Wakulima ambao hawajapeleka korosho zao katika maghala ya vyama vya msingi kwa ajili ya mauzo wameombwa wapeleke haraka ili kuwahi kabla ya msimu wa ununuzi kwa msimu wa 2021/2022 kufungwa.
Wito huo ulitolewa jana mjini Nachingwea na kaimu mkurugenzi wa masoko na udhibiti ubora wa korosho wa Bodi ya Korosho Tanzania(CBT), Domina Mkangara alipozungumza na wakulima walioshiri mnada wa kumi wa chama kikuu cha ushirika cha RUNALI kwa msimu wa 2021/2022.
Mkangara ambae aliwapongeza wakulima wa zao hilo kwakulinda ubora alisema kunahaja ya wakulima wasiopeleka korosho zao maghalani wapeleke haraka ili kuwahi soko kabla ya msimu wa ununuzi kufungwa.
Alisema baadhi ya wakulima wamehifadhi korosho majumbani wakitarajia mabadiliko ya bei. Hatahivyo hakuna dalili za bei ya zao hilo kuongezeka katika msimu huu.
Alibainisha kwamba msimu huu umekuwa na changamoto ambazo zimesababisha wanunuzi wanunue kwa bei ndogo. Nakwamba baadhi ya wanunuzi hawajapeleka korosho zao nje ya nchi kutokana na changamoto hizo.
Kwakuzingatia ukweli huo Mkangara alisema ni vigumu bei kuongezeka. Huku idadi ya wanunuzi ikiendelea kupungua.
" Kupungua wanunuzi kunasababisha ushindani sokoni kupungua. Kwahiyo hatutaraji mabadiliko ya bei, hasa kwenye kuongezeka," alisema Mkangara.
Aidha kaimu mkurugenzi huyo aliweka wazi kwamba ubora wa korosho msimu huu ni mkubwa na kiwango cha uzalishaji kinaridhisha. Kwani bado kiasi kidogo tu cha uzito ili kufikia lengo. Ambapo hadi sasa imefanyika minada 56 nchini kote kwa msimu wa 2021/2022.
Nae mwenyekiti wa RUNALI Audax Mpunga alisema wakulima ambao wameuza korosho kupitia chama hicho wanastahili pongezi kwa kudhibiti ubora. Kwani chama hicho kinaweza kuwa katika nafasi ya juu kwakuuza korosho bora kuliko vyama vikuu vingine.
Mpunga alisema wakulima ambao wameuza korosho kupitia chama hicho nipamoja na wakulima wa mkoa wa Morogoro ambao korosho zao zinahifadhiwa kwenye ghala la Kibaoni.
" Hata korosho za Morogoro ni nzuri na bora sana na hazina tofauti yoyote. Sisi kama RUNALI tutaendelea kupokea korosho zao kwani zinauzika sokoni," alisisitiza Mpunga.
Alitoa wito kwa wakulima wa korosho mkoani humo waendelee kuzalisha zao hilo kwa wingi ili liwakomboe kiuchumi kama ilivyo kwa mikoa ya Lindi na Mtwara.
No comments:
Post a Comment