Wadau mbalimbali wanaoshiriki katika wiki ya AZAKI inayoendelea Jijini Arusha wamejengewa uwezo wa matumizi sahihi ya teknolojia katika ustahimilivu wa fedha ili kuziwezesha Asasi zao kujisimamia kiuchimi.
Akizungumza katika mdahalo uliofanyika Jijini humo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya FCS TRUST ambayo ni Kampuni tanzu ya Foundation For Civil Society (FCS) Arthur Mtafya amesema muda umefika kwa AZAKI kuwekeza miundombinu itakayosaidia kufanikisha mstakabali wa kukuza ustahimilivu wa fedha, na kuondokana na utegemezi wa wahisani wa nje.
Akizungumzia majukumu ya FCS TRUST, Mtafya ameeleza kuwa taasisi hiyo ilianziashwa kwa lengo la kutoa ushauri wa kitaalam kwenye maendeleo ya AZAKI na uwekezaji, kwaajili ya kutengeneza faida na kuchangia kwenye ustahimilivu wa taasisi mama ya Foundation For Civil Society.
Aidha, ametoa ushauri elekezi na mafunzo kwa AZAKI, ambapo taasisi hiyo pia imefanya uwekezaji kwenye maeneo mawili ambayo ni Soko la Mitaji na kwenye majengo.
"Kwa sasa tuna mikakati ya miradi miwili ambapo tuna jengo ambalo tunatarajia kulipangisha ili tupate faida, pia tumewekeza kwenye soko la mitaji na tayari tumeshaanza kupata faida kidogo ambayo baada ya muda tunaamini tunaweza kupata mtaji utakaowezesha kufanya uwekezaji kwenye maeneo mengine mbalimbali kwa ajili ya kupata fedha itakayochangia kuimarisha ustahimilivu wa kifedha wa taasisi mama". amesema Mtafya.
Pia, amefafanua kuwa moja ya eneo ambalo taasisi hiyo inalifanyiakazi ni kuzijengea uwezo AZAKI, na kwamba kwenye mdahalo huo wamepata fursa ya kuwasilisha kile ambacho wanafanya katika matumizi ya teknolojia inayosaidia ustahimilivu wa fedha.
"FCS Trust tuna uzoefu wa kutengeneza mifumo ndani ya hizi taasisi ambayo inaweza kurahisisha mambo yao mengi ya ndani lakini pia namna ya kuwasiliana na taasisi za nje".ameongeza Mtafya
No comments:
Post a Comment