Masoko Tanzania yanaungua au yanaunguzwa? - KABATA

This is the special room for news where you need to settle with!


Breaking

Tuesday, 31 May 2022

Masoko Tanzania yanaungua au yanaunguzwa?

 

Kariakoo

CHANZO CHA PICHA,BONGO5

Matukio ya masoko kuungua nchini Tanzania, kwa sasa yanaonekana ni kama matukio ya kawaida, kutokana na kusikika na kutokea karibu kila leo. Mali zenye thamani ya mamilioni ya shilingi zimeteketea na kuathiri wafanyabiashara kiuchumi, kimitaji, kuharibu miundo mbinu ya masoko huku ikiwapa shida ya huduma za masoko maelfu kwa maelfu ya watu ndani na nje ya nchi.

Wiki hii Soko lingine limeungua, soko la Vetenari, lililopo eneo la Tazara, jijini Dar es Salaam ambapo vibanda karibu 453 vimeteketea na kuathiri mamia ya wafanyabiashara.

Kuungua kwa soko hili, ni muendelezo wa matukio mengi ya kuungua kwa masoko nchini humo. Katika miaka 10 iliyopita karibu mikoa yote imeshuhudia soko moja ama mawili yakiungua, lakini mkoa wa Dar es Salaaam, Mbeya, Arusha, Geita na Mwanza imekuwa na matukio mengi hasa katika siku za hivi karibuni.

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita masoko makubwa na ya kati yanayotegemewa na maelfu ya watu katika mikoa hiyo yaliungua. Soko la kimataifa la Kariakoo ambalo ni kubwa kabisa jijini Dar es Salaam, soko la Mitumba la Karume, Mbagala na sasa hili la Vetenari yameteketea.

Tazara

CHANZO CHA PICHA,PERUZ

Maelezo ya picha,

Soko la Vetenari, TAZARA ni la hivi karibuni kuungua nchini Tanzania

Mbeya, ni mkoa mwingine wenye historia ya masoko yake kuungua katika eneo la nyanda za juu kusini, tangu enzi hizo za kuungua kwa masoko ya Sido, Makunguru, Mwanjelwa na soko la Uhindini.

Soko la Mbuyuni huko Moshi mkoani Kilimanjaro liliungua mwaka huu, kama ilivyo kwa soko la Kakubilo CCM mkoani Geita ambalo liliungua Januari mwaka huu, huku nyuma kidogo kwenye mkoa huo huo masoko ya Kariakoo Geita na lile la Katoro yaliungua.

Matukio ya moto ni mengi na maswali ni mengi pia

s

CHANZO CHA PICHA,MICHUZI JR

Maelezo ya picha,

Inaelezwa Mshumaa ulikuwa chanzo cha kuungua soko la Karume

Kama kuna wakati ambao kumekuwa na maswali mengi kuhusu kuungua kwa masoko nchini Tanzania, basi ni wakati huu. Maswali haya yanatokana na kuongezeka kwa matukio ya masoko makubwa na madogo kuunga nchini humo.

Mwenyekiti wa Chama cha ukombozi wa Umma, CHAUMMA, Hashim Rungwe hivi karibuni aliungana na wenye kujiuliza maswali kuhusu matukio haya ya kuungua kwa masoko nchini Tanzania.

'masoko yamekuwa yakiungua sana nchini mnajua kwanini? Nyinyi (waandishi wa habari) kazi yenu mnatangaza tu (waandishi), tunataka kujua kwa nini? kwanini inatokea na (Serikali) haitoi taarifa', anasema Rungwe.

Maswali mengine ambayo wengi wanajiuliza ni kwanini moto hutokea usiku ama alfajiri na mapema, muda ambao hakuna watu, masokono yameshafungwa? Kingine kwanini ripoti za uchunguzi za matukio haya haziko wazi sana?

a

CHANZO CHA PICHA,MTAAKWAMTAA

Maelezo ya picha,

Soko la Mwanjelwa Mbeya likiteketea

Hata hivyo Mamlaka za Tanzania mara kadhaa zimejitokeza akiwemo Rais Samia Suluhu na kutaja sababu kadhaa zinazosababisha matukio ya moto kwenye masoko Tanzania ikiwemo; hitilafu ya umeme, kuwasha mishumaa na moto unaowashwa na kutelekezwa na wapishi kwenye maeneo ya masoko.

Lakini kati ya maswali yote na sababu zote zinazotolewa, swali kubwa linalozunguka kwa wengi ni Je Masoko haya yanaungua kweli kwa sababu hizo au yanaunguzwa kwa makusudi?

Ni ngumu kuwa na jibu la moja kwa moja kwenye swali hili. Lakini unaweza kuwa nafasi ya kutafsiri majibu unayoyasikia kutoka kwa watu wenye mamlaka, wafanyabiashara na wananchi wa kawaida.

Wapo wanaojiridhisha kwamba matukio ya kuungua kwa masoko ni ya kutengenezwa ama kufanyika kwa makusudi kwa malengo wanayoyajua hao wanaofanya hivyo.

Nani yuko nyuma ya pazia kuungua kwa masoko Tanzania?

Licha ya Mamlaka kuendelea kufanya uchunguzi wa kina wa matukio mbali mbali ya moto, ingawa pia ripoti za awali zinaweza kutumika kuthibitisha uhusika na chanzo cha moto, hilo halizuii watu kuendelea na mashaka yao kwa namna ya matukio ya moto kwenye masoko ya Tanzania yanavyotokea na kuendelea kutokea kila leo.

'mashaka ni lazima, haiwezekani kila siku usikie soko limeungua huku, kesho kule, na moto unavyotokea pia inaleta mashaka, yaani ni usiku tu, na huoni nguvu kubwa ya kuudhiti', anasema Yahaya Msakule wa Dar es Salaam.

Mashaka haya, yanatamatisha imani ya watu kwamba, pengine kuna mtu ama watu wanahusika na kinachotokea. Wengine lawama zao ni kwa Mamlaka, wengine uzembe wa watu, wengine ni miundo mbinu, licha ya mamlaka ya Zimamoto kuwahi kusema, inafanya kila inavyoweza kukabiliana na moto kwenye masoko, licha ya changamoto zilizoko, lakini ni nani hasa yuko nyuma ya pazia?

Hili linaweza kuwa gumu kulithibitisha, kutokana na mamlaka zenye mamlaka ya kuthibitisha kutothibitisha pasi na shaka kuhusika kwa kundi fulani ama watu fulani au mfu fulani kuhusika kuchoma soko fulani ama masoko fulani fulani hasa katika matukio ya hivi karibuni.

Samia

CHANZO CHA PICHA,GOOGLE

Maelezo ya picha,

Rais Samia

Lakini Rais Samia Suluhu akizungumza na viongozi wa wamachinga jijini Dae es Salaam mwezi Januari, mwaka huu mbali na kuwafariji wanaoathirika na kuungua kwa masoko hayo hasa wafanyabiashara alisema 'kuna wale ambao labda amekata bima ya biashara yake, lakini kwa miaka kadhaa bima hajafaidi matunda ya bima, kwahiyo anaamua tu ngoja niweke kicheche cha moto hapa, ukiungua , mimi kwa sababu nina bima, nitalipwa na bima, hilo nalo lipo,' .

Hili ni kundi la kwanza, ambalo hata Rais Samia ana mashaka nalo labda pengine linaweza kuwa na mkono wake, ingawa uchunguzi zaidi unaweza kuja kueleza na kuthibitisha.

Rais akataja kundi lingine ambalo linaweza kunyooshewa kidole, 'lakini jengine ni hawa wanaochukua mizigo madukani, inawezekana mtu keshachukua mzigo mkubwa kauza, moyo wa ushetani unamtuma asiende kurudisha, weka moto mwenye duka atajua soko limeungua, kwa hiyo sina chakulipa, mwenye duka labda ana bima, atalipwa huko, kwa hiyo yote haya yanaweza kuwa sababu', alisema Rais Samia.

Kwa mtazamo wa kawaida, ukiona suala mpaka Rais wa nchi analitaja kwa shaka, basi shaka yake hayapaswi kutiliwa shaka. Muhimu sasa ni hatua ya kushughulika na mashaka haya ili kubaini na kuthibitisha hujuma kama zipo, na kuwapa haueni wafanyabiashara kwenye masoko.

Nini kauli ya Serikali kuhusu matukio ya masoko kuungua

Sagini

CHANZO CHA PICHA,IPPMEDIA

Maelezo ya picha,

Naibu waziri wa mambo ya ndani, Jumanne Sagini

Akizungumza hivi karibuni (Mei 10,2022) bungeni mjini Dodoma, Naibu waziri wa mambo ya ndani, Jumanne Sagini alisema Jeshi la zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na vyombo vingine vimebaini kuwa masoko mengi yanaungua moto kutokuwa na uunganishaji holela wa mifumo ya umeme, kutozingatia tahadhari za umeme kwa mama lishe na baba lishe na shughuli za uchomeleaji vyuma.

"Katika kukabiliana na vyanzo vya matukio hayo umefanyika ukaguzi wa kinga wa tahadhari ya majanga ya moto sambamba na utoaji wa elimu na mafunzo ya matumizi ya vifaa vya awali vya kuzima moto katika masoko', alisema

Pamoja na hilo, akasema Serikali inapanga kuboresha miundo mbinu ya zima moto katika masoko na kuhakikisha ramani za masoko mapya zinakaguliwa na zinakuwa na vigezo vya kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto.

Kuna suluhu ya matukio haya ya moto masokoni?

Kariakoo

CHANZO CHA PICHA,MWANANCHI

Maelezo ya picha,

Soko la kimataifa la Kariakoo limepoteza ajira za maelfu ya wananchi waliokuwa na maduka na vibanda kwenye soko hilo kubwa kabisa Dae es Salaam

Hakuna shaka kuwa, matukio ya kuungua kwa masoko Tanzania, kunaleta madhara makubwa ya kiuchumi kwa taifa kwa kupoteza miundo mbinu yake ya thamani na kugharamia ukarabati ama ujenzi wake na watu binafsi wanaguswa na madhara haya wakiwemo wafanyabiashara.

Hata mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla aliwahi kusema wazi kwamba wafanyabiashara wanaounguliwa na bidhaa zao kwenye masoko haya, wapo waliokuwa wamekopa, wapo wanaopoteza mitaji na wapo wananchi wanaokosa huduma ya bidhaa kwenye masoko hayo yanayounguza. Athari ni za wazi lakini nini suluhisho la kudhibiti na kuepusha matukio haya?

Kuanzishwa kwa chombo maalumu cha majanga, kitakachokuwa na jukumu moja tu kubwa la kuratibu shughuli za kujiandaa na kudhibiti majanga katika maeneo mbalimbali nchini humo.

s

CHANZO CHA PICHA,MICHUZI JR

Maelezo ya picha,

Soko la Karume Dar es Salaam hutegemewa zaidi kwa nguo za mitumba lenyewe pia liliteketea usiku

Ofisiya waziri mkuu, inatekeleza jukumu hili, huku matukio mengine kama haya ya moto, Jeshi la Zimamoto likihusika kushugulika nayo, lakini chombo hiki kinaweza kusogeza huduma ya kuratibu na kudhibiti majanga kwa karibu, ili kuwalinda wafanyabiashara na majanga ya moto.

Mwanasiasa mkongwe aliyewahi kuwa kwenye kamati mbalimbali za bunge, James Mbatia alinukuliwa akisema ni muhimu kutekelezwa kwa sheria ya kuanzishwa kwa taasisi ya aina hii. Sheria anayoirejea Mbatia ni ile ya Disaster Management ya mwaka 2015.

"Kwakuwa sheria ya kuanzisha taasisi ya kupambana na kusimamia majanga ipo iliyotungwa mwaka 2015, Serikali inabidi iipe kipaumbele na utekelezaji sheria hiyo kwa kuanzisha taasisi hiyo ya kupambana na majanga," alinukuliwa na mtandao wa nukta Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here