Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amesema kuwa Serikali inakwenda kuanza ujenzi barabara ya Kibena - Lupembe (km 42) kwa kiwango cha lami ili kuufungua mkoa huo kiuchumi hasa kutokana na kilimo cha chai kinacholimwa katika kata ya Lupembe Halmashauri ya Njombe.
Ameyasema hayo mkoani Njombe Januari 23, 2024 wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Lupembe, tarafa ya Lupembe ambapo pamoja na mambo mengine amesema Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ameshatenga fedha takribani Bilioni 75 kwa ajili ya utekelezaji wa barabara hiyo.
“Tarafa hii inajulikana sana kwa kilimo cha chai na hii imempa nguvu Mheshimiwa Rais, ametoa maelekezo tumtafute Mkandarasi makini na tuanze kujenga kwanza km 42 kuanzia kibena kufika hapa lupembe”, amesema Bashungwa
Aidha, Bashungwa ameitaka Halmashauri ya Njombe kuweka mipango miji vizuri ili Ujenzi wa barabara hiyo utakapoanza Wananchi waweze kupata maendeleo kwa haraka.
Bashungwa amemtaka Meneja wa TANROADS Mkoa wa Njombe kuanza mapema hatua za manunuzi ya kumpata mkandarasi ili barabara hiyo iweze kujengwa na kukamilika kwa wakati.
Ameeleza kuwa barabara hii ipo kwenye ushoroba wa Njombe – Lupembe – Madeke – Mlimba – Ifakara - Mikumi yenye urefu wa kilomita 446.88 ambayo ni kiunganishi cha mkoa wa Njombe na Morogoro.
“Barabara hii ikikamilika itachochea ukuaji wa uchumi ikiwa ni pamoja na kupunguza muda wa usafiri, urahisishaji wa kufanya biashara na kuwezesha wananchi kuchangamana kwa urahisi, kuwezesha kufikika kwa urahisi kwenye vivutio vya utalii”, amefafanua Bashungwa.
Bashungwa ameongeza kuwa barabara hiyo ikikamilika itakuwa kizuri na barabara za ushoroba wa Makambako hadi Ruvuma.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Lupembe, Mhe. Edwin Swalle amesema kuwa wananchi wake kiu yao kubwa ni kupata barabara ya kiwango cha lami kwani wananchi wake wanalima sana zao la chai na mbao ambapo inahitaji miundombinu wezeshi ili kusafirisha maeneo mbalimbali na kupandisha bei ya soko la Chai.
Ameongeza kuwa uwepo wa barabara kwa kiwango cha lami utaibua wawekezaji wengi kuja kuwekeza katika Tarafa hiyo na hivyo kuchochea uchumi wa wananchi.
Waziri Bashungwa anaendelea na ziara ya kikazi mkoani Njombe ya kukagua miradi ya kimaendeleo ya barabara inayoendelea na ile iliyokamilika.
No comments:
Post a Comment