Kikosi cha KMC FC kimeanza maandalizi kuelekea katika mchezo unaokuja wa Ligi Kuu ya NBC soka Tanzania Bara dhidi ya Namungo utakaopigwa Januari 24 katika uwanja wa Uhuru hapa Jijini Dar es salaam.
Kikosi hicho cha Wana Kino Boys kimeanza leo maandalizi hayo ikiwa ni baada ya kutoka kucheza mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar uliomalizika kwa sare ya goli moja kwa moja Januari 13 katika uwanja wa Manungu na hivyo kupewa siku mbili za mapumziko na kurejea jana jioni .
Timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni chini ya kocha Mkuu Thierry Hitimana itakuwa nyumbani kwenye mchezo huo ambapo mipango mikakati ni kuhakikisha kwamba inafanya vizuri na hivyo kusogea kwenye nafasi iliyopo kwa sasa na kupanda kwenye nafasi za Juu.
” Tumeanza leo maandalizi ya mchezo mwingine dhidi ya Namungo, utakuwa mchezo mgumu kutokana na kwamba kila mmoja anataka kufanya vizuri kwenye michezo hii iliyobakia kabla ya kumalizika kwa msimu wa 2022/2023 hivyo kama Timu tuna muda wa kujiandaa vizuri.
Katika maandalizi hayo KMC FC inawakosa wachezaji watatu kutokana na sababu ya majeraha ambo ni Ibrahimu Ame, Awesu Ally Awesu pamoja na Hance Masoud Msonga huku Emmanuel Mvuyekure akiendelea vizuri na hivyo muda wowote atajiunga na wenzake ili kuongeza nguvu kwenye michezo iliyobakia.
Aidha mbali na wachezaji hao wengine waliobakia wamerejea wakiwa na hali na morali ya kujiandaa vema dhidi ya Namungo na hivyo kuhakikisha kwamba Timu ya Manispaa ya Kinondoni inafanya vizuri kwenye michezo iliyobakia.
” Ukiangalia kwa mujibu wa ratiba ya Bodi ya Ligi kuu Tanzania (TPLB) tutakuwa na muda mrefu wakufanya maandalizi kabla ya mchezo wetu dhidi ya Namungo kutoka leo Januari 16 hadi 24 na kwamba program ya kocha Mkuu Hitimana itakuwa ni kufanya mazoezi ya uwanjani , Bichi pamoja na kucheza mechi za kirafiki ambazo zitasaidia kuwaweka sawa wachezaji kwa kipindi hiki tukiwasubiria wapinzani wetu.
Hadi sasa KMC FC imeshacheza jumla ya mechi 20 ikiwa imebakiza michezo 10 na hivyo kukusanya jumla ya alama 23 huku ikiwa kwenye nafasi ya tisa mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC soka Tanzania Bara na kwamba malengo ni kuhakikisha kwamba Timu inafanya vizuri kwenye michezo iliyobakia na hivyo kumaliza msimu kwenye nafasi nzuri.
No comments:
Post a Comment