Namna Rais John Pombe Magufuli alivyojaribu kuibadili CCM Tanzania - KABATA

This is the special room for news where you need to settle with!


Breaking

Tuesday 15 March 2022

Namna Rais John Pombe Magufuli alivyojaribu kuibadili CCM Tanzania

 

.

CHANZO CHA PICHA,ERICKY BONIPHACE/GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,

Rais John Pombe Magufuli

line

Ni mwaka mmoja sasa tangu kutokea kifo cha rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani hayati John Pombe Magufuli.Wiki hii tutakuletea makala maalum kuhusu mambo mbali mbali ya utawala wake hadi nyakati zake za mwisho kama rais.

line

MEI 29, 2018, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilimtangaza Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, kuwa Katibu Mkuu wake mpya kuchukua nafasi ya Abdulrahman Kinana aliyeomba kupumzika wadhifa huo. Uteuzi huo ulishangaza wengi kwa vile kiongozi huyo mpya hakuwa maarufu kiutendaji na kiuongozi ndani ya chama, ukiacha kuteuliwa kuongoza Kamati iliyohakiki mali za chama hicho.

Katika wiki yake ya kwanza kazini, Dkt. Bashiru alifanya jambo ambalo halikuwa "la kawaida" kufanywa na kiongozi wa CCM. Kuna kigogo mmoja wa sekta ya habari nchini Tanzania alitaka kumpa kisimbuzi baada ya kubaini kwamba kiongozi huyo mpya hana kisimbuzi cha kampuni yake na hivyo asingeweza kuwa anatazama vipindi vya kituo hicho.

Kisimbuzi hicho kilipelekwa nyumbani kwa Bashiru mjini Dodoma lakini muda mfupi baadaye, Katibu Mkuu huyo alipiga simu kwa kigogo huyo kumweleza kwamba ameletewa kisimbuzi hicho lakini anakirudisha kwa sababu za kimaadili na badala yake atanunua kingine kwa fedha zake mwenyewe.

Kabla ya Bashiru, ilikuwa kawaida kwa baadhi ya viongozi wa CCM kuomba kupewa visimbuzi vya bure na kampuni zinazouza bidhaa hizo ili wanachama wao katika matawi, majimbo ya uchaguzi na ofisi za chama wapate mahali pa kutazama televisheni. Kwa maelezo yale ya Bashiru, kigogo huyo alifahamu kwamba CCM aliyoizoea itabadilika kuanzia hapo.

Bashiru ni mfano mmoja wa aina ya uteuzi uliokuwa ukifanyika ndani ya CCM wakati wa uenyekiti wa John Magufuli aliyefariki Machi 17, 2021. Urais na uenyekiti wake wa CCM ulikuwa unaenda sambamba na dhamira yake ya kutaka kuisuka upya CCM. Kabla ya kuingia kwa undani kuangalia ni kwa namna gani aliibadili CCM, ni vizuri kwanza kumtazama mwenyekiti huyo wa zamani wa CCM na historia yake kwenye chama hicho.

Wanachama wa CC

CHANZO CHA PICHA,IKULU TANZANIA

Mwenyekiti na rais asiyetarajiwa

Uchambuzi wowote kuhusu urais na uenyekiti wa Magufuli ni muhimu uanzie kwenye ukweli kwamba yeye mwenyewe kwenye chama alikuwa akionekana mgeni hasa kwa kukosa mizizi ya uongozi na kiutendaji chamani. Kulinganisha na watangulizi wake kama Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete - Magufuli alikuwa "kichuguu" miongoni mwa milima.

Mmoja wa washindani wake katika kuwania urais kupitia CCM na mmoja wa wanasiasa mashuhuri Tanzania, Prof. Mark Mwandosya, alipata kuonesha wasiwasi wa uwezo wa kiuongozi wa mtu ambaye kwenye maisha yake hajawahi kuwa hata mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC).

Magufuli naye alitambua upungufu huo kwenye maisha yake ya kisiasa. Kwenye mazungumzo ya binafsi na mmoja wa maswahiba wake wa kisiasa, mwenyekiti huyo aliwahi kuzungumza kuhusu hali ya kwamba kila mtu anayetaka kuanza kumwamini - "kuna watu" walikuwa wakimwambia; "Huyo wa Kikwete usimwamini… Huyo wa Lowassa au wa Kinana".

Rais huyo wa tano wa Tanzania alianzia maisha yake kama mwalimu na akajitosa kuwania ubunge mara ya kwanza 1990 akakosa na kupata mara ya pili 1995 pasipo kuwa na nafasi yoyote kwenye chama. Wasiwasi wake dhidi ya wale aliodhani hawamuoni kama "mwenzao" na wanaomuona kama "wa kuja" ulimfanya Magufuli kuamua kutengeneza aina mpya ya ufanyaji wa siasa na chama ambacho kingeakisi sura yake na ufanyaji kazi wake.

Namna CCM ilivyoanza kubadilishwa na Magufuli

Kiutamaduni, CCM ni chama ambacho kina makundi miaka yote. Jambo pekee ambalo linakifanya kionekane kimoja ni madaraka na uwezo wa kugawana fursa. Kitendo cha kubadilishana madaraka kila baada ya miaka 10 kwa Rais aliye madarakani kumekifanya chama hicho kifanikishe makundi tofauti kufaidi madaraka kila anapoingia mtu mpya.

Wakati wa Nyerere kuna kundi lilifaidika, kwa Mwinyi, Mkapa na Kikwete hivyohivyo. Hata sasa, kuna wanachama wanaendelea kuwa watiifu kwa sababu wanafahamu kwamba kuna mgombea ataingia madarakani na kundi lao litanyanyuka.

Tofauti ya Magufuli na watangulizi wake ni kwamba wakati wenzake walikuwa na makundi yao ndani ya chama, yeye aliamua kutoka nje na kutafuta watu wa kuwaingiza kwenye chama. Matokeo yake ni CCM kuanza kuingiza watu wa aina ya Bashiru ambao hawakujulikana kama makada awali na walionekana kuwa wageni miongoni mwa waliozoeana.

Taratibu, majina yaliyozoeleka miongoni mwa wana CCM yakaanza kuondolewa kwenye chama na kuingizwa majina mapya. Wanasiasa vijana wa CCM kama vile Nape Nnauye na January Makamba wakaanza kuonekana kama maadui kwenye chama na Emmanuel Nchimbi akapelekwa ubalozini nchini Brazil. Kuna kipindi wanachama wengine vijana kama Mwigulu Nchemba na Hussein Bashe nao waliwekwa kando kabla ya kurejeshwa serikalini.

Baadaye, vigogo kama akina Kinana na Yusuf Makamba waliowahi kuwa makatibu wakuu wa CCM wakawa wanakashifiwa na kuandikwa vibaya na vyombo vya habari vilivyokuwa vikitajwa kuwa na uhusiano wa karibu na dola. Hali ilikuwa mbaya kiasi kwamba ilifika wakati Kinana na Makamba waliandika waraka wa wazi kuhoji kuchafuliwa kwao. Haikuishia hapo kwani walijadiliwa na Kamati Kuu ya CCM Februari 2020. Makamba akasamehewa, Kinana akapewa adhabu ya karipio na mwanachama mwingine aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe akafukuzwa uanachama.

Kukosoana marufuku

Miongoni mwa wana CCM wa muda mrefu, kikao cha NEC kimekuwa na heshima yake. Kwa taratibu, hicho kilikuwa ni kikao ambacho wajumbe huwa huru kujieleza wanavyotaka. Inaelezwa kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa akipata taabu kwenye vikao hivyo kwa namna wajumbe walivyokuwa wakali.

Katika mkutano wa mwisho wa NEC kupitisha mgombea urais mwaka 2015, wajumbe waliomuunga mkono Edward Lowassa waliimba wimbo kikaoni wa kuonesha kuwa na imani na Lowassa ambaye hata hivyo, jina lake lilikuwa limekatwa hivyo kutokuwemo miongoni mwa majina matano ambayo yalichujwa na kubakia matatu yaliyowasilishwa kwenye mkutano mkuu na hatimaye kuteuliwa Magufuli kuwa mgombea wa CCM.

.

CHANZO CHA PICHA,IKULU TANZANIA

Maelezo ya picha,

Rais Samia

Magufuli alianzisha utaratibu mpya. Mara kwa mara vikao vya NEC vikawa vinafanyika Ikulu na si kwenye kumbi za mikutano za CCM. Wajumbe walikuwa wakieleza namna kulivyokuwa na ulinzi mkali na mazingira ya kuonesha kikao kile si kati ya watu wanaofanana.

Kwa maneno ya mmoja wa vigogo wa CCM, "chama hakikuwa kimeshika hatamu, bali mwenyekiti wa chama ndiye aliyekuwa na hatamu". Matokeo yake, CCM kikaanza kuwa chama cha "ndiyo mzee" tofauti na kile kilichokuwa kinakaribisha mijadala mikali na mivutano.

Utaratibu huo wa Magufuli haukuishia kwenye chama chake. Ulikwenda pia hadi nje ya chama ambako badala ya kutegemea nguvu na ushawishi wa wanachama wake, nguvu ya dola ilianza kutumika waziwazi. Uchaguzi wa kuwania ubunge na udiwani ulianza kuwa na vitendo visivyo vya kidemokrasia - tukio la kukumbukwa zaidi likiwa lile la kifo cha mwanafunzi siku moja kabla ya uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kinondoni Dar es Salaam Februari, 2018. Viongozi mbalimbali wa chama cha upinzani Cahdema waliokuwa katika maandamano siku ya tukio hilo walifunguliwa mashtaka mahakamani lakini baadaye mashtaka hayo yalifutwa.

Mfumo wa CCM kama chama dola umekuwa ukituhumiwa kukisaidia kushinda uchaguzi kwa miaka mingi lakini tofauti ya Magufuli na watangulizi wake ni kwamba yeye alitamka mara kadhaa hadharani kwa viongozi wa serikali kwamba hatakubali kulipa mishahara yao kama hawakisaidii chama hicho kushinda.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, CCM ilipata ushindi mkubwa lakini si kwa sababu ya kushawishi au kupendwa na watu lakini kwa sababu Magufuli hakujali kutumia njia yoyote kupata ushindi. Viongozi wa CCM wamekuwa wakikanuisha hali hiyo na kusema kuwa yeyote anayeona kutondewa hai katika uchaguzi aende mahakamani. Hata hivyo kwa sheria za Tanzania kesi inaweza kufunguliwa kupinga matokeo ya uchaguzi kwa ngazi mbalibali ikiwemo ubunge na udiwani lakini ni marufuku kufanya hivyo kwa ngazi ya urais.

Magufuli aliposhinda urais awamu ya pili 2020, kulikuwa na tuhuma kwamba alijiandaa au aliandaliwa kukubali mabadiliko ya Katiba ya nchi ili aruhusiwe kuwania muhula wa tatu wa urais. Kwa namna hali ilivyokuwa inaonekana, kungekuwa na uwezekano mdogo wa CCM kumzuia endapo angetaka kufanya hivyo.

Wakati anafariki dunia, hakukuwa na mtu wa kuzuia asifanye anachotaka ndani ya CCM wala serikalini huku baadhi viongozi akiwemo aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai na aliyekuwa mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy Mohamed wakitamka kuwa angelazimishwa kugombea "atake asitake". Hata hivyo Magufuli mwenyewe aliwahi kutamka mara kadhaa kuwa asingeongeza hada dakika moja baada ya kukamilika kwa mihula miwili ya uongozi.

Mwaka mmoja baada ya Magufuli

Baada ya kifo cha Magufuli, tayari CCM imeanza kurejea kwenye hali yake ya zamani. Mwenyekiti wake wa sasa, Rais Samia Suluhu Hassan, ni mwanaCCM na mmoja wa wajumbe wa muda mrefu wa Kamati Kuu ya chama. Tofauti na mtangulizi wake, yeye anakijua chama na ametokea kwenye chama.

CCM inafanya vikao vya NEC ambavyo wajumbe wanaeleza wameanza kuzungumza kwa uhuru na uwazi, vinafanyika kwenye kumbi za CCM na Ikulu na mazungumzo baina ya chama tawala na vile vya upinzani - ambayo ni kama yalikufa wakati wa Magufuli, yameanza upya.

Rais Magufuli na Mtangulizi wake Kikwete

CHANZO CHA PICHA,STRINGER/GETTY IMAGES

Vijana waliolelewa na kukuzwa na chama hicho kama Nape, January na Mwigulu sasa wamepewa nafasi kubwa serikalini na wanaonekana kama watu wa karibu na Rais. Vyombo vya habari vilivyokuwa vikikashifu wastaafu na wapinzani wa Magufuli ndani ya CCM sasa havina nguvu kubwa na kuna dalili za Bernard Membe kurejeshewa uanachama wake wa CCM baadaye.

Baada ya takribani miaka sita ya misukosuko, sasa tunaweza kusema 'CCM imerejea kwa wenyewe'.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here