Na Thabit Madai, Zanzibar.
IMEELEZWA kuwa Visiwa vya Zanzibar ni miongoni mwa sehemu barani afrika zenye uvumilivu mkubwa wa kisiasa, kidini na kikabila ambapo wananchi wake wanaishi kwa upendo, Amani na utulivu.
Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati ya Amani kitaifa Zanzibar Sheikh Fadhili Soraga wakati akifungua mafunzo ya Wiki Moja kwa wakufunzi wa masuala mbalimbali ya Amani kutoka nchi zaidi ya 14 barani afrika, ambapo mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Hotel ya Blue Bay Beach Resort kiwenga Kaskazini Unguja.
Sheikh Soraga alisema kuwa, kwa sasa jamii ya Zanzibar imepiga hatua kubwa katika suala zima la kulinda amani na utulivu ulipo huku wananchi wakiishi kwa uvumilivu wa kisiasa, kidini na kikabila.
“Jamii yetu ya Zanzibar imepiga hatua kwa kiasi kikubwa ambapo licha ya watu wake kuwa na Imani ya Dini, Makabila tofauti na hata mitazamo tofauti ya vyama vya kisiasa bado wanaishi kwa Amani na utulivu huku kila mmoja akimvumilia mwengine,”alisema.
Aliongeza kuwa mafanikio hayo yanatokana na uwepo wa mradi wa Amani Zanzibar ambapo kwa kiasi kikubwa umekuwa ukihubiri Umoja na mshikano kwa jamii bila ya kujali utofauti wa Dini, Kabila na vyama vya siasa.
“Ni jambo la faraja sana kuona watu wanatoka sehemu mbalimbali kuja kujifunza namna ya Zanzibar wanaishi kwa amani na utulivu ambayo kimsingi imetokana na juhudi za Viongozi wa Dini ya Kiislamu na kikristo nchini ambao wamezunguka kila koda kuhubiri Amani na upendo kwa jamii,” alisema Soraga.
Soraga alifafanua kuwa kabla ya mradi wa Amani Zanzibar jamii iliishi kwa chuki kubwa na kupelekea baadhi ya viongozi Dini kumwagiwa tindikali na wengine kupigwa risasi.
“Hapo nyuma hali ilikuwa mbaya sana watu waliishi kwa kuchukiana kutokana na Imani za Dini, Kabila na vyama vyao vya siasa mfano mimi binafsi nilimwagiwa tindikali kutokana na kuhubiri huu umoja baina ya wakristo na waislamu,” alieleza.
Katika hatua nyingine Sheikh Soraga aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuunga mkono juhudi zinazofanywa na viongozi mbalimbali wa Dini katika kulinda kudumisha Amani iliyopo nchini na kuwa wadau wakubwa katika mradi wa Amani Zanzibar.
Nae Katibu Mkuu wa majimbo ya Makanisa ya Anglikana afrika, Askofu Johnson Kofi aliiomba Serikali kuendelea kuunga mkono mradi huo kwani umeleta manufaa kwa waislamu wa dini tofauti pamoja na kuwaunganisha pamoja.
Aidha alisema kupitia mafunzo yanayotolewa kupitia mradi huo kwa viongozi wa dini umeweza kuwaunganisha na kuacha tofauti zilizokuwa zikijitokeza kwa waumini wao.
Kwa upande wake Maneja wa Mradi wa Amani Zanzibar Jamal Ali Hassan aliwashauri washiriki wa mafunzo hayo kuwa wanatakiwa kuunda kamati za Amani za Viongozi wa Dini Kitaifa pamoja Viongozi wa Serikali kuwa karibu na Viongozi wa Dini.
“tumewashauri wenzetu kufikia hapa tulipo sisi kwanza waunde kamati za Amani za viongozi wa Dini, Mashekhe, ofisi za fufti na maofisi ya maaskofu wanakutana wao na kujadiliana na kushusha ujumbe chini taasisi zilizokuwa chini yao,” alisema.
Alisema kuwa, ukaribu kati ya Viongozi wa Dini na viongozi wa Serikal unapelekea ka kiasi kikubwa kuelewana na wote kusisitiza suala zima la Amani na utulivu,” alibainisha.
“Pia tumewashauri kuwa viongozi wao wa Dini kuwa karibu na Serikali, ambapo hapo tumeona huko kwao hakuna viongozi wa Dini hawazungumzi vizuri na Serikali,”alieleza.
Katika hatua nyingine alieleza kuwa Uwepo wa Amani na utulivu pamoja na uvumilivu mkubwa wa wananachi wake umepelekea watu kutokana nchi mbalimbali kuja kujifunza Zanzibar kwa namna gani wameweza kufanikiwa.
“Tumeweka mafunzo haya ya wakufunzi wa masuala ya Amani hapa Zanzibar ili hawa watu kutoka mataifa mbalimbali wapate kujifunza namna ya Zanzibar ilivyofanikiwa kuwa na Amani na utulivu ambao umetokana na Mradi wa Amani Zanzibar,” alieleza.
Mradi wa Amani Zanzibar ni mradi endelevu unaofadhiliwa na Umoja wa nchi za Ulaya ambao ulianza mwaka 2018 na kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba.
No comments:
Post a Comment