Mamlaka nchini Morocco zimepiga marufuku filamu yenye utata ya Uingereza ya Lady of Heaven, baada ya kulaaniwa na baraza la kidini la nchi hiyo.
Filamu hiyo inadai kueleza kisa cha Bibi Fatima, bintiye Mtume Muhammad. Baraza Kuu la Ulamaa lilisema sinema hiyo ilikuwa ya "uongo wa wazi" wa Uislamu. Kumekuwa na maandamano ya kupinga filamu hiyo nchini Uingereza.
Wiki iliyopita, baadhi ya wanaoaipinga nchini Uingereza waliandamana kwenye maeneo kadhaa huku zaidi ya watu 120,000 wakitia saini zao isionyeshwe kwenye majumba ya sinema nchini humo.
Nchi za Misri, Pakistan, Iran na Iraq pia zimepiga marufuku na kulaani filamu hiyo. Baraza hilo lilishutumu filamu hiyo kwa "upendeleo wa kuchukiza" na kuwashutumu watengenezaji wa filamu kwa kutafuta "umaarufu" na "kuumiza hisia za Waislamu na kuchochea hisia za kidini", kulingana na vyombo vya habari vya serikali ya Morocco.
Mhariri wa Dini wa BBC, Aleem Maqbool, anasema ukosoaji unatokana na jinsi mtayarishaji filamu na kasisi wa Kiislamu wa Shia, Yasser Al-Habib, alivyowaonyesha watu mashuhuri katika Uislamu wa awali wa Kisunni, akimaanisha kwamba kuna ulinganisho kati ya matendo yao na wale wa kundi la Islamic State nchini Iraq.
Mtayarishaji wa filamu hiyo Malik Shlibak amewasuta wanaotaka filamu hiyo kufungiwa kwenye mitandao yake ya kijamii na kueleza kuwa ni ushabiki na kuwaambia iwapo hawaipendi filamu hiyo wasiitazame, tofauti na kuizuia.

No comments:
Post a Comment