TAARIFA KWA UMMA KUTOKA JESHI LA POLISI MKOANI MWANZA - KABATA

This is the special room for news where you need to settle with!


Breaking

Wednesday, 12 October 2022

TAARIFA KWA UMMA KUTOKA JESHI LA POLISI MKOANI MWANZA

 

JESHI  la Polisi Mkoa wa Mwanza limeendelea na operesheni mbalimbali za  kupambana na uhalifu na wahalifu kwenye maeneo ya nchi kavu na majini kwa nia  ya kuendeleza kudhibiti hali ya utulivu ndani ya Mkoa.  

Katika operesheni za nchi kavu, Jeshi la Polisi lilifanikiwa kukamata simu 118 na  watuhumiwa 8 waliokuwa wanajihusisha na ukwapuaji/uporaji wa simu katika  maeneo mbalimbali ya Jiji la Mwanza. Mafanikio haya ni kutokana na ushirikiano  wa wananchi uliowezesha kumkamata mtuhumiwa aliyekuwa anapokea na kununua  simu za wizi toka kwa watuhumiwa wa wizi wa simu hizo. 

Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama limefanikiwa  kukamata injini 4 za boti, nyavu haramu na watuhumiwa wa makosa mbalimbali ya  uvuvi haramu ndani ya Ziwa Victoria na kwa upande wa barabarani makosa  mbalimbali yameendelea kudhibitiwa na mengine yamekamatwa na kutozwa faini  kiasi cha Tshs 360,167,500/= ambazo zimeingizwa kwenye mfuko wa serikali.  

Hata hivyo, mapambano dhidi ya dawa za kulevya bado yanaendelea ambapo Jeshi  la Polisi Mkoa wa Mwanza limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 8 wa makosa  mbalimbali yanayohusiana na dawa za kulevya na watuhumiwa wote watafikishwa  mahakamani kukabiliana na mkono wa sheria.  

Aidha, Katika tukio lingine tarehe 9 Oktoba 2022 majira ya 16:45 Jioni, huko  maeneo ya hifadhi ya Msitu wa Sayaka uliopo Kata ya Itumbili, Wilaya ya Magu.  Mwanamke mmoja ambaye jina lake linahifadhiwa alikutwa amekatwa sehemu  zake za siri pamoja na chuchu za matiti yake yote mawili na mtu aliyetambulika kwa  jina moja la Masoud, ambaye inadaiwa alikuwa mpenzi wake waliyedumu naye kwa  muda wa miezi miwili.

Uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha tukio hilo ni imani za kishirikina ambapo  mtuhumiwa alimuadaa Mhanga kuwa anaenda kumuonyesha Shamba la dengu  lililopo katika msitu wa hifadhi ya Sayaka na walipofika alimkaba shingoni Mhanga  huyo ambapo ilipelekea kupoteza fahamu na kutekeleza unyama huo. 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linafanya kila jitihada kuhakikisha linamtia  nguvuni mtuhumiwa huyo ili aweze kufikishwa katika vyombo vya dola. Mhanga  wa tukio hilo anaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa Bugando na  hali yake inaendelea vizuri. 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linatoa wito kwa wananchi wote kuendelee kutoa  taarifa za uhalifu na wahalifu ili ziwezekufanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria,  kanuni na taratibu. 

Imetolewa na;- 

Ramadhani H. Ng’anzi – SACP. 

Kamanda wa Polisi (M) Mwanza.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here