Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, wakati alipowasili katika uwanja wa ndege wa Songwe, kwa ziara ya kikazi mkoani Mbeya na Songwe Januari 16, 2023. Kushoto ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya, Dkt. Stephen Mwakajumulo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa eneo la Mbalizi Mkoani Mbeya, baada ya kuwasili mkoani humo kwa ziara ya kikazi katika Mikoa ya Mbeya na Songwe Januari 16, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa Mbeya mjini, baada ya kuwasili mkoani humo kwa ziara ya kikazi katika Mikoa ya Mbeya na Songwe Januari 16, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
***********************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wananchi kuwa walinzi wa mbolea ya ruzuku iliyotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuhakikisha inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ya kuongeza uzalishaji wa mazao katika msimu wa 2022/2023 litimie.
Amesema kuwa kumekuwa na watanzania wachache wasiokuwa na nia njema wanaotorosha mbolea kwenda nchi jirani na kuwaacha watanzania bila kuwa na mbolea ya kutosha ”jambo hili lazima tulikemee na tulisimamie sote ili kuhakikisha mbolea iliyopo nchini ni kwa ajili ya watanzania, kila mmoja awe mlinzi kwa mwenzake”
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Januari 16, 2023) wakati akisalimia na wananchi kwenye eneo la Mbalizi jijini Mbeya akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali. Amesema utoaji wa ruzuku hiyo ya mbolea unalenga kuongeza uzalishaji wa chakula nchini na ni marufuku kuiuza nje.
Ameongeza kuwa awali mbolea iliuzwa kwa zaidi ya shilingi 100,000 lakini Mheshimiwa Rais Dkt. Samia akaridhia kutoa ruzuku shilingi bilioni 150 ili ikashushe bei ya mbolea na sasa inauzwa kwa shilingi 70,000. ”Tusikubali fedha hiyo kutumika nje la malengo, tulinde mbolea yetu isiuzwe kwa wasiohusika.”
”Nimefurahi sana kwa hatua zilizochukuliwa mkoani Songwe, tani 2199 zimekamatwa zikipelekwa nchi jirani hii haikubaliki, watanzania tuwe walinzi hii ni pesa yetu inatoroshwa na wachache, malengo yetu ni kuwahudumia ninyi kwa usimamizi wa Rais Dkt. Samia”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuelekeza hatua zilizofikiwa katika maendeleo ya uboreshwaji wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Songwe kuwa tayari njia ya kurukia ndege imekamilika kwa asilimia 100, jengo la abiria ujenzi umefikia asilimia 96 na sasa zoezi la ufungaji taa linaendelea na litakapokamilika uwanja huo utatumika wakati wote.
”Tunafanya hivi ili kuvuta masoko kutoka nchi jirani ikiwemo Kongo, Zambia na malawi walete ndege zako, haya yote yanafanywa na Rais wetu Dkt. Samia kwasababu ana maono ya mbali na dhamira yake ya dhati ya kuwaletea watanzania maendeleo.”
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ameidhinisha kiasi cha shilingi bilioni 3.3 kwa ajili ujenzi wa mradi wa maji wa Shongo – Igale ambao umekamilika na watu wanapata huduma ya maji.
Ameongeza kuwa, pamoja na mahitaji ya maji katika eneo la mbalizi kuwa lita milioni 8, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia alitoa shilingi bilioni. 4.8 kwa ajili ya kujenga mradi wa maji wa Inunga ili kuongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 8 hadi 12.
Naye, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, David Silinde amesema Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 580 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 29 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ambapo yote yamekamilika kwa asilimia 100 na yanatumika.
Awali, baadhi ya wananchi walimuomba Mheshimiwa Majaliwa awasaidie katika kutatua changamoto ya fidia iliyotokana na kupisha ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe tangu mwaka 2002, ambapo Meneja wa uwanja huo, Mhandisi Danstan Komba alisema wanachodai wananchi hao ni mapunjo ya fidia.
Alisema baada ya eneo lao kutwaliwa walilipwa fidia ambapo baadae yalitokea malalamiko ya mapunjo ya fidia ambapo timu ya uchunguzi ya suala hilo iliundwa na ilishafika katika eneo hilo, hivyo aliwaomba wananchi watulie wakati suala lao linaendelea kufanyiwa kazi.
No comments:
Post a Comment