SERIKALI YATOA BILIONI 17.8 UJENZI WA VIVUKO VIPYA VITATU MWANZA - KABATA

This is the special room for news where you need to settle with!

Thursday, 26 January 2023

SERIKALI YATOA BILIONI 17.8 UJENZI WA VIVUKO VIPYA VITATU MWANZA


Na. Alfred Mgweno (TEMESA MWANZA)
Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA)
imetoa zaidi ya Shilingi Bilioni 17 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vivuko
vipya vitatu Mkoani Mwanza. Vivuko hivyo vitatu, vimeanza kujengwa
kwa ajili ya kutumika katika ziwa Victoria katika maeneo ya Ijinga
Kahangala Wilayani Magu Mkoani Mwanza, Bwiro Bukondo Wilayani
Ukerewe Mkoani Mwanza, pamoja na Nyakaliro Kome Halmashauri ya
Buchosa Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza.

Akizungumza katika hafla fupi ya zoezi la uwekaji wa Msingi wa Kivuko
(Keel Laying) iliyofanyika mapema leo katika Yadi ya Songoro iliyopo
Ilemela Mkoani Mwanza, mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.
Adam Malima ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji huo mkubwa ikiwa ni
katika mkakati wa kuondoa kero ya usafiri kwa wananchi wa Mkoa wa
Mwanza na watanzania kwa ujumla na kusema uwekezaji huo utainua
hali za kiuchumi na kijamii za jamii zote zitakazonufaika.
‘‘Uzinduzi wa ujenzi wa vivuko hivi vitatu tunaoufanya leo ni hatua
muhimu ya kuanza ujenzi rasmi wa Vivuko hivi hivyo niwatake wahusika
wote kuhakikisha ujenzi huu unakamilika kwa wakati na viwango vya hali
ya juu ili kutimiza azma ya Serikali kuwaondolea kero wananchi na
kuwaletea maisha bora.“ Alisema Mhe. Malima na kuipongeza Serikali
ya Awamu ya Sita kwa kuwezesha utekelezaji wa miradi hiyo mitatu ya
Vivuko kwa pamoja.

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) unaendelea na
ujenzi na ununuzi wa vivuko vipya vinane, kati ya vivuko hivyo, vivuko
vitano viko kwenye hatua ya ujenzi ambavyo ni Kisorya-Rugezi
ambacho ujenzi wake unaendelea, Bwiru-Bukondo, Nyakaliro-Kome,
Ijinga-Kahangala, na Mafia-Nyamisati huku mikataba yenye thamani ya
shilingi bilioni 33.2 ikiwa tayari imeshasainiwa na wakandarasi
wameshalipwa malipo ya awali. Aidha vivuko vitatu vilivyosalia vipo

kwenye hatua ya manunuzi na Ujenzi wake unatarajiwa kuanza katika
mwaka huu wa fedha.
Serikali pia kupitia TEMESA inafanya ukarabati wa vivuko 14 kwa
gharama ya shilingi bilioni 22.99 na ukarabati wa miundombinu ya
vivuko kwenye maeneo 11 kwa gharama ya shilingi bilioni .4.1 huku
mikataba yenye jumla ya shilingi bilioni 60.3 bilioni ikiwa
imekwishasainiwa na kazi zinaendelea.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Ludovick Nduhiye
ambaye amemuwakilisha Katibu Mkuu Ujenzi akizungumza katika hafla
hiyo amesema Vivuko hivyo ambavyo ujenzi wake unazinduliwa leo
vimekuwa ni hitaji kubwa kwa wananchi wanaoishi maeneo ambayo
vivuko hivi vitaenda kutoa huduma baada ya ujenzi wake kukamilika na
hivyo mategemeo ya Wizara ni kwamba wananchi katika maeneo husika
watatumia fursa ya kuimarishwa kwa usafiri, kuimarisha shughuli zao za
kiuchumi na kijamii ili kuifikia azma ya Serikali ya kuwaletea maendeleo
wananchi.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania
(TEMESA) Lazaro Kilahala akisoma taarifa fupi ya miradi hiyo amesema
kukamilika kwa ujenzi wa vivuko hivyo kutawapatia wananchi wa
maeneo ya Nyakaliro Kome, Bwiro Bukondo na Ijinga Kahangala
pamoja na wana Mwanza na watanzania kwa ujumla uhakika wa usafiri
unaowaunganisha na hivyo kuchochea ukuaji wa shughuli zao za
kiuchumi na kuwawezesha kupata huduma mbalimbali za kijamii kwa
haraka zaidi.
Mtendaji Mkuu amebainisha kuwa kivuko cha Ijinga Kahangala
kinagharimu kiasi cha shilingi billioni 5.2 na kitakuwa na uwezo wa
kubeba abiria 200 na magari 10 sawa na tani 100, kivuko cha Bwiro
Bukondo kinagharimu kiasi cha shilingi bilioni 4.5 na kitakuwa na uwezo
wa kubeba abiria 200 na magari 10 sawa na tani 100 wakati kivuko cha
Nyakaliro Kome kinagharimu kiasi cha shilingi bilioni 8 na kitakuwa na
uwezo wa kubeba abiria 800 na magari 22 sawa na tani 170.

Kilahala ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa
kuuwezesha kifedha Wakala kutekeleza miradi hiyo na kuahidi kufanya
kazi kwa weledi na jitihada kubwa ili kufikia malengo na matarajio ya
Serikali na wananchi kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment