Serikali imeanza kutoa Hati za kumiliki
ardhi ndani ya Kipindi cha Siku 30 tangu kupokelewa kwa maombi tofauti
na awali ambapo mchakato wa kupata hati hizo ulichukua zaidi ya siku 90
ikiwa ni matokeo ya mikakati madhubuti iliyowekwa ili kuondoa changamoto
zinazoikabili sekta ya ardhi hapa nchini.
Akizungumza katika kipindi maalum cha
TUNATEKELEZA kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na
kuratibiwa na Idara ya Habari (MAELEZO), Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amesema dhamira ya Serikali ya
Awamu ya Tano ni kuhakikisha kuwa kila kipande cha Ardhi kinapimwa na
kumilikishwa.
“Tumejipanga vizuri na sasa taarifa zote
za Ardhi zitakuwa katika mfumo wa kielektroniki utakaounganisha
taarifa za nchi nzima hivyo tutaweza kudhibiti vitendo vyote vilivyokuwa
vikifanyika awali kinyume na utaratibu na kuchochea kuongezeka kwa
migogoro ya Ardhi hapa nchini,” alisisitiza Lukuvi
Ameendelea kwa kusema, hatua
zinazochukuliwa na Serikali ni pamoja na kutenga muda wa kuwasikiliza
wananchi na kuzipatia ufumbuzi chanagamoto zinazowakabili ikiwemo
kudhulumiwa viwanja ambapo Serikali imekuwa ikirudisha umiliki kwa
wananchi husika pale inapojiridhisha kuwa ndiye mmiliki halali wa eneo
husika.
Aliongeza kuwa, mapato ya Serikali
yemeongezeka kutoka milioni 46 hadi Bilioni 100 kwa mwaka ikiwa ni kodi
ya Ardhi. Aidha, kuongezeka kwa mapato hayo kumetokana na usimamizi
madhubuti wa Serikali katika sekta ya ardhi hapa nchini ili kuwapa
wananchi wote fursa yakutumia ardhi na kujiletea maendeleo.
Vile vile amesema, hatua nyingine
zinazochukuliwa na Serikali ni pamoja na kuanzisha ofisi za Kanda
zitakazokuwa zikitekeleza majukumu yanayotekelezwa na wizara ikiwemo
kutoa hati ili kusogeza huduma kwa wananchi hasa wanyonge waliopo
Vijjini ambao mara nyingi hushindwa kusafiri hadi makao makuu ya Wizara
kufuata huduma hizo.
Pia Lukuvi alibainisha kuwa Serikali
imenunua vifaa vya upimaji ardhi vitakavyotumika katika Ofisi za Kanda
ili kuwawezesha watumishi wake kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi hali
itakayosaidia sekta hiyo kutoa mchango mkubwa katika kujenga uchumi.
“Hati za Kimila elfu 46,000
zimeshatolewa kwa wananchi ili kuwawezesha kuwa na milki salama ambazo
zitachochea maendeleo katika maeneo yao kwani zinaongeza thamani ya
ardhi ya eneo husika, vile vile maeneo ya makazi zaidi ya 200,000
yametambuliwa na kurasimishwa,” alisisitiza Lukuvi
Aidha Mhe. Lukuvi amewaasa wamiliki wa
mashamba makubwa kuyaendeleza vinginevyo Serikali itayatwaa na
kuyamilikisha kwa wananchi ili wayatumie kwa shughuli za uzalishaji
ambapo kwa sasa mashamba makubwa zaidi ya 150 yamefutiwa umiliki na
kurudishwa kwa wananchi.
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi ni moja ya Sekta muhimu katika kujenga uchumi wa Viwanda na
imekuwa ikichukua hatua mahususi katika kutatua changamoto zinazoikabili
sekta ya Ardhi. Hatua hizo zinajumuisha ujenzi wa Kanzi Data ya taarifa
za ardhi kwa nchi nzima na pia kuunganisha mifumo yake na Mamlaka ya
Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ili kuimarisha mchango wa sekta hiyo
katika kujenga uchumi wa viwanda.
No comments:
Post a Comment