Share
Na Mwandishi wetu, Babati
ASKARI wanawake wa vyombo vya ulinzi na usalama Mkoani Manyara, wamewapatia msaada wa kibinadamu familia mbili za wajane wanazoishi maisha duni za Wilaya za Babati na Hanang’ ili kuwapunguzia ugumu wa maisha.
Askari wanawake hao wa vyombo vya ulinzi na usalama kupitia mtandao wa polisi wanawake (TFNET) wametoa misaada hiyo baada ya kuzitembelea na kubaini hali zao duni.
Misaada hiyo imetolewa kwa mjane Zaituni Haji wa kitongoji cha Walangi B Wilaya ya Babati na Paskalina Gidad wa kijiji cha Ming’enyi Wilayani Hanang’.
Mwenyekiti wa TFNET, mrakibu mwandamizi wa polisi (SSP) Georgina Matagi ambaye pia ni mkuu wa kikosi cha usalama barabarani (RTO) Mkoa wa Manyara, ameongoza tukio hilo la kukabidhi misaada hiyo kwa wajane hao wenye watoto watano kila mmoja kwa nyakati tofauti.
Matagi amesema wamekabidhi pikipiki moja kwa kila familia ili kuinua vipato vyao na kuwapatia vyakula, magodoro, sabuni na nguo za kuvaa kwa familia hizo.
Amesema waliokabidhiwa misaada hiyo ni watu wanaostahili kwani walifanya utafiti kupitia polisi kata na viongozi wa kata na vijiji ili kujiridhisha kuwa ni wahitaji na wanakidhi vigezo na wataenda kila wilaya na kufanya hivyo.
“Zaituni huyu mama, mume wake alifariki akiwa hana kiwanja ila amepambana akanunua kiwanja na kujenga chumba kimoja na ana hati, kiwanja ni chake hakuna mtu wa kumsumbua,” amesema Matagi.
Amesema mama huyo analima mboga na anawapa watoto wake wazungushe asubuhi wakimaliza wanaenda shule siku moja moja na kunasababisha utoro ila pikipiki waliyompatia itaondoa utoro maana wataongeza kipato zaidi.
Akiwa kijiji cha Ming’enyi amesema watoto wa mjane huyo walikuwa wanalala na mifugo yaani mbuzi na nguruwe nyumba moja kwa sababu ya ugumu wa maisha.
Zaitun Haji wa Babati akizungumza huku akibubujikwa na machozi huku akiwashukuru askari hao amesema alikuwa analala kanisani akiomba Mungu ayainue maisha yake.
Mjane wa Hanang’ Paskalina Gidad amewashukuru askari hao wa kike kwa kumpatia msaada wa pikipiki, vyakula, sabuni, mashuka, mablanketi na nguo.
Akiwapokea maaskari hao mkuu wa wilaya ya Hanang’ Janeth Mayanja amewapongeza na kuwataka kupigania usawa wa kijinsia katika jamii kwani harakati hizo zinaanza na wao.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ming’enyi Karan Sadan ameahidi kutoa bati 40 ili kumjengea nyumba mjane Paskalina na amewashukuru maaskari hao kwa msaada wao.
Awali, kabla ya kwenda kutoa misaada hiyo kamanda wa polisi mkoani Manyara, (ACP) George Katabazi akizungumza na askari hao wa kike kutoka vyombo vyote vya ulinzi amesema wameonesha mfano mzuri wa kuigwa.
Vikosi vilivyoshiriki ni askari polisi, magereza, jeshi la zima moto na uokoaji, uhamiaji, hifadhi ya Taifa ya Tarangire, taasisi ya wanyama pori (TAWIRI), Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) na SUMA JKT.
No comments:
Post a Comment