Ndugu Wananchi, Wizara ya Afya ina utaratibu wa kufuatilia taarifa za magonjwa ya milipuko yakiwemo yale yanayozuilika kwa chanjo kama Surua, Rubella, Polio na Homa ya Manjano ili kudhibiti magonjwa haya hapa nchini. Wizara pia hufuatilia uwepo wa milipuko ya magonjwa mbalimbali katika nchi jirani tulizopakana nazo ili kuchukua tahadhari za haraka na kuzuia magonjwa hayo yasiingie nchini kutokana na mwingiliano wa watu katika shughuli za kibiashara au kijamii.
Ndugu Wananchi, mnamo tarehe 03 Machi, 2022 Wizara ya Afya ilipokea taarifa kutoka Ofisi ya Shirika la Afya Duniani (WHO) iliyopo hapa nchini, ikielezea kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa Homa ya Manjano nchini Kenya katika County ya Isiolo umbali wa takribani Kilomita 285 (Kaskazini mwa Nairobi) . Taarifa hiyo ilieleza kuwa, mgonjwa wa kwanza mwenye dalili za ugonjwa huu alipatikana mnamo tarehe 12 Januari 2022 na hadi kufikia tarehe 03 Machi 2022, kulikuwa na jumla ya wagonjwa 15 na vifo vitatu (3) vilivyotokana na ugonjwa huu. Aidha, kati ya sampuli sita (6) zilizopimwa katika maabara ya Kenya (KEMRI), sampuli tatu (3) zilithibitika kuwa va virusi vya homa ya Manjano kwa kutumia vipimo vya serology na PCR. Vilevile, kumekuwa na tetesi za kuwa na wagonjwa wenye dalili za homa ya Manjano katika nchi za Uganda, Sudan ya Kusini na Chad.
Ndugu Wananchi, hapa nchini kwetu taarifa za kipindi cha miezi mitatu iliyopita katika mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa yaliyopewa kipaumbele wa (Integrated Disease Surveillance and Response-IDSR) zinaonesha kuwa hapajakuwepo na taarifa zinazoashiria kuwepo kwa ugonjwa wa Homa ya Manjano. Vile vile katika kipindi hiki, mfumo wa taarifa wa ufuatiliaji wa tetesi za magonjwa haujaashiria kuwepo kwa dalili za ugonjwa huo hapa nchini. Hata hivyo, ninatoa tahadhari kwa wananchi ili kuchukua hatua na kuhakikisha ugonjwa huu hauingii nchini kwetu.
Ndugu Wananchi, ugonjwa wa Homa ya Manjano husababishwa na virusi ambavyo huenezwa na mbu aina ya Aedes, kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na vilevile kati ya mtu na mtu. Watu wanaofanya kazi kwenye misitu huweza kuambukizwa kwa kung’atwa na mbu ambao hupata vimelea vya ugonjwa huo kutoka kwa wanyama wa porini kama Nyani nk. Vilevile ugonjwa huo huambukizwa kati ya mtu na mtu pindi mtu mwenye virusi hivyo anapoumwa na mbu na hatimaye kueneza kwa mtu mwingine.
Ndugu Wananchi, dalili za ugonjwa wa Homa ya Manjano ni pamoja na homa, kuumwa na kichwa, maumivu ya misuli pamoja na mgongo, mwili kutetemeka, kupoteza hamu ya kula, kusikia kichefuchefu na kutapika, mwili kuwa na manjano, kutokwa na damu sehemu za wazi kama mdomoni, puani, machoni na tumboni na wakati mwingine damu huonekana kwenye matapishi na kinyesi na ugonjwa unapokuwa mkali figo hushindwa kufanya kazi. Kipindi cha kuonekana kwa dalili za ugonjwa huu ni kati ya siku 3 hadi 6 baada ya kuambukizwa.
Ndugu Wananchi, ugonjwa wa Homa ya Manjano hauna tiba mahsusi bali mgonjwa anayezidiwa uhitaji huduma ya karibu, ambapo mgonjwa anatibiwa kutokana na dalili zinazojitokeza. Mara nyingi matibabu yanahusisha utoaji wa dawa za kushusha homa na kupunguza maumivu au kuongezewa maji mwilini kwa kunywa au kwa kuwekewa dripu.
Ndugu Wananchi, ugonjwa huu unazuilika kwa njia ya chanjo ambayo kutokana na ushauri wa Shirika la Afya Duniani (WHO) hutolewa kwa wasafiri hasa wanaokwenda katika nchi zile ambazo zimekuwa na ugonjwa huu ili kuwazuia wasafiri hao wasipate ugonjwa na kuingiza katika nchi zao pindi wanaporejea. Hapa nchini, pamoja na utoaji wa Chanjo kwa wasafiri, ufuatiliaji wa kina umekuwa unafanyika kwenye mipaka yetu ili kuhakikisha kuwa wasafiri wanaoingia kutoka katika nchi zilizokwishakuwa na ugonjwa huu wana vyeti vinavyoonesha kuwa wamepata chanjo hiyo.
Ndugu Wananchi, katika nchi za Afrika Mashariki, Tanzania haijawahi kuwa na taarifa ya mgonjwa yeyote aliyethibitika kuwa na ugonjwa wa Homa ya Manjano tangu mwaka 1950. Aidha, katika mfumo wetu wa kutolea taarifa za magonjwa yaliyopewa kipaumbele(IDRS), ugonjwa wa Homa ya Manjano ni mojawapo ya ugonjwa unaotolewa taarifa ndani ya saa 24 tangu anapopatikana mgonjwa aliyethibitika nchini. Takwimu zetu kupitia mfumo huo zimekuwa zikionesha kuwa hakuna ugonjwa tangu mfumo huo uanze kutumika nchini mnamo mwaka 2000.
Ndugu Wananchi, baada ya kupata taarifa za ugonjwa huo katika nchi ya Kenya, Serikali kupitia Wizara Afya inaendelea kuchukua hatua zote stahiki ikiwa ni pamoja na kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa watu wenye dalili za ugonjwa katika vituo vya Afya vya bandari, viwanja vya ndege na mipakani kwa wasafiri watokao nje ya nchi na kuhakikisha kuwa wasafiri watokao nchi zenye hatari ya ugonjwa huo wanakuwa na uthibitisho wa chanjo ya Homa ya manjano kabla ya kuruhusiwa kuingia nchini. Sambamba na hatua hizi, Wizara itaendelea kufanya yafuatayo:
· Kufuatilia kwa karibu wasafiri wote wanaoingia nchini hususani kutoka nchi zilizo katika hatari ya maambukizi ya homa ya manjano.
· Kuhakikisha kuwa chanjo za kutosha za ugonjwa wa Homa ya manjano zinakuwepo hapa nchini.
· Kusimamia na kuhimiza usafi wa mazingira ili kudhibiti mazalia ya mbu.
· Kuendelea kutoa elimu ya Afya kwa wananchi kuhusu ugonjwa huu.
Ndugu Wananchi, Wizara inapenda kuwaasa wananchi kuzingatia yafuatayo:
· Kutoa taarifa mapema katika vituo vya kutolea huduma ya afya pale wanapoona mgonjwa mwenye dalili zilizotajwa hapo juu.
· Kutumia vyandarua vilivyotiwa dawa.
· Kutilia mkazo usafi wa mazingira na kuzuia maji yasituame ovyo kwenye mazingira tunayoishi ili kuangamiza mazalia ya mbu katika maeneo yao.
· Kwa wasafiri wanaokwenda nje ya nchi, wahakikishe wamepata chanjo dhidi ya homa ya manjano (Yellow Fever). Huduma za chanjo hiyo zinapatikana katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere (Dar es Salaam), Hospitali ya Mnazi Mmoja, Ofisi za Afya Bandari (Dar es Salaam) na kituo cha Afya cha IST (Dar es Salaam) pamoja na Ofisi za Afya za mipakani.
· Kuwa watulivu na kusikiliza maelekezo na ushauri utakaotolewa na wataalam wa Afya katika maeneo yao au vyombo vya habari.
Ndugu Wananchi, Wizara inaendelea kutoa wito kwa wadau katika ngazi zote kuendelea kushirikiana katika kutekeleza jitihada mbalimbali za kupambana na magonjwa ya milipuko ikiwepo ugonjwa huu kwa kuzingatia kikamilifu miongozo inayotolewa na Wizara.
Wizara inawapongeza na kuwashukuru wataalamu wa Sekta mbalimbali, Wadau wa Maendeleo, Asasi za Kiraia, pamoja na wananchi kwa ujumla kwa michango yao mbalimbali katika kuendelea kudhibiti magonjwa ya kuambukiza nchini. Aidha, Wizara itaendelea kutoa taarifa kwa umma kuhusu mwenendo wa magonjwa ya milipuko nchini.
Imetolewa na:
Ummy A. Mwalimu (Mb)
WAZIRI WA AFYA
No comments:
Post a Comment