Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Martine Reuben Shigela kutokana na vifo vya watu 22 katika ajali ya barabarani.
Ajali hiyo imetokea tarehe 18 Machi, 2022 katika eneo la Melela Kibaoni Darajani, wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro saa 10:30 jioni na kusababisha vifo vya wanaume 15, wanawake 6 na mtoto mmoja wa kiume.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Fortunatus Musilimu, ajali imehusisha basi lenye namba T 732 ATH aina ya Scania, mali ya kampuni ya Ahmeed lililokuwa safarini kutoka Mbeya kwenda Tanga kugongana na lori aina ya Howo lenye namba IT 2816 likielekea nchi jirani.
Ajali hiyo ambayo imesababisha majeruhi 38 imetokana na uzembe wa dereva wa lori kutaka kuipita pikipiki (overtake) bila kuchukua tahadhari katika eneo lisilokuwa salama kabla ya kugongana na basi hilo.
Aidha, Rais Samia amevitaka vyombo vyote vinavyosimamia usalama barabarani kuongeza juhudi za kudhibiti ajali. Ametumia pia nafasi hiyo kuwaasa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani.
Rais Samia pia anawapa pole wafiwa wote na anaungana na familia hizo katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
Mungu azilaze roho za marehemu wote mahali pema peponi. Amina.
No comments:
Post a Comment