MADEREVA BODABODA MKOA WA TANGA WAPATA NEEMA YA MAFUNZO MAALUM YA UTOAJI HUDUMA YA KWANZA - KABATA

This is the special room for news where you need to settle with!

Tuesday, 26 March 2024

MADEREVA BODABODA MKOA WA TANGA WAPATA NEEMA YA MAFUNZO MAALUM YA UTOAJI HUDUMA YA KWANZA


Na Mwandishi Wetu,Tanga


MADEREVA bodaboda katika Jiji la Tanga wamepatiwa mafunzo ya huduma ya kwanza kwa lengo la kuwawezesha madereva hao kutoa msaada wa huduma ya kwanza inapotokea ajali

Mafunzo hayo ya huduma ya kwanza kwa madereva wa bodaboda inakwenda sambamba na elimu ya Usalama barabarani inayotolewa na Taasisi ya AMEND kwa kushirikiana na Ubalozi wa Uswisi ambao ndio wanaofadhili mradi wa utolewaji wa mafunzo hayo kwa madereva bodaboda.

Baadhi ya wadau ambao wanashirikishwa katika kutekeleza mradi huo wameeleza kwa kina kuhusu umuhimu wa mafunzo hayo kwa sababu yanakwenda kupunguza changamoto ya ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikisababisha vifo na ulemavu kwa madereva wengi wa bodaboda na watumiaji wengine wa usafiri huo.


Akieleza zaidi kuhusu mafunzo hayo CPL Hamisi anayetoka Kitengo cha Elimu Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga amesema wanaushukuru AMEND na Ubalozi wa Uswisi kwa kuona haja ya kutekeleza mradi huo kwani unakwenda kuongeza uelewa kwa madereva bodaboda kujiepusha na ajali pamoja na kutoa huduma ya kwanza inapotokea ajali.

Amesema ni muhimu kutolewa kwa huduma ya kwanza pale ajali inapotokea huku akisisitiza anapaswa kutoa hiyo ni mtu aliyepata elimu ya mafunzo ya jinsi ya kutoa huduma ya kwanza kwa mtu aliyepata ajali

"Mafunzo haya yatasaidia kuokoa maisha kwa mtu aliyepata ajali ya bodaboda,"amesema na kutoa mwito kwa baadhi ya bodaboda kuacha kujihusisha na vitendo vya uhalifu zinapotokea ajali na badala yake watumie elimu waliyoipata kuokoa maisha ya waliopatwa na ajali barabarani.

Kwa upande wake Ofisa Miradi kutoka AMEND Scolastica Mbilinyi ameeleza kwamba lengo la kutoa elimu ya huduma ya kwanza kwa bodaboda ni kusaidia kuokoa maisha ya watu pindi ajali zinapotokea.


Ameongeza wamekuwa na mradi huo wa kutoa mafunzo ya usalama barabarani kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Jeshi la Polisi na  Msalaba Mwekundu pamoja na wadau wote muhimu.

Aidha amesema AMEND miongoni mwa mambo wanayofanya ni pamoja na kutoa elimu ya usalama barabarani, ujenzi wa miundombinu ya barabara kwenye shule zilizopo maeneo hatarishi na kwa wakati huu huo wanatoa mafunzo ya huduma ya kwanza kwa madereva.

Pamoja na hayo amesema mpaka sasa  AMEND kwa ufadhili wa ubalozi wa Uswiswi wameshatoa elimu ya usalama barabarani katika mikoa ya Tanga na Dodoma na lengo ni kuwafikia madereva wa bodaboda 750.

Wakati huo huo Diana Kashmiry kutoka Kikosi kazi cha huduma ya kwanza- Shirika la Msalaba Mwekundu amesema elimu wanayoitoa inamuwezesha dereva bodaboda kufahamu changamoto aliyoipata mtu ajalini na jinsi ya kumsaidia kwa kumpa huduma ya kwanza

Aidha ametoa angalizo kutokana na mazingira hatarishi yanayokuwepo katika ajali, ni vema kwa mtu asiye na vifaa vya kutoa huduma ya kwanza asiye huduma hiyo ili kumuepusha na madhara yanayoweza kujitokeza yakiwemo ya magonjwa ya kuambukiza.

No comments:

Post a Comment