
WAKAZI
wa mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, kwa zaidi
ya wiki moja wamelalamikia kutopata huduma ya maji ya kunywa, baada ya
malori yanayouza maji hayo kutoka mji mdogo wa Boma ng'ombe wilayani Hai
mkoani Kilimanjaro kudaiwa kuzuiwa.
Kwa
zaidi ya miaka 20 wakazi wa mji mdogo wa Mirerani, wanatumia maji ya
kunywa yanayouzwa na malori kutoka mji mdogo wa Boma ng'ombe.
Hivi
sasa, baadhi ya wakazi wengine wa mji huo wanatumia maji ya visima
vifupi na virefu na maji ya mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira
jiji la Arusha (AUWSA) Mirerani, kwa ajili ya matumizi mengine ikiwemo
kunywa.
Baadhi
ya wakazi wa mji mdogo wa Mirerani, wakizungumza juu ya changamoto hiyo
wameiomba serikali kuingilia kati suala hilo kwani wanatumia gharama
kubwa kupata maji ya kunywa
Mmoja
kati ya wakazi hao, Andrew John amesema kwa zaidi ya miaka 20 walikuwa
wanatumia maji ya kunywa yanayotoka Hai ila wanasikitishwa hivi sasa
kupata zuio hilo.
"Tulikuwa
tunategemea malori ya kina 'Rumba Kali' kwa ajili ya kununua maji ya
kunywa ila wanadai wamezuiwa kuleta maji Mirerani bila sababu ya
msingi," amesema.
Amesema
maji ya Hai yamewasaidia kwa muda mrefu kwani ya kisima na mengine
hayakati kiu yana chumvi na maji ya chupa ni gharama kutumia na familia.
"Hivi
sasa kuna baadhi ya malori machache yamefanikiwa kuleta maji Mirerani
ila ndoo moja ya lita 20 ya maji ya kunywa tunauziwa Sh2,000 badala ya
Sh1,000 kama awali," amesema.
Mmoja
kati ya wauza maji wa eneo hilo, Abdi Soka amesema watu wengi
wameathirika kwa ukosefu wa maji kutokana na zuio la mkuu wa wilaya ya
Hai, Hassan Bomboko.
"Wanaoleta
maji na kutuuzia kupitia malori kutoka mji mdogo wa Boma ng'ombe
wamedai kuwa DC wa Hai, Hassan Bomboko amezua malori hayo yasilete maji
mji mdogo wa Mirerani," amesema Soka.
Meneja
wa mamlaka ya maji na usafi wa mazingira jiji la Arusha (AUWSA)
Mirerani, Fidelis Shayo ameeleza kwamba hata yeye amesikia changamoto ya
maji hayo kutopatikana.
Shayo
amesema AUWSA aihusiki kuzuia huduma ya maji kutoka maeneo mengine
japokuwa mradi wao wa maji wa Mirerani unaendelea kutoa huduma kwa
uhakika maeneo hayo yakiwa safi na salama.
"Maji
ya AUWSA Mirerani ni safi na salama kwani yametibiwa kwa dawa,
tunaendelea kuwasihi watu wa eneo hilo waendelee kutumia hata kwa kunywa
ndiyo sababu serikali imetenga Sh4.3 bilioni kwa ajili ya mradi wa maji
Mirerani," amesema Shayo.
Hata hivyo, mkuu wa wilaya ya Hai, Hassan Bomboko alipoulizwa kwa njia ya simu juu ya suala hilo alikataa kulizungumzia.
"Kama upo huko Mirerani waulize viongozi wa huko juu ya suala hilo," amejibu DC Bomboko na kukata simu.
Kwa
upande wake, ofisi mtendaji wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani (TEO)
Isack Mgaya amesema kwa sababu suala hilo lipo nje ya wilaya ya
Simanjiro wameshindwa kuingilia kati.
"Tulipata
taarifa kuwa uongozi wa Hai ulizuia maji hayo kwa madai kuwa ni
machache ila tumefikisha suala hilo kwa mkuu wa wilaya ya Simanjiro
Fakii Lulandala ili azungumze na uongozi wa Hai," amesema Mgaya.
No comments:
Post a Comment