Kansela
wa Ujerumani Angela Merkel atafanya mazungumzo ya kwanza leo
(30.11.2017) na mwenyekiti wa chama cha Social Democratic SPD, Martin
Schulz, kuangalia uwezekano wa kuunda serikali ya mseto.
Mkutano
huo unaofanyika chini ya mualiko wa rais wa Ujerumani, Frank Walter
Steinmeier, unatarajiwa kuanza saa mbili usiku saa za hapa Ujerumani na
unatarajiwa kuangalia ikiwa pande hizo mbili ziko tayari kuanza
mazungumzo ya serikali mpya. Baada ya uchaguzi wa mwezi Septemba
kumuacha Merkel bila wingi wa wajumbe bungeni, chama cha SPD kilitangaza
kwa ukaidi kwamba hakitaendelea kushirikiana na kansela huyo, baada ya
kufanya vibaya sana na kupata matokeo ya kuabisha katika uchaguzi huo.
Lakini
baada ya juhudi za Merkel kuunda serikali ya mseto na chama cha walinda
mazingira cha Kijani na chama cha kiliberali kinachowapendelea
wafanyabishara, FDP, kusambaratika, chama cha SPD kilikabiliwa na
shinikizo la kubadili msimamo wake ili kuepusha uchaguzi wa mapema.
Jarida
linalochapishwa kila wiki hapa Ujerumani, Der Spiegel, limedokeza
kwamba mkutano wa leo utakaohudhuriwa pia na Horst Seehofer, mwenyekiti
wa chama cha Bavaria cha Christian Social Union, CSU, ni wa umuhimu
mkubwa kwa mwanasiasa siasa huyo mkongwe. Kwa kansela Merkel "ni vita
vya kupigania mustakabali wake kisiasa ambavyo vinaanza" limesema jarida
la Spiegel na kuongeza kuwa Merkel analazimika kufanya kila kitu kuunda
muungano huu, ambao pekee utahakikisha mamlaka thabiti.
Akizungumzia
mkutano wa leo Schulz amesema kujenga mustakabali mwema kwa Ujerumani
ni jukumu la serikali ijayo. Hiyo haina maana kuongoza nchi bila mpango
wa muda mrefu. Ina maana kufanya mageuzi muhimu ambayo itabidi
yapiganiwe na kujadiliwa kwa kina.
"Kwa
ari nzuri kabisa duniani, siwezi kuwaambia matokeo ya mkutano huu
yatakavyokuwa. Naweza kuwahakikishia jambo moja: kwamba nitapigania
suluhisho bora linalowezekana kwa taifa hili, ambalo chama changu
kinafahamu jukumu lake. Jambo moja ni bayana: Tunahitaji uthabiti,
ushirikiano na mabadiliko."
Schulz
amekuwa chini ya shinikizo la rais Steinmeier na amebadili msimamo wake
wa kutotaka kushiriki katika serikali ya mseto. Ameashiria yuko tayari
kujadili njia itakayoisaidia Ujerumani kuondokana na mkwamo wa kisiasa
ambao umekuwa ukiikabili kwa miezi miwili sasa.
Kikao chakabiliwa na kiwingu
Mazungumzo
ya leo yanagubikwa na wingu la kisiasa lililosababishwa wiki hii na
mwanachama wa chama cha kihafidhina cha CDU, waziri wa kilimo Christian
Schmidt, ambaye alivuka mpaka wa serikali yake na kupiga kura kuunga
mkono dawa ya kuua magugu, glyphosite, yenye utata wakati wa kutano wa
Umoja wa Ulaya. Hatua hiyo ambayo Schmidt anasema aliichukua peke yake,
ilikosolewa kama uvunjaji wa uaminifu na chama cha SPD, ambacho kimekuwa
mshirika mdogo katika serikali ya kansela Merkel tangu mwaka 2013.
Huku
Merkel akijaribu kukishawishi chama cha SPD, hatua ya waziri Schmidt
yumkini ikasababisha athari kubwa kwa mahafidhina. Carsten Linnemann
anayeliongoza shirika la kampuni ndogo na za wastani la chama cha CDU,
amesema suala hili bila shaka litakuwa kikwazo katika mazungumzo ya leo.
Carsten
Schneider, kiongozi wa chama cha SPD bungeni amekiambia kituo cha
televisheni cha ARD kwamba tukio hilo linaonyesha Merkel hana udhibiti
wa jinsi mambo yanavyoendeshwa katika chama chake. Na licha ya kwamba
Schulz amekubali kukaa katika meza ya mazungumzo na Merkel, mpaka sasa
hajaahidi chochote kuhusu uwezekano wa kuundwa serikali nyingine ya
mseto ya mrengo wa kulia na kushoto.
Kansela
Merkel amesita kuunda serikali isiyo na wingi bungeni kutokana na
kuyumba kwa serikali ya aina hiyo. Lakini baadhi ya vyombo vya habari
vya Ujerumani vikivinukuu vyanzo ambavyo havikutambuliwa vimeripoti
kwamba sasa anapendelea chaguo hilo badala ya kufanya uchaguzi wa
mapema, iwapo mazungumzo na chama cha SPD yatagonga mwamba.
No comments:
Post a Comment