DAR ES SALAAM – Shirikisho la Kimataifa la Kriketi (International Cricket Council - ICC) limesema Tanzania ina nafasi ya kuwa miongoni mwa mataifa yatakayoweza kuandaa mashindano makubwa ya kriketi duniani siku zijazo, kufuatia uwekezaji unaoendelea katika miundombinu ya kisasa ya mchezo huo na maendeleo ya vijana.
Kauli hiyo imetolewa wakati wa uzinduzi wa Uwanja wa Kisasa wa Chama cha Kriketi Tanzania (TCA Cricket Arena), uliojengwa katika viwanja vya michezo vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Uwanja huo utatumika kama kituo cha taifa cha kukuza vipaji na kuandaa timu za taifa za wanaume, wanawake na vijana wenye umri wa chini ya miaka 19.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi, Mwenyekiti wa ICC, Jay Shah, alisema Tanzania imeonyesha dhamira kubwa ya kuendeleza mchezo wa kriketi kupitia uwekezaji katika miundombinu na programu za maendeleo ya vijana, hatua ambayo imeifanya kuwa miongoni mwa mataifa yanayokua kwa kasi katika mchezo huo barani Afrika.
Alisema iwapo kasi hiyo ya maendeleo itaendelea, Tanzania inaweza kuwa miongoni mwa nchi zitakazopewa fursa ya kuandaa mashindano makubwa ya kimataifa, ikiwemo Kombe la Dunia la Kriketi, katika miaka ijayo.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Chama cha Kriketi Tanzania (Tanzania Cricket Association - TCA), Hamisi Hassan Abdallah, alisema uwanja huo mpya utaongeza uwezo wa Tanzania kuandaa mashindano ya kimataifa huku ukiwapatia wachezaji mazingira bora ya mazoezi yanayokidhi viwango vya kimataifa.
Alibainisha kuwa kwa muda mrefu TCA ilikuwa na uwanja mmoja pekee, hali iliyokuwa ikizuia juhudi za kuandaa mashindano makubwa kutokana na uhaba wa miundombinu inayokidhi matakwa ya mashirikisho ya kimataifa.Naye Afisa Mwandamizi wa Michezo kutoka Baraza la Michezo la Taifa (NSC), Apansia Lema, alisema Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya michezo ili kuibua na kukuza vipaji vya vijana nchini.
Alisema maendeleo ya mchezo wa kriketi yanaendelea kuimarika, huku zaidi ya shule 400 nchini zikishiriki mchezo huo. Aidha, alitaja kufuzu kwa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 19 kushiriki Kombe la Dunia la Kriketi 2026 kuwa mafanikio makubwa yanayoonyesha mwelekeo mzuri wa maendeleo ya mchezo huo nchini.
Uzinduzi wa TCA Cricket Arena unatarajiwa kuifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha kriketi katika ukanda wa Afrika Mashariki na kuongeza uwezo wa nchi kuvutia mashindano ya kimataifa, kuendeleza vipaji vya vijana na kukuza utalii wa michezo.




No comments:
Post a Comment