Viongozi wa vyama 10 vya siasa vya
upinzani wamesisitiza bado kuna umuhimu wa kuendelea na mchakato wa
Katiba mpya itakayokuwa na misingi bora ya uongozi, kulinda rasilimali
za nchi na nidhamu kwa viongozi.
Wamesema Katiba iliyopo ina upungufu na
ilitengenezwa na watu wachache lakini mchakato wa upatikanaji wa Katiba
mpya chini ya Jaji Joseph Warioba uliwashirikishwa Watanzania wengi.
Vyama hivyo ni AFP, Chaumma, NCCR-Mageuzi, ADC, TLP, NLD, UPDP, SAU, Demokrasia Makini na DP.
Viongozi wa vyama hivyo wameeleza hayo
leo Jumanne Novemba 28, 2017 katika majadiliano kuhusu mchakato wa
Katiba mpya yaliyoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC).
Naibu Katibu Mkuu wa TLP, Richard Lyimo
amesema kwa hali ilivyo sasa hakuna ubishi kwamba Katiba mpya bado ina
umuhimu na itamsaidia Rais John Magufuli kutekeleza majukumu yake kwa
ufanisi.
"Rais Magufuli anafanya kazi nzuri na
tunazitambua juhudi zake, lakini tunahitaji Katiba mpya ili Rais
akiondoka na mwingine kuchukua madaraka ayaendeleze katika misingi bora
iliyopo kwenye Katiba," amesema Lyimo.
Katibu Mkuu wa SAU, Johnson Mwangosi ameungana na Lyimo akisema Katiba mpya ni lazima kwa masilahi na mustakabali wa Taifa.
Hata hivyo, akijibu swali bungeni hivi
karibuni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema Serikali inatambua
mchakato wa Katiba mpya lakini kwa sasa kipaumbele chake ni kuwapa
wananchi huduma za jamii.
Awali, akifungua mjadala huo, Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga amesema lengo la kuuandaa ni
kupata maoni kutoka kwa vyama vya siasa na hasa baada ya mchakato huo
kukwama.
Mwaka 2014, Bunge Maalumu la Katiba
lilivunjwa baada ya kumalizika kwa kupata Katiba iliyopendekezwa na
kilichobaki ni wananchi kupiga kura ya maoni ili kupata Katiba mpya.
No comments:
Post a Comment