Benki ya Biashara DCB kuendelea kuboresha Maisha ya Watanzania - KABATA

This is the special room for news where you need to settle with!

Saturday, 14 September 2024

Benki ya Biashara DCB kuendelea kuboresha Maisha ya Watanzania

Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Biashara ya DCB, Bi. Zawadia Nanyaro (wa nne kulia) akishikana mikono na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya DCB, Bw. Sabasaba Moshingi baada ya kumaliza Mkutano Mkuu wa 22 wa Mwaka wa Wanahisa wa benki hiyo uliofanyika kwa njia ya mtandao jijini Dar es Salaam leo.

*Yajivunia kutoa Mikopo ya zaidi ya Shs Bilioni 740 Tokea Ilipoanzishwa

BENKI YA BIASHARA YA DCB imesema itaendelea kusimamia misingi ya kuanzishwa kwake ambayo ni kusaidia miradi endelevu ya kupunguza umasikini, kuendeleza jamii na kutoa huduma bora zinazokidhi mahitaji halisi ya kila siku ya wateja wao.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo wakati wa Mkutano Mkuu wa 22 wa Mwaka wa Wanahisa wa benki ya Biashara DCB, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Sabasaba Moshingi alisema, tokea kuanzishwa kwa DCB, takriban miaka 22 iliyopita benki hiyo imeendelea kukua mwaka hadi mwaka ikiendelea kutoa masuluhisho tofauti kwa wateja wake wa kada zote na hivyo kudhihirisha ukweli kuwa DCB ni ‘Mkombozi wa Kweli’ wa maisha ya watanzania.

Ikiwa ni Mkutano wake Mkuu wa kwanza tokea ajiunge na DCB, Bw. Moshingi akileta uzoefu wake wa miongo kadhaa katika tasnia za kibenki anasema benki inaendelea kujivunia kuwa kiongozi katika kuleta ufumbuzi wa tatizo la mitaji ya kibiashara kwa wajasiriamali wadogo wadogo kwa kuingiza sokoni bidhaa zenye ubunifu na kwa kutumia teknolojia za kisasa zinazoendana na mageuzi ya sayansi na teknolojia yanayoendelea duniani kote.

Benki ya Biashara DCB imekuwa mstari wa mbele katika kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo wanaopata changamoto za kupata huduma hizo katika baadhi ya taasisi za kifedha kutokana na kutokidhi masharti waliyoweka, lakini pia tumeendelea kufanya vizuri katika mikopo ya watu binafsi na vikundi vya wajasiriamali huku tukiendelea kuboresha mikopo hiyo ili iendane na mahitaji yao, kwa kipindi cha miaka 22 tokea DCB imeanzishwa, tunajivunia kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shs bilioni 741 iliyowanufaisha zaidi ya watanzania 420,000”, alisema Bwana Moshingi.

Katika kipindi hiki cha mwaka mmoja tokea mkurugenzi mtendaji huyu mpya aingie madarakani, Benki ya biashara DCB imepiga hatua kadhaa za maendeleo ikiwa ni pamoja uimarishaji wa huduma za kibenki kwa njia za kidigitali pamoja na kuanzisha mikopo yenye lengo la kuinua maisha ya makundi maalumu hususan wanawake wajasiriamali.

Tumeanzisha huduma maalumu iitwayo ‘Tausi’ ikiwalenga wanawake yenye lengo la kuinua vipato vya wanawake wajasiriamali wadogo, tukianzia na mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Dodoma kwa kutoa mikopo ya kuendeleza biashara zao, kuwapa elimu ya kifedha pamoja na mbinu za uendeshaji wa biashara".

Sifa za kuwa mwanachama lazima uwe mkazi wa eneo husika, uwe na biashara, tukitumia mfumo wa kikundi kinachoanzia watu 15 hadi 30 wenye umri kuanzia miaka 18 mpaka 65, huku mikopo ikianzia 300,000 hadi milioni 1 kutegemea na aina ya biashara ya mteja na marejesho ni kati ya miezi mitano hadi 10”.

Bwana Moshingi anaongeza kuwa mbali na mikopo ya wanawake, DCB pia imeendelea kufanya vizuri katika mikopo mingine ya vikundi, mikopo ya nyumba, mikopo ya wafanyakazi hususan walimu, mikopo ya guta, pikipiki na bajaji na mingineyo.

Kwa upande wa huduma za jamii, benki yetu imekuwa mstari wa mbele pia katika kuisaidia serikali yetu katika kuwaletea watu wake maendelea hususan katika nyanja za elimu na afya kupitia miradi yetu mbalimbali inayoendelea, bila kusahau akaunti maalumu ya elimu ya DCB Skonga yenye lengo la kuboresha elimu ya watoto wetu".

Mwaka jana tulikabidhi madawati katika shule tano za Manispaa zote za jiji la Dar es Salaam na kauli mbiu isemayo ‘Elimu Mpango Mzima na Mama Samia’ tukikusudia kukabidhi madawati 1000 katika shule mbalimbali nchini kati ya mwaka 2023 na 2025, mradi huu unaendelea vizuri na wiki ijayo tutakabidhi baadhi ya madawati haya katika Shule ya Msingi ya Msisiri B, Kinondoni, jijini Dar es Salaam”, alisema.

Aidha anaongeza, “Ukiacha hayo benki yetu imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuuunga mkono serikali yetu katika miradi yake ya kimkakati kama tulivyofanya hivi karibuni tulipodhamini walimu 1000 kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwenda kufanya utalii katika mbuga za mikumi kwa kutumia treni ya SGR, kwa kufanya hivyo tunasaidia kuitangaza treni hii pamoja na utalii wa nchi yetu ndani na nje ya Tanzania”.

Pamoja na hayo mkurugenzi huyo anasema DCB imeendelea pia kufanya vizuri katika huduma na akaunti nyingine zikiwemo; Wahi Akaunti, akaunti ya mshahara, mikopo ya nusu mshahara, akaunti za wastaafu, huduma za malipo ya serikali (GePG) pamoja na malipo mengine kwa watoa huduma mbalimbali yanayofanyika katika matawi ya benkina kwa njia za mtandao.

Kaimu Mkurugenzi wa Fedha DCB, Bwana Siriaki Surumbu alisema benki imeendelea kukuza mapato ikijikita katika shughuli za utoaji mikopo yenye ubora hasa kwa vikundi maalum vya wanawake na wajasiliamali mbalimbali. Maboresho katika vitengo mbalimbali vya huduma hususan huduma za kidigitali ambazo zitaongeza ufanisi katika utoaji huduma na kuongeza mapato ya benki.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya DCB, Bi. Zawadia Nanyaro alisema benki imekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika ajenda yake ya kuona huduma za kibenki zinawafikia watanzania wote wakifanya huduma zao za kibenki kwa njia za kidigitali kuwa bora zaidi na zenye gharama nafuu.

Bi Nanyaro alisema kwa sasa mkakati wa kuhahakisha huduma zake zinapatikana nchi nzima unaendelea vizuri ukiwezeshwa na uimarishaji wa huduma hizo, kusambaa kwa mtandao wa mawakala zaidi ya 1000 nchini kote pamoja na vituo vidogo 1500 vya kutolea huduma katika maeneo ya kimkakati.

Nipende kutoa shukurani kwa serikali yetu chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira yanayosaidia sekta ya fedha kufanya biashara katika mazingira bora na wezeshi, lakini pia kwa kuona umuhimu wa kushirikisha sekta binafasi katika miradi ya kimkakati inayoendelea kwa mafanikio katika sehemu mbalimbali nchini".

Nipende pia kuwahakikishia wanahisa wetu, wateja wetu na wadau wetu kuwa benki yenu ipo katika mikono salama na inaendelea vizuri chini ya uongozi wa Bwana Moshingi, menejimenti, wafanyakazi wote pamoja na Bodi ya wakurugenzi".

Tunachohitaji tu ni ushirikiano kutoka kwenu wanahisa wote, wadau pamoja na wateja wetu ili benki yetu izidi kufanya vizuri sokoni na kutekeleza mikakati yote ya maendeleo tuliyojiwekea".

Natoa wito kwa watanzania wote kujiunga na benki yetu na kufaidika na fursa mbalimbali za huduma bora za kibenki tunazozitoa, DCB ni Mkombozi wa Kweli kwa watanzania wote, Wajasiriamali wadogo na wa kati, wanawake na vijana, DCB ni Mkombozi wa Kweli kwa wafanyabiashara wa kada zote”, anamaliza Bi Nanyaro.
Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Biashara ya DCB, Bi. Zawadia Nanyaro, akizungumza na wanahisa wakati wa Mkutano Mkuu wa 22 wa mwaka wa Wanahisa wa benki hiyo uliofanyika kwa jijini Dar es Salaam leo. Bi Zawadia alisema DCB Itaendelea kusimamia misingi ya kuanzishwa kwake ambayo ni kusaidia miradi endelevu ya kupunguza umasikini, kuendeleza jamii na kutoa huduma bora zinazokidhi mahitaji halisi ya kila siku ya wateja wao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya DCB, Bw. Sabasaba Moshingi , akizungumza na wanahisa wakati wa Mkutano Mkuu wa 22 wa mwaka wa Wanahisa wa benki hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam leo. Bwana Moshingi aliwaambia wanahisa kuwa DCB chini ya uongozi wake, kwa kushirikiana na Bodi pamoja na wafanyakazi wote wamejizatiti kuandika upya historia ya benki hiyo na hii ikianza kuonekana baada ya DCB kufanya vizuri katika robo ya kwanza na ya pili mwaka huu.
Mwanasheria Mshauri wa Benki ya Biashara ya DCB, Bw. Alex Mgongolwa, akizungumza na wanahisa wakati wa Mkutano Mkuu wa 22 wa mwaka wa Wanahisa wa benki uliofanyika jijini Dar es Salaam leo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bodi ya Ukaguzi na Usimamizi wa Benki ya Biashara ya DCB, Prof. Tadeo Satta, akizungumza na wanahisa wakati wa Mkutano Mkuu wa 22 wa mwaka wa Wanahisa wa benki hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam leo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya DCB, Bw. Sabasaba Moshingi (kulia) akizungumza na baadhi ya wawakilishi wa wanahisa wa benki hiyo wakati wa Mkutano Mkuu wa 22 wa mwaka wa Wanahisa wa benki hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam leo. Kutoka kushoto ni Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Bw. Selemani Kateti, Mwakilishi kutoka UTT AMIS, Bw. Medson Enock na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni, Bw. Rajab Gondomo.

Kuhusu DCB

Benki ya Biashara ya DCB ilianzishwa mwaka 2002 na mwaka unaofuata kupewa leseni ya kujiendesha kama benki ya kijamii, ikijulikana kama Benki ya Watu wa Dar es Salaam ‘Dar es Salaam Community Bank’ ambayo wanahisa wake waanzilishi wakiwa ni Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam pamoja na Manispaa zake za Ilala, Kinondoni na Temeke. Wanahisa wengine ni Mifuko ya NHIF na UTT AMIS pamoja na wananchi wa kawaida.

Kuanzishwa kwa DCB kulitokana na maono ya Rais mstaafu wa awamu za tatu, Hayati Benjamin William Mkapa kutoka na kilio cha wananchi wenye kipato cha chini na cha kati kukosa mikopo ya mitaji katika benki za kibiashara kutokana na kutokidhi vigezo vilivyowekwa.

Katika miaka hii 22 tokea kuanzishwa kwa DCB, benki imepitia hatua mbalimbali; ilikuwa benki ya kwanza kuorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es salaam (DSE) mnamo mwaka 2008, ambapo Februari 2012 ilifanikiwa kuhuisha leseni yake kutoka benki ya kijamii na kuwa benki kamili ya kibiashara na kubadilisha jina kutoka Benki ya Watu wa Dar es Salaam na kuwa Benki ya Biashara ya DCB.

Benki ya DCB ina mtandao wa matawi 9 ya kibenki ndani na nje ya Dar es Salaam ikiwa na mtandao wa mawakala 1000 na vituo vya kutolea huduma 1500 sehemu mbalimbali nchini. Ina zaidi ya mashine 280 za ATM zilizounganishwa na Umoja Switch, lakini pia inatumia Kadi za Visa zinazoweza kutumika katika mashine zinazosapoti kadi hizo ndani na nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment