ya Marekani.

RUSSIA - CIRCA 1900: Clara Zetkin (1857-1933), German politician, in Moscow during a military parade.

CHANZO CHA PICHA,HARLINGUE

Maelezo ya picha,

Clara Zetkin alikuwa anaongoza mapambano ya haki za wanawake

Zetkin alijumuika na wanawake 100 kutoka nchi 17 katika Kongamano la Kimataifa la Wanawake Wanaofanya Kazi katika mji mkuu wa Denmark Copenhagen mwaka 1910.

Mkutano huo kwa kauli moja ulikubaliana na pendekezo la Zetkin kwamba kuanzia mwaka unaofuata Siku ya Wanawake itaadhimishwa nchini Austria, Denmark, Ujerumani na Uswizi.

Wazo la Zetkin la Siku ya Kimataifa ya Wanawake halikuwa na tarehe maalum.

Ilirasimishwa baada ya mgomo wa baada ya vita, wanawake nchini Urusi mwaka 1917. Wanawake walidai "mkate na amani" - na siku nne za mgomo wa wanawake, Tsar alilazimika kujiuzulu na serikali ya muda hiyo iliwapa wanawake haki ya kupiga kura.

Tarehe ambayo mgomo wa wanawake ulianza kwa kalenda ya Juliana, ambayo wakati huo ilikuwa ikitumika nchini Urusi, ilikuwa Jumapili Februari, 23.

Siku hii katika kalenda ya Gregori ilikuwa Machi 8. Huu ndio wakati ambapo sasa inaadhimishwa kama siku ya mapumziko nchini Urusi na nchi zingine takribani dazeni mbili.

Vipi kuhusu Afrika?

Siku ya wanawake duniani inaadhimishwa kama sikukuu ya umma katika nchi saba za Afrika. Hii ni pamoja na Eritrea, katika kutambua mchango mkubwa ambao wanawake na wasichana walitoa - kama wapiganaji - katika mapambano ya muongo mzima ya uhuru wa nchi hiyo.

Fighters of the Eritrean People's Liberation Front (EPLF) are considered equal among their male colleagues in the struggle for an independent Eritrea, 20th June 1978

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,

Wanawake walipigana sawa na wanaume nchini Eritrea, wakati wa mapambano ya kupata uhuru

Mataifa mengine ya Afrika ambayo yametangaza tarehe 8 Machi kuwa siku ya mapumziko ni Angola, Burkina Faso, Guinea-Bissau, Sierra Leone ,Uganda na Zambia.

Huko Madagascar, ni siku ya mapumziko kwa kwa wanawake pekee.

Baadhi ya nchi za Kiafrika zina Siku yao ya Wanawake - Afrika Kusini inaadhimisha kama siku ya mapumziko tarehe 9 Agosti kwa heshima ya wanawake 20,000 walioandamana siku hiyo mwaka 1956 kupinga sera za kibaguzi ya utawala wa wazungu wachache uliokuwa madarakani kwa wakati huo.

"Unampambana na mwanamke, unagonga mwamba," wanawake hao waliimba huku wakielekea kwenye kiti cha mamlaka ya serikali katika mji mkuu wa Pretoria.

Mbali na hayo, Umoja wa Afrika umetangaza tarehe 31 Julai kuwa Siku ya Wanawake wa Afrika.

AU inasema siku hiyo inalenga "kutambua na kuthibitisha" nafasi ya wanawake katika "kufikia uhuru wa kisiasa wa Afrika na kuendeleza hali ya kijamii na kiuchumi ya wanawake katika bara hilo".

Ingawa bado kuna mengi yanahitajika kufanywa ili kufikia usawa wa kijinsia.

Wanawake barani Afrika wamepata mafanikio makubwa ambapo takwimu za Umoja wa Mataifa za mwaka 2021 zinaonesha kuwa Rwanda ina idadi kubwa ya wanawake bungeni - 61%, ikifuatiwa na Cuba na Bolivia zenye 53% kila moja na Umoja wa Falme za Kiarabu kwa 50%.

Afrika Mashariki na Kusini ndizo zenye uwakilishi mkubwa zaidi wa wanawake bungeni katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara - 32% kufikia Disemba 2020, ikilinganishwa na wastani wa kimataifa wa 24.5%.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here