Mam ia ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka Wilaya za Temeke na Kigamboni jijini Dar es Salaam wamesema wana imani kubwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Asha-Rose Migiro, wakieleza kuwa uteuzi wake umeipa CCM mwelekeo mpya wa uongozi na mshikamano.
Wanachama hao, ambao ni mabalozi wa mashina, wamesema Dk. Migiro ameandika historia kwa kuwa Katibu Mkuu wa kwanza mwanamke ndani ya CCM, huku uzoefu na uwezo wake wa kisiasa ukiwapa imani kuwa chama kiko mikononi mwa kiongozi sahihi.
Wakizungumza leo Januari 7, 2026 katika ukumbi wa TPA – Sabasaba jijini Dar es Salaam, walipofika kushiriki kikao kazi kilichoandaliwa na Katibu Mkuu huyo, mabalozi hao wamesema wanaamini kikao hicho kitawapa mwelekeo na maneno ya faraja yanayojenga umoja na ari ya kuendelea kukitumikia chama.
Balozi wa Shina kutoka Kibada, wilayani Kigamboni, Mwakibona Jumanne, amesema wanamshukuru Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kumuamini na kumteua Dk. Migiro kuwa Katibu Mkuu wa chama.
Amesema ujio wa Katibu Mkuu huyo Dar es Salaam ni ishara ya kuimarisha mawasiliano kati ya uongozi wa juu wa chama na wanachama wa chini, akieleza kuwa wana imani kuwa atawapa ujumbe unaobeba faraja na mwelekeo kwa wana CCM na Watanzania kwa ujumla.
Aidha, Mwakibona ameipongeza Serikali kwa kudumisha amani na utulivu nchini, akisema hali hiyo imewezesha wananchi kuendelea na shughuli za maendeleo bila hofu.
“Kwa utulivu na amani ndipo maendeleo ya kijamii na kiuchumi yanaweza kupatikana. Tuna imani Serikali itaendelea kusimamia misingi hiyo ili Tanzania iendelee kusonga mbele,” amesema.
Kwa upande wake, Asia Sadick, Katibu Mwenezi wa CCM kutoka Kijiji cha Wavuvi, Kata ya Mtoni, amesema uteuzi wa Dk. Migiro umeongeza imani ya wanachama kwa uongozi wa chama, akieleza kuwa hawana shaka na uwezo wake wa kiuongozi.
Amesema wanatarajia kikao kazi hicho kitoe ujumbe unaojenga imani, mshikamano na matumaini mapya kwa Taifa la Tanzania.
Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Asha-Rose Migiro, ameanza rasmi ziara yake katika Mkoa wa Dar es Salaam ambapo leo Januari 7, 2026, anakutana na viongozi mbalimbali wa chama, wakiwemo mabalozi wa mashina wa Wilaya za Temeke na Kigamboni. Kikao hicho kinafanyika katika ukumbi wa TPA uliopo katika viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment