BENKI YA DCB KUONGEZA MTAJI WA SH BILIONI 10.7 - KABATA

This is the special room for news where you need to settle with!


Breaking

Monday, 11 November 2024

BENKI YA DCB KUONGEZA MTAJI WA SH BILIONI 10.7

Mkurugenzi wa Usimamizi wa Masoko na Uchunguzi wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bw. Exaut Julius (katikati), akikata utepe, kuashiria uzinduzi rasmi wa zoezi la uuzaji wa Hisa za Upendeleo za Benki ya Biashara ya DCB, jijini Dar es Salaam leo. Wa nne kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya DCB, Bi. Zawadia Nanyaro na wa tatu kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Sabasaba Moshingi pamoja na wawakilishi wa taasisi nyingine waliohudhuria.

*Ni kwa kupitia uuzaji wa Hisa za Upendeleo

BENKI ya Biashara ya DCB, imezindua zoezi ya uuzaji wa Hisa za Upendeleo, ikitarajia kupata zaidi ya sh bilioni 10.7 ili kuongeza kiasi cha mtaji wake unaofikia sh bilioni 15 kwa sasa, ili pamoja na mambo mengine kukidhi vigezo vilivyowekwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), pamoja na kuwaletea wanahisa wake na watanzania kwa ujumla tija za kiuchumi.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi rasmi wa uuzaji wa hisa hizo jijini Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa Bodi ya DCB, Bi. Zawadia Nanyaro alisema uamuzi huo unaenda sambamba na mikakati yao ya maendeleo ya miaka mitano katika kuongeza mtaji wake kutoka ulipo sasa hadi kufikia sh bilioni 61.

Bodi ya Wakurugenzi ya DCB iliidhinisha mpango mkakati wa miaka mitano ukijikita kwenye mambo makuu Matano; Kwanza kukuza mtaji wa benki kutoka shs bilioni 15 (2024) hadi kufikia shs bilioni 61 ifikapo mwaka 2028, pili ukusanyaji wa amana nafuu za benki kupitia wanahisa wakuu na wateja wetu, tatu kuongeza wigo wa mikopo bora itakayotolewa kwa ufanisi na umahiri, nne utaoaji wa mikopo kwa wateja wadogo wadogo na wa kati ili kuendelea kutimiza lengo la kuanzishwa kwa benki yetu na tano, kuboresha njia za utoaji huduma na kuongeza bidhaa zinazotolewa kwa njia za kijiditali."

Tukio la leo linaenda kuandika historia ya benki na kuanza kutimiza mkakati wa kwanza wa kuongeza mtaji wa benki, hivi sasa, mtaji wa benki uko kwenye kima cha chini kilichowekwa na Benki Kuu ya Tanzania, na ili kuweza kusimama imara kama benki, ongezeko la mtaji ni muhimu sana, benki inadhamiria kufanya biashara kubwa ambapo ili kufanikisha lengo hili, kuna ulazima wa kuongeza mtaji”, alisema Bi. Zawadia.

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa ili kuweza kuhakikisha mtaji wa benki unaendelea kukua mwaka hadi mwaka baada ya zoezi hili na pia kutumiza malengo ya benki, Bodi ya Wakurugenzi iliona ni muhimu kufanya mabadiliko machache ya kiutawala katika menejimenti ya benki yetu, na kumteu Ndugu Sabasaba Moshingi kama Mkurugenzi Mtendaji wa benki mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 20 katika tansia ya benki, huku mabadiliko mengine yakifanyika katika idara ya biashara, mikopo na uendeshaji na teknolojia, idara zote hizi kwa ujumla ni nguzo muhimu katika biashara ya benki.

Alisema uuzaji wa Hisa za upendelo unatarajia kuwaletea wanahisa na watanzania kwa ujumla tija za kiuchumi, baada ya kuongeza mtaji wa benki ambapo unalenga kukuza biashara na kuwapatia wafanyabiashara wadogo wadogo na wa kati mitaji ya kukuza biashara zao na upande mwingine umiliki wa hisa za benki ya DCB unaunga mkono juhudi zinazoendelea za serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi shupavu wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuwaletea watu wake maendeleo.

Bodi ya DCB pamoja na Menejimenti ya benki ilipendekeza na kuidhinisha uuzaji wa Hisa za Upendeleo 97,646,913 zenye thamani ya shs 10,741,160,430 kwa bei ya punguzo ya shs 110 kwa kila hisa moja, kinyume na shs 160 iliyopo sokoni, ni matumaini yetu zoezi hii litapata muitikio mkubwa kutoka kwa wanahisa wetu, ambao wana imani na benki hii, bodi na menejimenti yake kwa ujumla."

Benki imerahisisha ununuzi wa hisa kwa kuruhusu ununuzi kwa njia za kidigitali ili kuongeza wigo wa ushiriki wa wanahisa, natoa rai kwa wanahisa kuchangamkia fursa hii ya kununua hisa kwa njia za kidigitali, au kupitia mawakala wa Soko la Hisa la Dar es Salaam au kwa kufika kwenye matawi yetu ya benki”, aliongeza Bi. Nanyaro.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Masoko na Uchunguzi wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bw. Exaut Julius aliipongeza Benki ya DCB kwa uamuzi huo uliofanyika kwa weledi na ufanisi mkubwa na kupata idhini kutoka CMSA.

Akimwakilisha Ofisa Mtendaji Mkuu wa mamlaka hiyo, CPA Nicodemus Mkama, Bwana Julius alisema, serikali kupitia Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ina jukumu la kuendeleza na kusimamia masoko ya mitaji hapa nchini, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba shughuli katika masoko ya mitaji zinafanyika kwa kufuata sheria, taratibu na miongozo ili kuleta uwazi na haki kwa washiriki wote.

Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana itaendelea kujenga mazingira wezeshi na shirikishi ili kuwezesha taasisi katika sekta ya umma na binafsi kutumia masoko ya mitaji kupata fedha za kutekeleza miradi na shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuuza hisa kwa umma, hatifungani za miundombinu, hatifungani rafiki za mazingira, hatifungani za bluu, hatifungani za jamii na hatifungani za taasisi za serikali”, alisema Bw. Julius.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Sabasaba Moshingi alisema, yeye pamoja na menejimenti yote ya DCB wamejipanga kuhakikisha hadi kufikia Mwaka 2028 wanaandika upya historia ya benki hiyo sambamba na mkakati wa miaka mitano wa maendeleo ya benki hiyo wa kuhakikisha benki inaendelea kukua na kupata faida.

Alisema kwa kuthibitisha hayo, benki hiyo imeweza kutengeneza faida katika robo ya pili na ya tatu huku ikiendelea kutoa huduma za kibenki bila kusahau jukumu la kuanzishwa kwake takribani miaka 22 iliyopita ikiweka mkazo mkubwa katika huduma zake za kidigitali ili kuhakikisha watanzania wengi wanafikiwa na huduma za kibenki.

Tumejipanga kuhakikisha benki yetu inaendeleza maono ya kuanzishwa kwake ambayo ni kusaidia miradi ya kupunguza umasikini kwa kutoa mikopo ya mitaji kwa wajasiriamali wadogo na wa kati waliokosa huduma hizi kutokana na kutokidhi vigezo vya benki ya kibiashara za wakati ule."

Uuzaji huu wa Hisa za Upendeleo ambao sasa benki yetu inafanya kwa mara ya nne kwa vipindi tofauti utasaidia kuongeza uwezo wa benki yetu katika kuwahudumia wateja wetu na ni imani yetu pia kuanzia mwakani wanahisa wetu wataweza kuanza kupata gawio hivyo tunaomba waendelee kutuunga mkono”, alisema.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Masoko na Uchunguzi wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bw. Exaut Julius (katikati), Mwenyekiti wa Bodi ya DCB, Bi. Zawadia Nanyaro (wa nne kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Sabasaba Moshingi (wa tatu kulia), Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Bw. Peter Nalitolela, wakionesha kitabu chenye taarifa muhimu kuhusu Hisa wakati wa uzinduzi rasmi wa zoezi la uuzaji wa Hisa za Upendeleo za Benki ya DCB, jijini Dar es Salaam leo. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria wa DCB, Bi. Regina Mduma, pamoja na wawakilishi kutoka taasisi nyingine waliohudhuria hafla hiyo.
Mkurugenzi wa Biashara wa Benki ya DCB, Bw. Ramadhan Mganga, akizungumza katika hafla hiyo, jijini Dar es Salaam leo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya DCB, Bi. Zawadia Nanyaro, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Hisa za Upendeleo za benki hiyo, jijini Dar es Salaam leo. Alisema Bodi na Menejimenti ya benki ilipendekeza na kuidhinisha uuzaji wa Hisa za Upendeleo 97,646,913 zenye thamani ya shs 10,741,160,430 kwa bei ya punguzo ya shs 110 kwa kila hisa moja. Huku bei ya soko ikiwa shs 160.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here