Ni mwezi mmoja sasa na siku kadhaa tangu kuanza kwa vita kati ya Urusi na Ukraine, huku dunia ikiendelea kushuhudia athari mbalimbali zilizojitokeza kutokana na mgogoro huo.
Punde tu, baada ya kuanza kwa vita hivyo mwezi jana, Zanzibar ilijikuta ina watalii kutoka nchini Ukraine wapatao 1000 wakiwa hawajui hatima yao ya kuwa ugenini na ile ya familia zao.
Hata hivyo, kutokana na jitihada mbalimbali, wengi wao hivi sasa wameondoka na kwenda kuanza maisha katika nchi nyengine kama vile Ufaransa, Ujerumani na hata Uhispania.
TWATAKA KUSIKIA KUTOKA KWAKO:Wewe au jamaa zako mlitoroka vita Ukraine?Lakini kuna wale walioamua kubaki nchini Tanzania licha ya kupata fursa ya kwenda kuanza maisha katika nchi za Ulaya.
Miongoni mwao wanasema, wanahisi wako salama zaidi Zanzibar kuliko kuwa sehemu nyengine ya dunia.
Olha, ni mtalii kutoka Ukraine, ambae kwa mwezi mmoja sasa amejikuta amekwama na mwenzake baada ya kufika Zanzibar kufanya utalii. Kabla ya vita kuanza walikuwa katika moja wa hoteli za kitalii, lakini baada ya vita tu kuanza, maisha yakabadilika. Fedha za matumizi zikawaishia, hali iliyowalazimu kubadilisha mfumo wa maisha na kwenda kuishi sehemu ya bei rahisi zaidi.
Hata hivyo, licha hivi sasa ya kupewa hifadhi ya bure katika moja wapo ya hoteli zinazomilikiwa na raia wa Ukraine, lakini changamoto yao kubwa ni fedha za kujikimu kila siku. Hivyo wakati mwingine, hutegemea msaada wa chakula kutoka kwa wasamaria wema, hasa wenyeji wa Matemwe.
Hivi karibuni, Olha na mwenzake, walipata nafasi ya kwenda Poland lakini wakaikataa. Wanasema, wanajihisi wapo salama zaidi wakiwa Zanzibar.
"Tunajisikia tuko salama zaidi hapa. Tutakaa hapa mpaka vita vitakapokwisha, baada ya hapo tutaona nini cha kufanya. Tulipata nafasi ya Kwenda Poland, lakini tuliamua kubaki hapa baada ya kuona raia wengi kutoka Ukraine wameingia Poland," anasema Olha.
Waswahili wanasema, mgaagaa na upwa, hali wali mkavu. Hii inaonekana kwa baadhi ya watalii wanaoendelea kujishughulisha na kazi za mitandaoni ili kujipatia kipato cha kuweza kujikimu kimaisha.
Ozirnyi Kyrylo yeye ni mfanyabiashara wa soko la hisa. Licha ya kukwama nchini Tanzania, lakini ameweza kutumia ujuzi wake kuendelea kufanya kazi kupitia mtandaoni. Kipato chake, kimemsaidia kulipa kodi ya nyumba lakini pia kumtumia mama yake ambae yuko ugenini fedha za kijikimu.
"Mimi ni mfanyabiashara wa soko la hisa. Kwangu mimi kitu muhimu ni kuwepo kwa mtandao, ambao ninao hapa, hii ni kama ofisi yangu, mara nyengine nafikiria kuhusu vita, lakini sasa hivi familia yangu iko sehemu salama, hivyo mara nyingi najikita katika kufanya kazi," anasema Ozirnyi Kyrylo.
Lakini kadri vita vinavyoendelea, miundombinu nayo inazidi kuharibika huku makampuni na mashirika yakiendelea kuyumba na kuwa hatarini kusitisha shughuli zake nchini Ukraine. Hii inaondoa matumaini ya baadhi wanaofanya kazi kwa njia ya mtandaoni.
Ivanna Leibiuk ambae amekwama Zanzibar na binti yake Veronica mwenye umri wa miaka 12, yeye ni mtaalamu wa masuala ya IT na amekuwa akiendelea na kazi yake kwa kutumia laptop. Hata hivyo, hivi sasa amejawa na wasiwasi wa kupoteza kibarua ambacho ndio tegemeo lake.
"Nafanyakazi katika kampuni ya IT kupitia laptop yangu, lakini mambo hayatabiriki, nahofia kupoteza kazi yangu wakati wowote kwa sababu mambo hayataribiki kutokana na vita,"anasema Ivanna Leibiuk.
Ingawa, idadi kubwa wa watalii hawa hivi sasa wamehama katika hoteli za kitalii na kutafuta makazi ya muda uraiani, lakini hoteli nyingi za kitalii zimeendelea kuwa na msaada mkubwa kwao. Gilbert Kazungu ni Meneja Mkuu wa hoteli ya Amani Beach Bungalow, anasema walikuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanatoa kila aina ya msaada ikiwemo kuwapa punguzo la chini kabisa baadhi ya watalii waliokwama.
"Tunajua kwamba, shida zinakwisha, na hawa watalii iko siku watarudi Zanzibar kutokana na ukarimu wetu," anasema Gilbert Kazungu.
Hivi sasa, katika maeneo mingi ya utalii Zanzibar, kama vile Nungwi, Matemwe na hata Paje, ule msemo wa mgeni aje mwenyeji apone umebadilika. Baadhi ya wenyeji hivi sasa wao ndio wamekuwa msaada mkubwa kwa wageni wao.
Juma Abdallah ambae ni 'Beach Boy' Nungwi, anasema hali ya baadhi ya wageni inasikitisha na wakati mwengine analazimika kuwapelekea msaada wa chakula wageni wake.
Hivi sasa msimu wa utalii uko chini, hali inayowafanya baadhi ya watalii hawa waliokwama kuweza kuyamudu maisha katika eneo ambao maisha yake ni ghali kutokana na kuendeshwa na shughuli za utalii.
Swali ni je, lini mgogoro huu utapata ufumbuzi ili kuwanasua maelfu ya raia waliopo katika maeneo mbalimbali duniani?
Mengi zaidi
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
- SILAHA:Mzozo wa Ukraine:Makombora ya stinger na silaha nyingine kali zinazotumiwa Ukraine


No comments:
Post a Comment