
erikali imeeleza kwamba matatizo ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa
Elimu ya Juu (HESLB) ni kulipwa kwa wanafunzi hewa, ubadhirifu wa
fedha...
erikali imeeleza kwamba matatizo ya
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ni kulipwa kwa
wanafunzi hewa, ubadhirifu wa fedha na kuwepo kwa watendaji wanaohusika
kuweka fedha za wanafunzi wanne kwa mwanafunzi mmoja.
Kadhalika imeeleza tabia ya HESLB
kujiona ‘Mungumtu’, kuwaona watoto wa Watanzania kama ni shida kwao na
wasiostahili kupewa mikopo na hata kuwa na majibu ya mkato yasiyokuwa na
chembe ya kazi ya utoaji huduma.
Waziri wa Elimu, Sayansi ya Teknolojia,
Profesa Joyce Ndalichako alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati
akizindua Bodi mpya ya HESLB na kuitaka kujitenga na menejimenti wakati
wa utekelezaji wa majukumu yake na kuhakikisha matatizo hayo yote ambayo
yapo katika taarifa aliyowakabidhi, yanakaguliwa upya, kuhakikiwa na
kufanyiwa kazi.
Pia alisema taarifa hiyo imeambatanisha taarifa ya fedha za HESLB zilizochezewa.
Alikabidhi taarifa hiyo kwa Makamu
Mwenyekiti wa bodi mpya, Madina Mwinyi akiagiza ifanyiwe kazi
kuhakikisha na kujiridhisha pamoja na kuwajua wadeni wa HESLB huku
ikiepuka kuiamini menejimenti kama ilivyokuwa kwa bodi ya awali badala
yake kuisimamia.
“Ninakabidhi taarifa yenye changamoto za
Bodi ya Mikopo kwenu Bodi ya Wakurugenzi ambayo inaainisha uwepo wa
wanafunzi hewa na ambao wanalipwa mikopo wakiwemo waliomaliza au kuacha
chuo,” alisema.
Pia alisema taarifa hiyo inahusisha
kuwepo kwa watendaji wanaohitajika kujieleza ambao walikuwa wakiweka
fedha za wanafunzi wanne kwa mwanafunzi mmoja ambapo ushahidi upo na
eneo hilo bado kuna shida.
Kadhalika, aliiagiza Bodi mpya kutazama
upya na kujiridhisha kuhusu vigezo vya utoaji mikopo kwani kumekuwa na
matatizo, na hata kutizama utoaji wa mikopo kama taratibu na sheria
zinazingatiwa.
“Malalamiko ya Bodi ya Mikopo yapunguzwe
ama kuondolewa kabisa ili kukidhi matarajio ya wadau wa elimu nchini,
endeleeni kukagua na hata majina ya wanaohitajika kupata mikopo kabla ya
kutolewa rasmi,” alisema Profesa Ndalichako.
Kuhusu Bodi mpya aliitaka isimamie zaidi
urejeshwaji wa mikopo kwani hadi sasa serikali imetoa Sh trilioni 3.1
tangu kuanzishwa kwa bodi, lakini ni Sh milioni 217 pekee zilizorejeshwa
huku Sh bilioni 588 zikiwa zimefikia muda wake zikitakiwa kulipwa.
Akizungumza baada ya bodi hiyo
kuzinduliwa, Makamu Mwenyekiti, Madina Mwinyi alisema katika kufanyia
kazi changamoto za HESLB wataanza kwa kujipanga wao wenyewe katika
taasisi wanamotoka ili kila mmoja kujua ni kiwango gani cha mikopo
kinachotakiwa kurejeshwa.
Kadhalika alisema bodi hiyo itahuisha
taswira ya HESLB pamoja na kuiaminisha jamii kuwa suala la mkopo wa
elimu ya juu ni lazima kurejeshwa kwa wakati.
Wajumbe wa bodi hiyo na taasisi
wanazotoka katika mabano ni Profesa Caroline Nondo (Mwakilishi kutoka
Tume ya Vyuo Vikuu), Susan Urio (Mwakilishi wa Wanafunzi), Madina Mwinyi
ambaye ni Makamu Mwenyekiti (Mwakilishi wa Wizara ya Elimu Zanzibar).
Wengine ni pamoja na Naibu Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Gerson Mdemu (Mwakilishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
wa Serikali), Dk Dalmas Nyaoro (Mwakilishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi
na Teknolojia), Frank Mgeta (Mwakilishi wa Wizara ya Fedha na Mipango),
Dk Francis Masika (Mwakilishi wa Baraza la Elimu ya Ufundi) na Mjumbe
mmoja ambaye ni Mwakilishi wa Wizara ya Fedha Zanzibar hajateuliwa.
No comments:
Post a Comment