Wanawake wafanyakazi wa Tume ya Madini Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani, wamesherehekea siku hiyo na watoto yatima na wenye kuishi kwenye mazingira magumu wamekabidhi vyakula katika kituo cha Light In Africa, Mirerani.
Mfanyakazi wa Tume ya Madini Mirerani, Zainab Athuman amesema wamewakabidhi watoto hao vyakula mbalimbali ikiwemo mchele, soda, sabuni, mafuta na kula nao keki.
Zainab amesema wameshiriki siku hiyo kwa kuwatembelea watoto hao, kuwapa vyakula na kula keki pamoja katika kuwathamini watoto hao.
"Wafanyakazi wote wa Tume ya Madini Mirerani tumeshiriki kuchanga fedha zetu na kununua zawadi hizi za watoto hawa yatima na wenye kuishi kwenye mazingira hatarishi," alisema.
Mmoja kati ya watoto hao, Caroline Zacharia amewashukuru wanawake hao kwa kuwapatia msaada huo.
Caroline amesema watu wanapowatembelea na kuwapatia msaada hujisikia faraja na kuona wanapendwa na jamii inayowazunguka.
Mwenyekiti wa bodi ya Light In Africa, Vincent Mamasita amewasihi wadau wengine waige mfano huo katika kuwachangia watoto wenye uhitaji.
Mamasita amesema katika kituo hicho cha Light In Africa Mirerani wanawahudumia na wamewagawa watoto wakiume, wakike na walemavu.
No comments:
Post a Comment