Vita vya Ukraine : Tulikaa chumba kimoja na wafu- hali ya kutisha nje ya Chernihiv - KABATA

This is the special room for news where you need to settle with!


Breaking

Friday, 8 April 2022

Vita vya Ukraine : Tulikaa chumba kimoja na wafu- hali ya kutisha nje ya Chernihiv

 

Mykola Klymchuk
Maelezo ya picha,

Mykola na wengine wengi walilazimishwa kwenda kwenye handaki la shule kuondoka kwenye nyumba zao ambako kulikuwa kunalengwa na risasi

Katika ukuta mweupe, katika handaki la shule ya Yahidne kuna kalenda ghafi, iliyochorwa kwa rangi nyekundu. Inaashiria kipindi cha kiwewe kisichofikirika - kuanzia tarehe 5 Machi hadi tarehe 2 Aprili - kwa watu wa kijiji hiki.

Yahidne, iko kilomita 140 (maili 80) kaskazini-magharibi mwa Kyiv na nje kidogo ya jiji la Chernihiv ambalo liko karibu na mipaka ya Belarus na Urusi, ulikaliwa na wanajeshi wa Urusi kwa karibu mwezi mmoja.

Walipoingia, waliwachukua wanaume, wanawake na watoto kutoka kwa nyumba zao wakiwa wamewaelekezea bunduki na kuwaweka katika handaki la shule ya mtaa kwa muda wa wiki nne - karibu watu 130 walibanwa ndani ya chumba chenye ukubwa wa takriban 65 sq m (700 sq ft).

Mykola Klymchuk mwenye umri wa miaka sitini alikuwa mmoja wao. Alijitolea kutuonyesha handaki hiloTuliposhuka katika ngazi fupi, tulianza kusikia uvundo. Chumba kilikuwa kichafu - magodoro kadhaa, nguo, viatu na vitabu vilikuwa vimetapakaa sakafuni, kulikuwa na vitanda vidogo vinne katikati na vyombo kwenye kona moja.

Mykola alitupeleka moja kwa moja hadi mwisho kabisa wa chumba.

"Hii ilikuwa nafasi yangu ya nusu mita. Nilikuwa nikilala nimesimama," alisema. Alishindwa kuongea na kuanza kulia. "Nilijifunga kwenye reli hapa na kitambaa changu ili nisianguke. Nililala hivyo kwa usiku 25 namna hii."

Mykola alisema huwezi kusogea hata kidogo kwa kuogopa kukanyaga watu. Takriban watoto 40 au 50 walikuwa miongoni mwa wale waliotekwa, waliokuepo na watoto wachanga. Mdogo alikuwa na umri wa miezi miwili tu.

Vikosi vya Urusi vilifanya haraka kufikia vijiji kama vile cha Yahidne walipoanzisha mashambulizi yao kwa Chernihiv.

Kwa wiki kadhaa jiji hilo lenye watu wapatao 300,000 lilikatiliwa mbali huku majeshi ya Urusi yakiuzingira na kulishambulia kwa mabomu, baada ya kupata upinzani.

Pia waliharibu daraja katika barabara ya kuelekea mji mkuu wa Kyiv, na kuwaacha wakazi wa maeneo hayo bila pa kukimbilia.

Sasa Warusi wamejiondoa kufuatia kushindwa kwao kuchukua Kyiv.

BBC ni mojawapo ya mashirika ya kwanza ya habari kufika eneo hilo na hofu ya kile kilichotokea chini ya uvamizi na mashambulizi ya mabomu yanaweza kufichuliwa.

Karibu sana na mpaka, watu wana wasiwasi pia kwamba Warusi wanaweza kurudi tena hivi karibuni.

basement in yahidne
Maelezo ya picha,

Watu wapatao 130 walikaa hapo kwa muda wa wiki nne

Anastasiia mwenye umri wa miaka kumi na tano alikuwa katika handaki ya Yahidne akiwa pamoja na baba yake na bibi yake.

"Hakukuwa na chumba chochote. Tulikuwa tunaishi tumeketi. Tulikuwa tunalala tumeketi. Sio kwamba tulilala kabisa. Haikuwezekana. Ilikuwa vigumu," alisema.

Chumba hakikuwa na uingizaji hewa. Dirisha zake mbili ziliwekwa juu.

"Wakati nikiwa hapa, watu 12 walikufa," Mykola alisema.

Kuishi na wafu

Wengi wao walikuwa wazee. Haijulikani walikufa kutokana na nini, lakini Mykola anaamini baadhi yao walikosa hewa hadi kufa.

Watu walipokufa, miili haikuweza kuondolewa mara moja. Wanajeshi wa Urusi hawakuruhusu kila siku. Na kwa sababu ya mapigano ya mara kwa mara nje - makombora ya chokaa, milipuko na milio ya risasi - ilikuwa hatari pia.

Hii ilimaanisha kwamba watu, ikiwa ni pamoja na watoto, waliishi na maiti kwa saa kadhaa, na wakati mwingine siku kadhaa, hadi walipoweza kutolewa nje.

anastasia
Maelezo ya picha,

Anastasiia ana hofu bado na ana msongo wa mawazo kutokana na maisha aliyopitia

"Ilikuwa inatisha sana. Nilikuwa nawajua watu waliokufa," anasema Anastasiia. "Walikuwa watu wema sana. Nilisikitika sana, walikufa tu hapa bila sababu."

"Katika hali ya kawaida, wasingekufa. Putin ni mhalifu wa vita," alisema Mykola.

"Miguu yangu ilikuwa imeanza kuvimba. Lakini niliendelea kujiwazia, lazima nipone, niishi. Ni lazima, kwa ajili ya binti yangu na wajukuu zangu wawili wa kike."

Mara nyingi watu walikuwa hawaruhusiwi kutoka nje hata kutumia choo. Iliwabidi kutumia ndoo badala yake.

"Wakati mwingine askari walichukua watu nje ili kuwatumia kama ngao," Mykola alisema.

Waliruhusiwa kupika nje mara mbili kwa siku. Kijiji kilikuwa na akiba ya chakula cha kutosha na kisima cha maji.

Mmoja wa wanajeshi wa Urusi alimwambia Mykola kuwa wameambiwa watakuwa Ukraine kwa siku nne tu, ambazo zingetosha kuchukua udhibiti wa Kyiv.

Kutafuta wapendwa wao - katika makaburi

Mnamo tarehe 3 Aprili, Warusi waliondoka Yahidne.

Wanajeshi wa Ukraine sasa wako katika kijiji hicho, na wengi wa wale waliokuwa wametekwa wamehamishwa hadi maeneo ya karibu.

"Ninaamka mara nyingi kila usiku. Ninahisi kama ninasikia sauti ya risasi. Ninakimbilia kwa wazazi wangu, nikiogopa," anasema Anastasiia.

Warusi waliteka vijiji kama vile Yahidne karibu na Chernihiv kwa nia ya kuuzingira mji huo na hatimaye kuudhibiti.

Hawakuweza kuingia katika jiji hilo, lakini kumekuwa na uharibifu mkubwa katika maeneo mengi na maafisa wanasema takriban raia 350 wameuawa.

destroyed building in chernihiv

CHANZO CHA PICHA,EPA

Maelezo ya picha,

Mapigano ya anga yaliharibu majengo ya Chernihiv

Tangu Urusi ilipoondoka maeneo ya karibu na Chernihiv, watu wa kujitolea wamekuwa wakifanya shughuli ya kuwazika waliokufa.

Sehemu moja ya makaburi ya eneo hilo sasa imejaa makaburi mapya kabisa, na bango lililowekwa juu ya kila moja, kwa madhumuni ya utambuzi.

Familia ambazo zimetengana zimekuwa zikija kuona ikiwa zinaweza kuona makaburi ya wapendwa wao.

Uwanja wa soka wa eneo hilo ulilipuliwa kwa bomu, maafisa wa Ukraine wanasema na ndege za Urusi.

Kreta kubwa inaweza kuonekana katikati ya uwanja ambapo bomu moja. Lingine liliharibu sehemu ya stendi, ambayo sasa imechafuka kwa viti vya plastiki vilivyovunjika na vya chuma.

Kando ya uwanja huo, maktaba ya watoto iliyo kwenye jengo la kihistoria pia imeharibiwa vibaya.

Tulipokuwa tukiendesha gari katikati ya jiji, tulipita vitongoji kadhaa vya makazi ambayo yameathirika na ushambulizi huo.

chernihiv
Maelezo ya picha,

Baadhi ya maeneo ya jirani ya Chernihiv

Katika Novoselivka, kaskazini mwa Chernihiv, uharibifu unaonekana wazi kabisa.

Kuna mawe na matofali yamepaangwa maeneo ambayo yalikuwa nyumba zao . Tuliona koti la rangi ya pinki la mtoto,mdoli na kipande cha bango linaloonesha njia ya kuingia makazi ya watu.

Njiani, tuliona mashimo zaidi ya mabomu.

'Kwa nini hatukuonywa?'

Mwanamke na mtoto wakiwa kwenye baiskeli walituashiria tuwafuate.

Nina Vynnyk mwenye umri wa miaka sitini na mbili na mjukuu wake, Danylo mwenye umri wa miaka 10, walitaka kutuonyesha nyumba yao - imeharibika kabisa, kila kitu ndani na karibu yake imeharibiwa.

Nina
Maelezo ya picha,

"Hakuna kitu," anasema Nina

Binti yake Nina na mama yake Danylo, Ludmyla mwenye umri wa miaka 39, amepoteza mguu wake na yuko hospitalini.

Nyumba ya Nina ilipoanza kupigwa makombora, walikimbilia kwenye nyumba ya mtu mwingine wakitumaini kutafuta hifadhi kwenye chumba chao cha chini. Lakini huko kulilipuliwa pia.

"Tulipata mshtuko wa milipuko, wengine walijeruhiwa, wengine walipata kiwewe na tuliporudi katika hali zetu, niliona binti yangu anapiga kelele, "Mama, mama, sina mguu." Ilikuwa hali ya kutisha. " alisema.

Ludmyla alitambaa na kupelekwa hospitalini.

"Ninahisi kuwa hali hii ni jinamizi la kutisha. Haiwezi kuwa kweli. Kwa nini serikali yetu haikutuonya? Kwa nini hawakutuhamisha," alisema Nina.

Vizazi vinne vya familia yake viliishi nyumbani. "Kwa wakati mmoja, hakuna kitu kilichosalia. Sijui nitaishi wapi wakati wa baridi," alisema.

Hana uwezo wa kulipia dawa na kulipia mguu bandia kwa ajili ya binti yake.

Kuhusu matamshi ya Urusi kwamba hawajawalenga raia, anasema, "Yeye [Putin] amejaa uongo. Kuna mwanamke hospitalini hana mguu. Huo ndio ukweli.

"Mwacheni Putin amlipe upasuaji wake. Mwacheni Putin ajenge nyumba hii. Aliitaka sana, sivyo? Mwache alipe yote sasa."

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here