Serikali
ya Tanzania na Finland zimetiliana saini mikataba mitatu yenye thamani
ya Euro milioni 28.8 sawa na Shilingi bilioni 75 kwa ajili ya kuendeleza
misitu, ubunifu na masuala ya uongozi.
Akizungumza
wakati wa utiaji saini wa mikataba hiyo, Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha
na Mipango, Bw. Doto James amesema, msaada huo kutoka Finland umetolewa
ili kuendeleza uwezo wa viongozi na kufanya
maamuzi sahihi yenye tija kwa ukuaji wa uchumi wa Taifa, mradi ambao
unasimamiwa na Taasisi ya Uongozi, ambapo kiasi cha Euro milioni 9.90
zimetolewa kuendeleza mradi huo.
Aidha
Serikali ya Finland imetoa kiasi cha Euro milioni 8.95 kwa mradi
wa kuiimarisha mfumo wa ubunifu nchini kwa kutengeneza mazingira rafiki
kwa wabunifu ili kuweza kubuni na kuendeleza ubunifu wao na kuchochea
ukuaji wa viwanda.
Bw.
James alisema fedha hizo zitatumika kuwasaidia wabunifu kwa kuwapatia
vifaa na msaada wa kitaalamu ili kuyaendeleza mawazo yao na kuyafanya
yawe ya kibiashara na kuweza kusaidia kubadili mawazo hayo kuwa
viwanda.
“Fedha
hizi zitasaidia kutatua changamoto katika viwanda vilivyopo nchini ili
vifanye kazi kwa ufanisi kwa kuwaunganisha wanataaluma mbalimbali
nchini, ikiwa ni pamoja na wabunifu wachanga, wataalamu kutoka vyuoni,
wataalamu kutoka Serikalini na Sekta binafsi” Alisema Bw. Doto James
Eneo
lingine lililonufaika na msaada huo ni programu ya misitu, ambayo
imepatiwa Euro milioni 9.95 kwa lengo la utuzaji wa misitu na uongezaji
thamani ya mazao yatokanayo na misitu ili kuongeza kipato kwa Wananchi,
kupunguza umasikini na kulinda mazingira.
Katibu
Mkuu amemshukuru balozi wa Finland Nchini, Mhe. Pekka Hukka kwa msaada
walioutoa na kwa kuunga mkono shughuli za maendeleo za Serikali, na
kuongeza kuwa Finland wamekuwa wakifadhili miradi mbalimbali nchini,
ukiwemo mradi wa kilimo biashara Mkoani Lindi na Mtwara (LIMAS),
uliogharimu Euro milioni 9, Mradi wa kuimarisha usambazaji na
upatikanaji wa umeme wa uhakika Jijini Dar es Salaam, uliogharimu Euro
milioni 25, na Programu ya maboresho ya Serikali za Mitaa, Euro milioni
10.5
Akizungumza
baada ya kupokea msaada huo Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Profesa Joseph
Semboja aliiishukuru Serikali ya Finland kwa kuendelea kuisaidia Taasisi
hiyo.
‘Hii
ni mara ya tatu Finland wamekuwa wakitusaidia kuendeleza jitihada
zilizoanzishwa na Serikali yetu ambapo awamu ya kwanza ilikuwa ni mwaka
2012 ambapo walitupatia Euro milioni 7, mwaka 2014 Euro milioni 12 na
sasa wametupatia Euro milioni 9.90 huu ni msaada mkubwa’ alisema Profesa Semboja.
Aidha
kwa upande wake Balozi wa Finland Bw. Pekka Hukka, aliishukuru Serikali
ya Tanzania kwa kuendeleza ushirikiano na Serikali yake, na kuongeza
kuwa msaada huo ni muhimu sana katika kutimiza malengo ya maendeleo ya
nchi.Amesema
msaada huo ukitumika ipasavyo hasa katika kuendeleza mnyororo wa
thamani wa mazao ya misitu utasadia kuongeza ajira na kuongeza pato la
Taifa.
Ameitaka
Serikali kupitia Wizara ya nishati, kushirikiana na sekta binafsi na
kuitumia fursa hiyo ya kuboresha misitu ili kuiongezea nchi mapato zaidi
yatakayotokana na makusanyo ya kodi.
Katibu
Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (kulia) akionesha kalamu
aliyozawadiwa na Balozi wa Finland Bw. Pekka Hukka (kushoto) ambayo
imetengenezwa kwa mbao, akionesha uzalendo wa matumizi ya misitu. Kutoka
kulia ni Kamishna wa Bajeti Wizara ya Fedha na Mipango Bibi. Mary
Maganga na Kamishna wa Fedha za Nje Bw. John Rubuga.
Katibu
Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Dotto James (kulia) akitia saini
moja kati ya mikataba mitatu yenye jumla ya shilingi bilioni 75 kama
msaada kwa Tanzania, Kushoto ni Balozi wa Finland Bw. Pekka Hukka kwa
pamoja wakisaini mikataba hiyo.
Katibu
Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (kulia) akibadilishana
mkataba na Balozi wa Finland Bw.Pekka Hukka. Mkataba wa kwanza wa Euro
milioni 9.9 ni kwa ajili ya kusaidia Taasisi ya Uongozi, wa pili wa Euro
milioni 8.9 kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa ubunifu na watatu wa Euro
milioni 9.5 ni kwa ajili ya program ya misitu.
Katibu
Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (kulia) pamoja na Balozi
wa Finland Bw. Pekka Hukka (kushoto) wakionesha moja ya mikataba mara
baada ya kumaliza kutia saini mikataba hiyo.
Mkuu
wa Taasisi ya Uongozi Prof. Joseph Semboja (Kulia) akiishukuru Serikali
ya Finland kwa kuwapatia msaada wa Euro milioni 9.9 ambayo itawasaidia
kuendesha shughuli mbalimbali za Taasisi hiyo. Kushoto ni Balozi wa
Finland Bw. Pekka Hukka.
Katibu
Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (katikati, waliosimama
mbele) akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya hafla ya utiaji saini
mikataba mitatu ya jumla ya shilingi bilioni 75. (Picha na Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)
No comments:
Post a Comment