MIAKA TISA YA FAIDA YA MAENDELEO BANK Plc KIMAPATO NA UTENDAJI - KABATA

This is the special room for news where you need to settle with!


Breaking

Wednesday, 17 April 2024

MIAKA TISA YA FAIDA YA MAENDELEO BANK Plc KIMAPATO NA UTENDAJI

Mkurugenzi Mtendaji wa Maendeleo Bank Dr. Ibrahim Mwangalaba (katikati) akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 17, 2024 katika Ofisi za Makao Makuu ya Bank hiyo Jijini Dar es Salaam.

*Yajipanga kufungua matawi mikoani mwaka huu na kuwa Benki ya kitaifa, kuendelea kurudisha kwa jamii

MAFANIKIO Makubwa yameendelea kuonekana kwa benki ya ‘Maendeleo Bank Plc’ ambapo kwa mwaka 2023 matokeo ya kifedha yameonesha kukua kwa faida kwa asilimia 66 baada ya kodi na kufanya faida baada ya kodi kuongezeka hadi shilingi Bilioni 2.3 kutoka shilingi Bilioni 1.4 mwaka 2022 kutokana na uimarishwaji wa njia za uchumi unaofanywa na Serikali ya awamu ya sita na ushirikiano kutoka kwa wafanyakazi, bodi ya wakurugenzi, wateja na wadau mbalimbali.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam wakati akitangaza matokeo ya kifedha kwa mwaka 2023, Mkurugenzi Mtendaji wa Maendeleo Bank Dr. Ibrahim Mwangalaba amesema, Ukuaji huo wa kuvutia wa faida umechangiwa zaidi na mikakati mizuri ambayo benki ilijiwekea kwa mwaka 2023 pamoja na usimamizi bora wa watendaji na wafanyakazi wa benki hiyo kwa kushirikiana na wateja na wadau mbalimbali.

Ameeleza kuwa; Baadhi ya vichocheo vya mafanikio ya Benki hiyo ya kwanza nchini kuorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE,) na kuweka historia ya kuwa benki yenye faida kwa miaka tisa mfululizo tangu mwaka wa pili wa kuanzishwa kwake ni pamoja na kuimarika kwa ubora wa mikopo kutoka mikopo chechefu ya asilimia 5.2 mwaka 2022 hadi kufikia asilimia 4.95 mwaka 2023 kulikosababishwa na kuimarika kwa hali uchumi na kufanya wateja wao kulipa mikopo kwa wakati.

Aidha amesema, kumekuwa na ongezeko Amana za wateja kwa asilimia 15 kutoka shilingi Bilioni 78.0 mwaka 2022 hadi kufikia shilingi Bilioni 90.0 kwa mwaka 2023.

Pia mikopo ya wateja imeongezeka kwa asilimia 21 kutoka shilingi za kitanzania Bilioni 61.0 hadi shilingi za kitanzania Bilioni 74.0 kwa mwaka 2023….ukuaji huu utaendelea kwa kuwa Benki imejipanga kutoa huduma kwa ufanisi zaidi kwa wateja wake.” Ameeleza.

Dr. Mwangalaba amesema mali za benki zimeongezeka kwa asilimia 17 kutoka shilingi za kitanzania Bilioni 107.0 kwa mwaka 2022 hadi kufikia shilingi Bilioni 125.0 kwa mwaka 2023 huku mtaji wa benki ukiimarika kwa asilimia 12 kutoka shilingi za kitanzania Bilioni 17 kwa mwaka 2022 hadi shilingi Bilioni 19 kwa mwaka 2023.

Kuhusiana na mtaji na kuwafikia wananchi katika mikoa nchini kote Dr. Mwangalaba amesema kuwa, Benki hiyo imefikisha mtaji wa Shilingi Bilioni 19 ambao unakidhi benki kufanya kazi nchini kote na tayari wameanza mazungumzo na wasimamizi wao ambao ni Benki Kuu ya Tanzania (BOT,) ili wapate kibali cha kufungua matawi mikoani kuanzia mwaka huu huku wakiendelea kufuatilia mwenendo wa kiuchumi wa dunia pamoja na utekekezaji wa majukumu yao kwa kuhakikisha mafanikio ya benki yanakuwa endelevu.

Amefafanua kuwa, Utendaji kazi bora wa mwaka 2023 umejenga msingi thabiti wa utendaji kwa mwaka 2024 ambapo wamejipanga kutanua huduma zaidi kwa kufungua angalau tawi moja na mawakala wapya zaidi ya 500 kutokana na mafanikio makubwa ya mwaka 2023 ambapo walifunga na mawakala 1600 katika mikoa 11 ambao walikusanya zaidi ya Bilioni 5 kila mwezi kama amana kila mwezi kupitia wateja.

“Benki inawekeza sana katika teknolojia na kwa mwaka 2024 tumejipanga kuanzisha huduma mpya za kidigitali ikiwemo Benki mtandao yaani Internet Banking, mfumo wa ukusanyaji malipo ikiwemo ada za shule (PCS,) na mikopo kwa njia ya simu ambayo itawezesha benki kuongeza faida kwa fedha za wanahisa kwa mwaka 2024 na kuboresha njia mbadala za upatikanaji wa huduma za wateja….,,,, na kwa kuonesha juhudi za kuboresha na kusogeza huduma kwa wateja mwaka huu 2024 tumefungua tawi jipya Mbagala hapa Dar es Salaam likiwa tawi la tano huku tukiwa na lengo la kusogeza huduma zetu kwa wakazi wa Mbagala na maeneo jirani.” Amefafanua.

Aidha ameeleza kuwa Benki hiyo imeendelea kurudisha kwa jamii kupitia Marathon na kulenga makundi mbalimbali wakiwemo watoto waliozaliwa kabla ya wakati Pamoja na watoto wenye utindio wa ubongo .

Mwaka jana kupitia Marathon tulikusanya washiriki 5000 na tulisaidia vituo viwili vya Mtoni kinachohusika na watoto wenye mtindio wa ubongo pamoja na kituo cha watoto waliozaliwa kabla ya wakati KCMC…. Na mwaka huu Marathon msimu wa pili itafanyika tarehe 7/9 mwaka huu na tumelenga kukusanya shilingi milioni 200 na kusaidia makundi ya watoto wenye usonji, waliozaliwa kabla ya wakati, kutembelea na kusaidia shule na hospitali pamoja na watoto wenye mtindio wa ubongo na nitoe wito kwa watanzania kuangalia na kusaidia makundi hayo kwa kuwa uhitaji ni mkubwa.

Maendeleo Bank Plc imeendelea kukua huku idadi ya wateja ikiongezeka kila mwaka hadi kufikia sabini na tano elfu mwaka 2023 huku malengo yakiwa ni kufikia zaidi ya wateja elfu tisini mwaka huu, Na mpango wa kuwafikia wateja katika mikoa yote nchini unatarajiwa kuwafikia maelfu ya wateja kutokana na ufanisi katika utoaji wa huduma za kibenki.
Mkurugenzi Mtendaji wa Maendeleo Bank Dr. Ibrahim Mwangalaba (katikati) akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 17, 2024 katika Ofisi za Makao Makuu ya Bank hiyo Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Maendeleo Bank Dr. Ibrahim Mwangalaba (katikati)akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 17, 2024 katika Ofisi za Makao Makuu ya Bank hiyo Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Maendeleo Bank Dr. Ibrahim Mwangalaba akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 17, 2024 katika Ofisi za Makao Makuu ya Bank hiyo Jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here