Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amewaasa wanafunzi wa kidato cha sita kuzidisha jitihada katika masomo yao ili kuweza kupata viongozi bora na weledi wa baadae watakaoliletea heshima Taifa letu.
Ameyasema hayo kwakati akikabidhi futari kwa wanafunzi wanaoishi dahalia mbali mbali kisiwani Pemba kwa lengo la kuwarahisishia upatikanaji wa ftari katika kipindi hichi cha mwezi mtukufu wa ramadhani.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dkt Hussen Mwinyi imeamua kuftari na wanafunzi wanaoishi katika madahalia kwa njia ya kuwapeleka futari kwenye maskuli yao jambo ambalo litawasaidia kukidhi mahitaji yao hasa katika mwezi mtukufu wa ramadhani.
Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar amesema kuwa mkakati wa Serikali ya Awamu ya Nane(8) ni kuhakikisha wanafunzi wanaoishi katika madahalia na sehemu nyengine wanasoma kwa utulivu ili Taifa liweze kupata wataalamu bora na viongozi wazuri wa baadae.
Mhe. Hemed amesema Serikali itaendelea kulipa kipao mbele suala la elimu kwa kuimarisha miundombinu ya elimu sambamba na kuboresha mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu kwa lengo la kuhakikisha Zanzibar inapata matokeo mazuri pamoja na kuzalisha wataalamu wenye uweledi katika kada mbali mbali.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed amesema Serikali inaangalia uwezekano wa kujenga dahali ya kisasa katika skuli ya Madungu Sekondari pamoja na kuijenga ya ghorofa skuli ya Sekondari ya Shamiaani ili kupunguza changamoto ya uhaba wa madarasa sambamba na kuweka mazingira bora ya kusomea na kujifundishia kwa wanafunzi skulini hapo.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. LELA MOHAMMED MUSSA amesema kuwa Serikali itaendelea kutoa misaada ya aina mbali mbali kwa wanafunzi kwa lengo la kuwaondolea changamoto wanazokumbana nazo wakiwa maskulini hasa wanafuzi waoishi katika madahalia.
Waziri LELA amemshukuru Makamu wa Pili wa Rais kwa msaada alioutoa kwa wanafunzi hao na kuahidi kuwa utatumika kama ulivyokusudiwa na kuwataka wanafunzi waliopatiwa msaada huo kuongeza bidii katika masomo yao na kupata matokeo mazuri katika mitihani yao ili Taifa liweze kupata wataalamu wazalendo watakaolipigania Tifa lao.
Akitoa shukrani kwaniaba ya wanafunzi wenzake mwanafunzi wa Kidato cha Tano (5) Skuli ya Sekondari ya Fidel Castro OMAR MOHAMMED SHAALI ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwawekea miundombinu mizuri ya kujifunzia sambamba na kuwapatia msaada huo jambo ambalo linapelekea kuondosha changamoto zinazowakabili wakiwa mashuleni hasa kwa wanafunzi wanaoishidahalia.
Aidha mwanafuzi OMAR amemuahidi Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar kuwa watahakikisha wanasoma kwa bidii na maarifa ili waweze kufaulu vizuri katika masomo yao na kutimiza malengo waliojiwekea. .
Miongoni mwa skuli zilizopatiwa ftari hio ni pamoja na Skuli ya madungu sekondari,Fidel Castro, Chuo Cha Kiislamu Kiuyu, Dkt. Amani Micheweni, Idrisa Abdulwakili Kizimbani, Utaani, Wete Sekondari pamoja na kituo cha kulelea yatima Micheweni Pemba.
Wakati huo huo Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar amekabidhi futari kwa wafanyakazi wa Kitengo cha Uratibu wa shuhuli za Chama cha Mapinduzi, Viongozi na watendaji wa Chama hicho katika Mikoa miwili ya kichama.
No comments:
Post a Comment