NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI DAVID KIHENZILE ATEMBELEA ENEO LINALOJENGWA BANDARI MPYA YA MBAMBABAY WILAYANI NYASA - KABATA

This is the special room for news where you need to settle with!


Breaking

Monday, 26 February 2024

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI DAVID KIHENZILE ATEMBELEA ENEO LINALOJENGWA BANDARI MPYA YA MBAMBABAY WILAYANI NYASA

 


SERIKALI imeanza ujenzi wa Bandari mpya na ya kisasa katika mji wa mdogo wa Mbambabay wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma,itakayokuwa makao makuu ya bandari zote za ziwa Nyasa ambayo itaunganisha nchi za Malawi na Msumbiji.

Meneja wa Bandari za Ziwa Nyasa Manga Gassayah alisema, ujenzi wa bandari hiyo ni mkakati wa serikali ya awamu ya sita kuimarisha ushoroba wa maendeleo wa Mtwara(Mtwara Development Corridor) ambayo ni njia fupi na rahisi ya kuhudumia mizigo ya nchi jirani za Malawi kutoka Bandari ya Mtwara.

Alisema,mradi huo utahusisha ujenzi wa gati lenye uwezo wa kuhudumia meli mbili,jengo la utawala la ghorofa tatu,jengo la abiria,barabara ya kuingia bandarini,majengo ya kuhifadhi shehena za mizigo na unatekelezwa na kampuni ya Xiamen Ongoing Group Co Ltd ya nchini China kwa gharama ya Sh.bilioni 81.

Alisema,wa bandari hiyo utakamilika kwa muda wa miezi 24(miaka 2) ambapo itaongeza uwezo wa kuhudumia shehena ya mizigo kwa bandari za ziwa Nyasa kutoka tani 110,000 za sasa hadi tani 550,000 kwa mwaka.

Gassayah alitaja manufaa ya mradi huo mara utakapokamilika ni pamoja na kuongeza uwezo wa bandari kupokea meli kubwa na kuhudumia mizigo kwa wingi na kuwa kiungo muhimu kwa sekta ya usafiri na usafirishaji kati ya bahari ya Hindi na ziwa Nyasa.

Kwa mujibu wa Gassayah,faida nyingine zitakazopatikana ni kukuza viwanda vidogo na vya kati na kuongeza mauzo na uagizaji wa bidhaa nje ya nchi,kuongeza pato la mwananchi na serikali,kuboresha usalama wa vyombo vya abiria na kutoa ajira na biashara wakati wa ujenzi na wakati wa uendeshaji.

Pia alisema,serikali kupitia mamlaka ya bandari nchini(TPA)imepanga kujenga gati ndogo kwenye baadhi ya bandari ikiwemo bandari ya Liuli katika wilaya ya Nyasa,Manda wilaya ya Ludewa mkoani Njombe,Matema na Kiwira katika wilaya ya Kyela mkoani Mbeya.

Alieleza kuwa,miradi hiyo imepangwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 na tayari serikali imeshatoa fedha jumla ya Sh.bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa miradi hiyo muhimu kwa uchumi wa nchi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa uchukuzi David Kihenzie,amemtaka mkandarasi anayejenga bandari hiyo kuhakikisha anazingatia ubora na muda uliopangwa ili wananchi waweze kuitumia katika shughuli zao za kujiletea maendeleo.

Alisema,mradi huo ni wa kihistoria na ni mapenzi na maono makubwa ya Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wa Nyasa na mkoa wa Ruvuma.

Kihenzie,amewataka wananchi hususani vijana kuchangamkia fursa ya ujenzi wa bandari hiyo kwa kufanya kazi zitakaowaingizia kipato,kuwa walinzi wa vifaa vitakavyoletwa kwa ajili ya ujenzi na kuhaidi kuwa mradi huo utakamilika kwa muda uliopangwa.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri alieleza kuwa,serikali ya awamu ya sita imeanza mchakato wa ujenzi wa Reli kutoka Mtwara-hadi Mbambabay mkoani Ruvuma ili kutoa fursa kwa wafanya biashara kusafirisha bidhaa na mizigo kwenda nchi jirani ya Msumbuji na Malawi kupitia ziwa Nyasa.

Mbunge wa jimbo la Nyasa Stella Manyanya, ameishukuru serikali kutoa fedha zitakazotumika kujenga bandari mpya katika mji pekee wa kitalii wa Mbambabay wilayani Nyasa ambayo itasaidia sana kuharakikisha kukua kwa Uchumi wa mtu mmoja mmoja,wilaya na mkoa wa Ruvuma.

Mkazi wa mji wa Mbambabay Ramadhan Mkilinya,ameiomba serikali kupitia mamlaka ya bandari nchini(TPA)kuhakikisha vijana wa Nyasa wanapewa kipaumbele katika ujenzi wa bandari hiyo badala ya kutafutwa watu kutoka nje ya Nyasa na mkoa wa Ruvuma.
Mbunge wa jimbo la Kyela mkoani Mbeya Ali Jumbe kulia na diwani wa kata ya Mbambabay wilayani Nyasa Ajali Hassan kushoto,wakimsaidia kusimama mbunge wa jimbo la Nyasa Mhandisi Stella Manyanya aliyeanguka kwa furaha kufuatia serikali kutoa kiasi cha Sh.bilioni 81 kwa ajili ya ujenzi wa bandari mpya katika mji wa Mbambabay wilayani humo.
Naibu waziri wa uchukuzi David Kihenzile wa pili kushoto,akikagua eneo linalojengwa bandari mpya na ya kisasa katika mji mdogo wa Mbambabay wilayani Nyasa,wa kwanza kushoto Mkuu wa wilaya ya Songea ambaye ni kaimu mkuu wa wilaya ya Nyasa Kapenjama Ndile,wa pili kulia Mbunge wa Jimbo la Nyasa Mhandisi Stella Manyanya na kulia diwani wa kata ya Mbambabay Ajali Hassan.
Naibu waziri wa uchukuzi David Kihenzile kulia,akimsikiliza meneja wa Bandari za ziwa Nyasa Manga Gassayah kushoto,kuhusiana na ujenzi wa mradi wa Bandari mpya inayojengwa katika mji mdogo wa Mbambabay wilayani Nyasa, ambapo serikali imetoa kiasi cha Sh.bilioni 81 ili kujenga bandari hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here