Katika jitihada za kuendeleza sekta ya usafirishaji nchini Tanzania kampuni ya uuzaji na utengenezaji wa magari ya kusafirisha mizigo ya Sinotruk International inatarajia kujenga kiwanda cha kuunda magari ya kusafirisha mizigo nchini ili kurahisisha shughuli za wafanyabiashara nchini.
Hayo yalisemwa wakati kampuni ya GSM kupitia kampuni yake ya Usafirishaji ya Galco Limited ikikabidhiwa malori mapya zaidi ya 100 kutoka kwa kampuni ya uundaji malori ya SINOTRUK International.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla fupi ya makabadhiano ya magari hayo Meneja Mkuu wa kampuni ya Sinotruk International nchini Tanzania, Bw. Li zhongyuan amesema kuwa, “Mwaka 2022, Kampuni za Sinotruk and Saturn Corporation Limited tunatarajia kujenga kiwanda cha uundaji wa vifaa vya malori/magari ya mizigo Tanzania.
“Katika Nyanja ya usafirishaji, Sinotruk imefanikiwa kutoa huduma zake na kuanzisha mahusiano ya muda mrefu na makampuni makubwa kama vile GSM, Dangote, OILCOM(T) LIMITED, Tanzania Road Haulage (1980) Limited, Golden Coach/Fleet Ltd, ASAS, AZAM, na Mount Meru. Malori ya HOWO yametamalaki katika mipaka ya nchi, majiji, na vijiji tofauti nchini. Kwa kuzingatia kuwa na mahusiano mazuri ya kibiashara ndani ya nchi na uwezo wa kuhudumia masoko ya nje, Sinotruk inatoa mchango mkubwa wa maendeleo ya ufanisi katika kiwanga cha shughuli za usafirishaji nchini Tanzania,” alihitimisha Meneja Mkuu wa Sinotruk nchini Tanzania.
Naye kwa upande wake Afisa Biashara Mkuu wa GSM, Bw. Allan Chonjo amebainisha kuwa, “Leo ni siku njema sana kwetu sisi GSM Pamoja na wateja wetu wote ndani na nje ya Tanzania kwa maana tumeongeza uwezo na ufanisi wa kufanya biashara hii ya usafirishaji kwa kuongeza malori mengine mapya na kufanya idadi ya malori yetu kufikia 800.”
“GSM Kupitia Galco imekua ikifanya usafirishaji wa mizigo kwa malori makubwa ya Tani 30 ndani na nje ya nchi kwa takribani miaka 10 sasa. Nchi zinazohudumiwa ni; DRC Congo, Msumbiji, Malawi Zambia, Burundi, Rwanda, Uganda, Kenya Pamoja na Sudan ya kusini. Galco ina ofisi tatu, Tanzania, Zambia Pamoja na Afrika kusini hivyo nchi zote za Afrika Mashariki na Kati Pamoja na za ukanda wa SADC zinahudumiwa kwa ufanisi mkubwa,” aliongezea Bw. Chonjo.
“Sambamba na kufungua fursa, tunapenda kuishukuru serikali yetu kwa kuendelea kuimarisha mahusiano ya nchi yetu na nchi Jirani. Isingekua rahisi kwetu kuweza kuingia na kutoka kwenye nchi za watu bila bugudha kama mahusiano yetu na nchi hizo yasingekuwa mazuri. Matokeo yake na sisi tunatoa fursa kwa wadau wengine ikiwemo ajira, ubora wa huduma na kuongeza pato la taifa,” alihimitimisha Afisa Biashara Mkuu wa GSM nchini Tanzania.
Sinotruk ni miongoni mwa makampuni makubwa ya utengenezaji wa malori duniani ambapo tayari imeshauza bidhaa zake katika nchi zaidi ya 110. Kampuni ina uwezo wa kusafirisha malori takribani 50,000 ya kusafirisha mizigo na kufanya kazi nzito kwa mwaka, na imeshikilia nambari moja kwa viwango kwenye sekta ya magari ya mizigo mizito nchini China kwa miaka 17 mfululizo.
Mwanzoni mwa miaka ya 1970, malori 731 aina ya Sinotruk Huanghe yametumika katika ujenzi wa reli ya Tanzania na Zambia. Siku zote Sinotruk imekuwa ikijizatiti katika kuunga mkono maendeleo ya miundombinu ya Tanzania kwa kuwapatia huduma wananchi wake na mustakabali wa maendeleo yao. Kwa sasa, Sinotruk inafanya kazi katika mradi wa kituo cha Uzalishaji Umeme cha Mwl. Nyerere, mradi wa Reli ya Kisasa, viwanja vya ndege, na ujenzi wa barabara katika maeneo tofauti nchini.
No comments:
Post a Comment