KAULI YA NYERERE ILIMBEBA LOWASSA, AKAAMINIKA CHADEMA/UKAWA - KABATA

This is the special room for news where you need to settle with!

Monday, 12 February 2024

KAULI YA NYERERE ILIMBEBA LOWASSA, AKAAMINIKA CHADEMA/UKAWA

 Mwaka 1995, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika moja ya mikutano na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM kuelekea uchaguzi Mkuu aliwahi kusema Kiongozi Safi  Hawezi Kutoka nje ya CCM.


Aliwasisitiza wajumbe wafahamu hivyo na waende kupiga kura kwa ajili ya kumpata mtu sahihi wa kuliongoza taifa la Tanzania.

Aliwataka wajumbe wapiga kura kuhakikisha wanamleta mtu wa kukidhi matarajio ya Watanzania.

Mwalimu alikiamini chama. Aliamini kuwa CCM ni tanuru linaloivisha viongozi katika kila eneo, uongozi bora, maadili, uzalendo na hata utumishi uliotukuka kwa Taifa.

Mwalimu hakuwa amebahatisha hicho alichokisema na ndio maana CCM inaendelea kushika dola kutokana na weledi wa viongozi wake. Kwa upande mwingine, kwenye tafakuri, hicho ndicho kinachokitesa, Chama cha Chadema.

Chama hicho kimekuwa kikipambana bila mafanikio kupata nafasi ya kushika dola Tanzania, lakini bado kauli ya Baba wa Taifa, inaendelea kutikisa kuwa bado Kiongozi Safi atatoka CCM.

Mchakamchaka wake, ulifika hatua, wakati wa uchaguzi wa mwaka 2020 baada ya Lowassa kushindwa kupenya kwa jina lake kukatwa, alifanya uamuzi mgumu wa kwenda Chadema.

Chadema imekuwa ikimezea mate viongozi wa CCM inapofikia uchaguzi. Inatamani kupata kiongozi mwenye ushawishi kuja kwenye chama chao kwa ajili ya kushika nafasi za juu za uongozi ikiwemo nafasi ya Urais.

Mwaka 2015, wakati Tanzania inaingia kwenye kinyang`anyiro cha uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani, wenyewe walikuwa hawafahamu nani asimame, mwenye ushawishi.

Chadema ilipumua baada ya Lowassa kutangaza kuingia upande wa pili na hapo sasa, moja kwa moja ilimtangaza kuwa ndiye mgombea Urais.

Wakati huo Chadema ilijipima na kuona hakuna mtu mwenye sifa, hakuna mtu safi na mwenye mvuto na hawakuwa na mtu mzito wa kupambana na mwamba wa CCM aliyekuwa akipeperusha bendera ya chama hicho, wakati huo; John Magufuli (hayati).

Baada ya kumalizika mchakato wa kupitisha majina matatu kwa ajili ya kuingia Halmashauri Kuu ya CCM kwa ajili ya kupiga kura, jina la Lowassa liliishia hukuhuku ndipo akajiunga na UKAWA.

Kitendo cha kupewa nafasi ya kusimama kama mgombea urais kupitia UKAWA, ni wazi kuwa alisimama na kuiwakilisha kauli ya Baba wa Taifa kuwa Kiongozi Safi Hawezi kutoka Nje ya CCM.

Hivyo ndivyo ilivyo. Ilifika hatua Lowassa alikuwa kama alama muhimu kuwa wananchi walitaka kumwona kiongozi safi kutoka CCM kwani wananchi hawakuwa wanawaelewa wengine kwa nafasi hiyo.

Kutokana na hilo, ndiyo maana kwenye mikutano yake, kulikuwa na maelfu ya watu  waliokuwa wanataka kumuona mtu kutoka CCM na wanataka kusikia anasema nini.

Nilipangiwa na ofisi niliyokuwa nafanya kazi wakati huo kwenda kuripoti mikutano ya kampeni, tulimaliza Kanda ya Ziwa kabla ya kuhamia mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, kote Lowassa alikuwa na mvuto, maelfu walianza kukusanyika tangu asubuhi na kufika jioni hata pa kusogeza mguu hakuna.

Hiyo yote ni kutokana na kupikwa na chama na wakati mwingine alikuwa akijisahau na kuitaja CCM kumbe yuko Ukawa.

Pamoja na hayo, ndoto ya Lowassa ilikuwa kupata urais, lakini bado peke yake alikuwa hatoshi kwa maana ya kwamba waliokuwa wanamzunguka, hawakutoka kwenye tanuru la CCM.
Hii ndiyo maana kila leo, kuna viongozi wengi, wapo waliokuwa viongozi wanaondoka na kurudisha kadi na kujiunga na CCM.

Bado CCM itabaki kuwa na viongozi safi na mfano mzuri tunauona, Rais Samia Suluhu Hassan ametimia katika kuiongoza Tanzania.

Ibrahim M. Bakari ni Mwandishi wa Habari
MAONI 0655/0754 264003

No comments:

Post a Comment